Home 2022 January 19 Imani Dhidi ya Dhana!

Imani Dhidi ya Dhana!

Imani Dhidi ya Dhana!

Neno la Mungu linasema katika Waebrania 11:6 kwamba “pasipo imani haiwezekani kumpendeza”.

Hakuna kitu kitakachomsumbua mwanadamu kama hofu kwamba Mungu anaweza kuchukizwa naye, wala haiko furaha yoyote kubwa inayolingana na kuwa na uhakika kwamba Mungu ameridhika naye…!

Hata hivyo, ni upumbavu kudhani kwamba tunaweza kumpendeza Mungu kwa mambo tunayofikiri kwamba Yeye (Mungu) anayatamani. Inatupasa (sisi); tumpe (Yeye) kile anachosema anakitamani. Tunamshukuru Mungu, kwa sababu si vigumu kuamua hili, kwa kuwa ametuambia, tena na tena katika Neno lake, kwamba ni imani ndiyo anayoitamani zaidi ya yote. ANATUTAKA TUMWAMINI; TUMTAMBUE YEYE KAMA ILIVYONENWA KATIKA NENO LAKE.

Biblia inatuambia kwa kirefu jinsi Mungu alivyotupenda, licha ya dhambi zetu, na akamtoa Mwanawe mbarikiwa afe kwa kutundikwa juu ya mti wa Kalvari ili kuisafisha njia yetu ya kwenda mbinguni, lakini ole ni kwa wale ambao, badala ya kumchukulia Mungu kwa Neno lake, wamegeuka na kuliacha ‘toleo lake tukufu la neema’, na “kujaribu kuithibitisha haki yao wenyewe” (Warumi 10:3).

Wana juhudi katika kutenda “matendo mema” na “kujidhabihu” vya kutosha lakini kwa viwango walivyojiwekea wenyewe, huku wakifikiri kwamba Mungu mwingi wa upendo, bila shaka, atazikubali jitihada zao na hivyo kupuuza dhambi zao. Hii ni dhana, na wala sio imani! Je, Mungu mwenye haki anawezaje kupuuza dhambi? Tunapaswa kumshukuru sana Mungu wetu kwamba, katika upendo wake usio na kifani, Yeye mwenyewe alilipa kwa ajili ya dhambi zetu ili tuwe huru, na kwamba wokovu ni “zawadi kutoka Kwake,” inayopatikana kwa imani pekee.

Kaini alidhani kwamba Mungu angekubali dhabihu yake ya kuvutia badala ya ile iliyowekwa, lakini Mungu alimkataa yeye na sadaka yake. Farao alidhani kwamba angeweza kuvuka Bahari ya Shamu kama Musa, lakini aliangamia katika bahari hiyo, yeye na jeshi lake, kwa kumdharau Mungu. Naamani, mwenye ukoma, alikataa njia ya Mungu ya utakaso, akisema, “Tazama, nalidhania…”, lakini jemadari huyu mkuu alibaki mwenye ukoma hadi alipomkubali Mungu kwa Neno Lake.

Wewe, Je! Utamkubali Mungu katika Neno Lake na kumwamini Kristo kama Mwokozi wako?

“Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu” (Wafilipi 1:9-11)

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *