Home 2022 March 10 Maagizo ya Bwana

Maagizo ya Bwana

Maagizo ya Bwana

“Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana” (1 Wakorintho 14:37)

Wakristo wengi wana wazo wasilolielewa kwamba Kristo Yesu alipopaa kutoka Mlima wa Mizeituni kwenda mbinguni, aliacha kusema – yaani, Hakuongea tena! Lakini haliko jambo lolote linaloweza kutusukumia mbali kutoka kwenye ukweli huu usiopingika kwamba Kristo Yesu aliongea tena!

Paulo anasema kwamba mambo aliyowaandikia Wakorintho, na kwa Kanisa – Mwili wa Kristo kwa ujumla wake, yalikuwa ni “maagizo ya Bwana”! Vivyo hivyo, katika waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike, Mtume Paulo anasema, “Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu” (1 Wathesalonike 4:2).

Baada ya Yesu Kristo kupaa mbinguni, Israeli iliendelea katika uasi wake dhidi ya Mungu kwa kukataa huduma ya Roho Mtakatifu kupitia wale wanafunzi kumi na wawili. Hivyo, Israeli ikawekwa pembeni (kando) kwa muda na Mungu (Matendo 7). Kisha Mungu akamwinua mtume mpya – mtume mwingine, na kumpa ujumbe mpya, ujumbe ambao haujawahi kufunuliwa (kutolewa) kabla yake (Matendo ya Mitume 9; Wagalatia 1:11-12): KRISTO ALINENA TENA KUTOKA MBINGUNI!

Kutoka mbinguni Kristo aliyetukuzwa, akiwa katika ENZI YAKE YA SASA, alimpa Mtume Paulo ufunuo mpya kuhusu huduma yake ya mbinguni kwa Kanisa, Mwili Wake. Kwa Paulo, mtume wa Mataifa (Warumi 11:13), zilikabidhiwa amri zake Kristo kwa ajili ya Kanisa, Mwili Wake leo.

Katika nyaraka za Paulo, tunayaona/tunayapata mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu ya Kikristo kwa wakati huu wa kipindi cha maongozi ya neema ya Mungu. Katika nyaraka za Paulo, tunapata mafundisho ya neema ambayo Kanisa limejengwa juu yake na linapaswa kuishi kwayo na kuyashirikisha kwa ulimwengu.

Tambua kwamba maneno ya Mtume Paulo, kama yalivyofunuliwa Kwake na Kristo Yesu, yamesemwa/yameandikwa kama “MAAGIZO.” Hili si neno la kujiamlia ‘kulichukua’ au ‘kuliacha’ – bali ni AMRI! Amri inapotolewa na Mungu, hatutarajii/hatutatarajia tuwe na maamuzi (mjadala) kinyume nayo kwamba tutii au la na kujaribu kuyapatanisha mapenzi yetu na mapenzi yake. Katika vipindi vilivyotangulia (vilivyopita), amri zingine nyingi zilitolewa ambazo zilikuwa halali wakati ule zilipotolewa, lakini siyo kwa ajili ya wakati huu wa leo, na siyo kwa ajili ya utii wetu, sisi Kanisa Mwili wa Kristo.

Angalia chakula, kwa mfano! Biblia inamuamuru mwanadamu kula mboga na matunda tu, kisha inaruhusu kula nyama pamoja na matunda na mboga mboga, kisha inaamuru vyakula fulani fulani tu kuliwa, kisha inaamuru kwamba chakula chochote kinaweza kuliwa. Haiwezekani kuzitii amri hizi zote tofauti tofauti kwa wakati mmoja…!

Kuna na maswala mengine mengi katika Maandiko kama haya, kwa hivyo ni muhimu kuamua ni maagizo gani ambayo Mungu anayataka tuyatii hivi leo sisi Kanisa Mwili wa Kristo. Jibu ni kwamba nyaraka za Mtume Paulo ni MAAGIZO YA BWANA ambayo ndiyo maagizo halali kwa leo chini ya neema ya Mungu.

Na Paulo anasema tuna uhuru wa kula vitu vyote; Hakika kuna uzuri usio kifani, kuishi chini ya neema!

“Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uwongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.” (1 Timotheo 4:1-5)

Utukufu na Wema na Uweza Vina Yeye Milele Yote; AMINA.

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *