Home 2022 June 17 Watoto Wachanga na Watu Wazima!

Watoto Wachanga na Watu Wazima!

Watoto Wachanga na Watu Wazima!

Bwana wetu, Yesu Kristo alimwambia kiongozi mmoja wa ‘kidini’ wa siku zake maneno haya:

“Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3)

Wakristo wote wa kweli wamezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu:

“Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.” (Tito 3:4-7)

Kwa hiyo wao ni wana wa Mungu:

“Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;  na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.” (Warumi 8:16-17)

Watoto ni furaha katika kaya yoyote ile ya kawaida, lakini pia huwa ni janga kubwa pale mtoto ‘anapobaki kuwa mtoto’ – yaani, anapodumaa kimwili, kiakili au katika vyote viwili! Ni janga pia, pale Wakristo wengi, hasa wale waliozaliwa mara ya pili, wanapobaki kuwa watoto wachanga kiroho – yaani, hawakui. Wanajua kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zao lakini hawajachukua hatua yoyote ya maendeleo katika ‘neema’ au katika ‘ujuzi wa Neno’. Kwa waamini kama hao Paulo aliwaandikia ujumbe huu:

“Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?” (1 Wakorintho 3:1-3)

Ndio kusema, wale ambao hawakuwa na maendeleo ya kiroho, waliweza tu kumeng’enya maziwa, au mambo rahisi/mepesi/madogo ya Maandiko, hawa waliitwa “wa kimwili” na “watoto wachanga,” tofauti na wale waamini “wa kiroho” ambao walikuwa wamekua katika neema na kuweza ‘kumeza’ au ‘kubeba’ kweli za ndani zaidi za Neno la Mungu.

Hili si pongezi kwa wale wanaojisifu kila mara kwamba wameridhika na “mambo hayo mepesi,” na kushindwa kujifunza Neno la Mungu, kama 2 Timotheo 2:15 inavyo tuagiza. Mtume Paulo anaandika tena, kwa waamini hao; kwa maongozi ya Mungu maneno haya:

“Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.” (Waebrania 5:12-14).

Mtoto mchanga mpya katika Kristo ni furaha kumpokea na kumtazama, lakini kila Mkristo aliyezaliwa mara ya pili anapaswa kukua kwa kujifunza Neno la Mungu. 1 Petro 2:2 inasema hivi:

“Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”

Utukufu una Yeye KRISTO, Milele na Milele; AMINA.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *