Home 2022 April 05 Fahari Yetu Pekee!

Fahari Yetu Pekee!

Fahari Yetu Pekee!

“Hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo…” (Wagalatia 6:14)

Mtakatifu Paulo wakati fulani alikuwa Farisayo mwenye kiburi, mwenye kujiona kuwa mwadilifu. Katika Wafilipi 3:5-6, anaorodhesha baadhi ya mambo ambayo alijivuna nayo sana hapo kabla:

“Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”

Lakini kila kitu kilibadilika tangu siku ile Bwana alipomtokea njiani akiwa anaelekea Dameski. Ghafla alijiona kuwa mwenye dhambi aliyepotea, na mwenye hukumu mbele za Mungu mtakatifu na alikuwa ameonja neema isiyo kifani ambayo imeweza kushuka kutoka mbinguni na kumwokoa hata mwovu kama yeye. Alitambua sasa kwamba hangeweza kusimama mbele za Mungu kwa HAKI yake, au “kwa miguu yake mwenyewe,” kama wengine wanavyosema. Usalama wake pekee mbele ya kizuizi cha HAKI ya Mungu ulikuwa ni kukimbilia katika Kristo, kama asemavyo yeye mwenyewe katika Mstari wa 9:

“Tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.”

Sasa alijua, kama sisi sote tunavyopaswa kujua, kwamba kwa kweli hakuwa na kitu cha kujivunia kuhusu haki yake binafsi mbele za Mungu, kama alivyosema katika Mistari ya 7-8:

“Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo.”

Baada ya hapo, kwa muda wa maisha yake yote yaliyobakia, Mtakatifu Paulo alijivunia jambo moja tu; nalo ni MSALABA, ambapo Kristo Yesu alikuwa ameteseka vikali hadi kufa kwa ajili ya dhambi zake ili yeye (Paulo) ahesabiwe haki mbele za Mungu. Mengine yote ambayo Mtakatifu Paulo alikuwa anajivuna nayo yalikuwa yamekumbatiwa katika msalaba huo wa Kristo.

Hilo ndilo jambo pekee tunalopaswa kujivuna nalo na kwa mtakatifu mwingine yeyote mcha Mungu anapaswa kuungana na Paulo kwa shauku kusema:

“LAKINI MIMI, HASHA, NISIONE FAHARI JUU YA KITU CHO CHOTE ILA MSALABA WA BWANA WETU YESU KRISTO, AMBAO KWA HUO ULIMWENGU UMESULIBISHWA KWANGU, NA MIMI KWA ULIMWENGU.”

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *