Home 2021 November 18 Kula na Mfalme!

Kula na Mfalme!

Kula na Mfalme!

“Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu  alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli” (Luka 22:29-30)

Kama unavyoweza kuona kutoka kwenye maneno haya ambayo Bwana wetu, Yesu Kristo, aliwaambia wale mitume kumi na wawili; kula pamoja na Mfalme kunahusishwa pia na kutawala pamoja Naye. Tunaona wazo hilo hilo pia, katika maneno ya Bwana kwa Wayahudi wakati wa Dhiki Kuu ambao watahitajika kushinda jaribu la kuchukua/kupigwa chapa ya mnyama ikiwa watataka kutawala pamoja na Kristo katika ufalme wake wa mbinguni, hapa duniani:

“… Mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi…” (Ufunuo 3:20-21)

Kama bado unaendela kushangaa kwamba, kunaweza kuwa na uhusiano gani kati ya kula na mfalme na kutawala pamoja naye; tambua kwamba mezani pa mfalme palikuwa ni mahali ambapo mambo ya kifalme yalikuwa yanajadiliwa!

Tunaona uhusiano huu kati ya kula na kutawala ukifananishwa na hadithi ya Mefiboshethi. Ikiwa utakumbuka, baada ya Daudi kuwa mfalme wa Israeli, alitaka kuonyesha wema kwa washiriki wowote wa nyumba ya Sauli ambao angeweza kuwapata (2 Samweli 9:1). Mefiboshethi alipoletwa kwake (mstari wa 2-6), Daudi akamwambia;

“… Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima” ( 2 Samweli 9:7)

Daudi alifanya hivyo, alimpa Mefiboshethi “mali yote iliyokuwa ya Sauli na nyumba yake” (mstari 9), na kumbuka, Sauli aliwahi kuwa mfalme wa Israeli. Kwa maneno mengine, Mefiboshethi alipewa urithi wa mfalme, na alialikwa kuketi mezani pa mfalme na kutawala pamoja naye “kama mmojawapo wa wana wa mfalme” (mstari 11). Heshima kubwa imetolewa kwa mjukuu wa mtu ambaye hapo awali alikuwa ni adui mkubwa wa mfalme wa sasa!

Watu wengine wanaweza kuichukulia heshima kubwa kama hiyo kuwa ni kitu rahisi tu, lakini haikuwa hivyo kwa Mefiboshethi! Baadaye alimwambia Daudi maneno haya:

“… Jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi? (2 Samweli 19:28)

Mefiboshethi alitambua kwamba alikuwa amepewa heshima kubwa sana kiasi kwamba alihisi hakuwa na haki nyingine ya kumwomba mfalme wake jambo lolote tena.

Sasa, wewe je? Nikukumbushe tu hapa kwamba, kile mfalme Daudi alichomfanyia Mefiboshethi ndicho hasa ambacho Mfalme wako amekufanyia wewe! Mungu “alitufufua pamoja” na Kristo, “na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu,” (Waefeso 2:4-6); sisi ambao hapo awali tulikuwa washiriki wa familia ya “adui” wa Mungu (Warumi 5:10). Kama vile Bwana alivyowaalika watakatifu katika ‘ufalme’, kuketi na kutawala pamoja Naye katika ufalme wa Baba Yake; Paulo anatuambia kwamba, nasi tunaoiamini kazi kamilifu ya Msalaba wa Kristo, kuwa tumealikwa kuketi na kutawala pamoja na Kristo katika ufalme wa Baba yake mbinguni – yaani, kuketi pamoja Naye katika kiti chake cha enzi! Akimzungumzia Kristo, Paulo anasema kwamba Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, na pia akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa – Mwili Wake” (Waefeso 1:22-23). Kwa kuwa Mungu “anayataja yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako” (Warumi 4:17), hivyo tayari umeketishwa pamoja na Kristo, katika ulimwengu wa roho, kwenye mkono wa kuume wa Baba, na HAKIKA siku moja utatawala pamoja naye juu ya malaika (1 Wakorintho 6:3).

Katika kuyatafakari hayo, unaweza kunung’unika na kulalamika juu ya nafasi yako katika maisha, au unaweza kufurahi katika nafasi yako mbinguni, na pengine kuungana na Mefiboshethi kujiuliza kama una haki ya kuomba chochote cha ziada kutoka kwa Mungu zaidi ya kile ambacho Yeye tayari amekifanya katika kukupa urithi wa Kifalme (Waefeso 1:11) na kukuketisha kwenye meza ya Mfalme “kama mmoja wa wana wa mfalme” (rejea Wagalatia 4:4-7)!

“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”

Nina uhakika mfalme Daudi angeweza kumpa Mefiboshethi chochote alichokiomba, lakini moyo wa Mefiboshethi ulijaa shukrani kiasi kwamba alihisi hana HAKI ya kuthubutu kuomba tena chochote cha ziada. Pamoja na ukweli kwamba, tunalo agizo lililo wazi kutoka kwa Mungu kupitia kwa Mtume Paulo kwamba “haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6), lakini kabla ya kumwomba Mungu jambo lolote, inaweza ikawa ni busara kujifanyia “tathimini ya Mefiboshethi” katika kiwango chako cha shukrani…

Hata hivyo; hata kama Mungu hatakufanyia jambo jingine lolote lile la ziada kwa ajili yako, yale ambayo tayari amekufanyia katika Kristo; MUNGU AMEFANYA VYA KUTOSHA…!!!

Kwa Utukufu Wake Kristo Yesu

Author: Festus Patta

7 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *