Home 2022 April 01 Hii Ni Kwa Ajili Ya Yesu!

Hii Ni Kwa Ajili Ya Yesu!

Hii Ni Kwa Ajili Ya Yesu!

Wakati fulani huko nyuma, nilipata fursa ya kumtembelea mchungaji fulani mchanga na familia yake ambapo niliona mfano wenye kugusa moyo wa utumishi wa kweli wa Kikristo.

Ulikuwa ni wakati wa kwenda kanisani, wakati mke wa mchungaji huyo alipokitafuta kisanduku kidogo (kibubu) chenye sarafu chache na kumkabidhi kijana wake mdogo wa kiume kibubu hicho. Sarafu kwenye kibubu hicho, ziliwakilisha mapato aliyopokea mvulana huyo kwa kazi alizofanya, tabia nzuri, utii, adabu, n.k.

Kwa umakini mkubwa, mvulana huyo alitafakari yaliyomo kwenye kisanduku na kuchukua kutoka humo sarafu mbili – hii ikiwa ni sehemu kubwa ya yote yaliyokuwemo katika kisanduku hicho. Kisha akanitazama usoni na kusema kwa ujasiri: “Hii ni kwa ajili ya Yesu“.

Tunayakumbuka mambo kadhaa ya Kimaandiko kuhusu kutoa kwa ajili ya Kristo tunapoliangalia tukio hilo ‘dogo’:

  • Kijana huyu mdogo alikuwa tayari amefundishwa wajibu wa kushiriki kwa ‘utaratibu’ katika kusaidia kazi ya Bwana (1 Wakorintho 16:2).
  • Alitoa “kama alivyokusudia moyoni mwake”; hakuna aliyependekeza ni kiasi gani alichopaswa kutoa (2 Wakorintho 9:7).
  • Baada ya kulitafakari kwa umakini, alitoa kama dhabihu (2 Wakorintho 8:9).
  • “Alithibitisha unyofu wa upendo wake” (2 Wakorintho 8:8), kwa maana ilikuwa kwa mapenzi ya dhati, kama yaliyo mapenzi ya kitoto ndio maana alisema: “Hii ni kwa ajili ya Yesu”.
  • Zaidi ya yote, sadaka yake ilikuwa thibitisho hai la himizo la Paulo katika Warumi 12:8: “mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe”. Hakukuwa na mbwembwe, hakukuwa na majivuno, hakukuwa na mihemko yoyote kudhihirisha kwamba alikuwa akifanya mengi kwa ajili ya Bwana; bali alionyesha tu mtazamo sahili na kuwa na unyenyekevu kwamba naye angeweza kujiunga na wengine katika kuunga mkono kazi ya Kristo…!!!

Je! Vipi kuhusu sisi, ambao mara nyingi tumekuwa wagumu tena miaka mingi, hatuwezi kujifunza kutoka kwa huyu watoto?

“Bwana akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu.” (Kutoka 25:1-2)

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *