Home 2022 March 10 Mtume wa Neema

Mtume wa Neema

Mtume wa Neema

Je, unafahamu kwamba Mtakatifu Paulo ndiye aliyechaguliwa na Mungu kuwa mtume wa neema?

Maandiko Matakatifu yanamshudia kuwa:

Alikuwa ndiye mfano mkuu wa Mungu wa neema, yaani “mkuu wa wenye dhambi” watakaokolewa kwa neema (1 Timotheo 1:15-16):

“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.”

Kwake huyo, Mtume wa neema, ulikabidhiwa “usimamizi wa neema ya Mungu” (Waefeso 3:1-2):

“Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu.”

Yeye alitumwa kutangaza “injili ya neema ya Mungu” (Matendo 20:24):

“Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.”

Lakini pia, Mtume Paulo aliandika kweli nyingi zaidi kuhusu neema ya Mungu kuliko mwandishi mwingine yeyote yule wa Biblia; Hata Nyaraka zake zote hufungua au kufunga (au yote mawili) kwa salamu “Neema na iwe kwenu.”

Mtume Paulo ndiye anayetutangazia hivi:

“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” (Waefeso 1:7)

Mtume Paulo ndiye anayetuonyesha, jinsi Mungu alivyoipanga (kuiweka) neema hii, kwa ajili ya waamini tangu katika zama zote zilizopita:

“Ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele.” (2 Timotheo 1:9)

Mtume huyu wa neema ndiye pia anayetuonyesha jinsi neema hii itakavyo kuwa yetu katika nyakati zijazo:

“Ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.” (Waefeso 2:7)

Mtume Paulo pia, ndiye anayetuonyesha jinsi neema hii ya Mungu ilivyo kuu kuliko au kupita dhambi zetu zote:

“Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi.” (Warumi 5:20)

Mtume Paulo anatuonyesha jinsi neema hiyo inavyotupa mwonekano wa wenye haki mbele za Mungu:

“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.” (Warumi 3:23-24)

Mtume Paulo anaonyesha jinsi neema ya Mungu inavyotupa sisi waumini nafasi kule mbinguni (katika ulimwengu wa roho):

“Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” (Waefeso 2:6)

Paulo Mtume anatuonyesha jinsi neema ya Mungu inavyotosha kwa matatizo yetu na inaweza kutusaidia kuishi maisha thabiti ya Kikristo:

“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.” (2 Wakorintho 12:9)

“Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.” (2 Wakorintho 9:8)

Ni nani huyo awezaye kuukataa wokovu huu mkubwa, unaopatikana BURE “kwa neema, kwa njia ya imani” ikiwa ni “zawadi ya kipekee kutoka kwa Mungu”, itupatiayo uzima wa milele…???

Paulo Mtume, anatujuza haya:

“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” (Waefeso 2:8-10)

Sifa na Uweza na Ukuu Vina Yeye Milele Yote; AMINA.

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *