Home 2022 April 21 Uaminifu wa Mungu na Wetu!

Uaminifu wa Mungu na Wetu!

Uaminifu wa Mungu na Wetu!

Watu wengi wanadhani kwamba wokovu ni thawabu ya Mungu kwa wale wanaofanya vyema zaidi katika kuishi maisha mema. Hivyo sivyo ilivyo, kwa sababu Neno la Mungu linasema haya kwa wale wanaookolewa:

“Ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele.” (2 Timotheo 1:9)

Akizungumzia juu ya “wokovu huu ulio katika Kristo Yesu,” Roho Mtakatifu kupitia kwa Mtume Paulo asema hivi:

“Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia.” (2 Timotheo 2:11).

Kwa maneno mengine:

Mwamini, akiiangalia Kalvari vyema, “anakufa pamoja na Kristo.”

Akiutazama Msalaba kwa usahihi, anakuwa akisema: “Hiki si kifo cha Kristo. Yeye hakuwa mwenye dhambi; Hakuwa na kifo cha kufa. Anakufa kifo changu!”

Na hivyo kwa imani anakuwa “amesulubishwa pamoja na Kristo” (Wagalatia 2:20):

“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”

Adhabu ya dhambi zake zote imelipwa kikamilifu, kwani alikufa – katika Kristo, na hivyo pia amefufuka pamoja na Kristo ili “kuenenda katika upya wa uzima” (Warumi 6:3-4):

“Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.”

Haya yote ni matendo ya Mungu, na ni wakati huu tu ambapo mwamini yupo katika nafasi ya kutenda matendo mema ambayo yatampendeza Mungu. Kwa sababu hiyo, Mtume Paulo anaandika juu ya waumini, katika 2 Timotheo 2 maneno haya:

“Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi” (Mstari wa 12).

Wakati huduma ya kila mwamini kwa Kristo itakapopitiwa (itatathiminiwa), wengine kwa hakika, “watapata thawabu,” lakini wengine “watapata hasara,” ingawa wao wenyewe “wataokolewa, lakini ni kama kwa moto” (1 Wakorintho 3:13-15):

“Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Hakika itakuwa ni jambo la aibu sana, katika siku hiyo, kwa Wakristo (Waamini) wasio waaminifu; kumkabili, katika utupu wa mikono yao, Yule ambaye alitoa Yake yote, mpaka akajitoa Yeye Mwenyewe, ili kuwaokoa!

Pamoja na hayo, wokovu unabaki kuwa ni kwa neema; hivyo Mtume Paulo anaharakisha kuhitimisha kauli yake hiyo katika 2 Timotheo 2, kwa kusema maneno haya:

“Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.” (Mstari wa 13).

Hivyo, thawabu zetu kama waumini zinategemea uaminifu wetu; lakini wokovu wetu, asante kwa Mungu wetu, UPO JUU YAKE!

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *