Home 2022 January 30 Mbinguni…, Na Nani Ataenda Huko…?

Mbinguni…, Na Nani Ataenda Huko…?

Mbinguni…, Na Nani Ataenda Huko…?

Watu wengi hushangaa wanapogundua kwamba Agano la Kale, ingawa ni kubwa mara tatu zaidi ya Agano Jipya, halina ahadi hata moja kuhusu kwenda mbinguni. Watu wa Mungu, katika nyakati za Agano la Kale, walitazamia kwa hamu dunia iliyotukuzwa, ambayo Masihi akiwa ndiye Mtawala wayo.

Hili lilikuwa hivyo hata wakati Bwana wetu, Yesu Kristo, alipokuwa duniani na liliendelea kuwa hivyo hata baada ya Pentekoste. Mtume Petro, akiwahutubia jamaa zake mara tu baada ya Pentekoste, kimsingi alisema maneno haya: “Tubuni, na Mungu atamshusha (apate kumtuma) Kristo Yesu” (angalia Matendo 3:19-20), lakini Paulo, katika nyaraka zake, anasema kwa uvuvio wa kimungu kuwa: “Amini, na Mungu atakuchukua na kukupeleka huko juu.”

Mtume huyu wa neema anatufundisha kwamba Mungu tayari amewapa waumini katika Kristo nafasi na “baraka zote za kiroho” katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo (Waefeso 1:3; 2:4-6). Na anatufundisha zaidi kwamba katika mwisho wa kipindi hiki cha neema “…Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.” (1 Wathesalonike 4:16-17).

Hivyo Paulo, mtume wa pekee wa Mungu kwa siku zetu, anatangaza kwamba “uwenyeji wetu uko mbinguni” (Wafilipi 3:20) na anaandika pia juu ya “tumaini tulilowekewa akiba mbinguni” (Wakolosai 1:5). Hivyo ndivyo anavyowatia moyo watakatifu wanaoteswa, akisema: “Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo mbinguni” (Waebrania 10:34).

Kwa sababu hiyo, anaandika hivi kuhusu kifo:

“Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.” (2 Wakorintho 5:1)

“Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana.” (Wafilipi 1:21-23)

Sifa na Uweza na Ukuu Vina Yeye Milele Yote; AMINA.

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *