Home 2021 November 06 MFANO WA ONESIFORO!

MFANO WA ONESIFORO!

MFANO WA ONESIFORO!

“Bwana awape rehema wale walio wa mlango wake Onesiforo; maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu” (2 Timotheo 1:16)

Katika aya iliyoitangulia hii, Paulo alimpa Timotheo maagizo haya:

“Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, WALA usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu” (mstari wa 8)

Kufuatia changamoto hii, Paulo alimkumbusha Timotheo juu ya wale ndugu wa Asia ambao walimwonea aibu na kumuepuka yeye Paulo, mfungwa wa Bwana:

“Waijua habari hii, ya kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene” (mstari wa 15)

Baada ya kumkumbusha Timotheo juu ya picha hii mbaya ya kukosekana kwa uaminifu, Paulo hata hivyo; anauleta mfano mzuri wa uaminifu na wa kipekee, kinyume na ule wa wale wa Asia: Onesiforo, mtu ambaye “hakuuonea haya” mnyororo wake (mstari wa 16).

Onesiforo ni mfano muhimu sana kwa Kanisa, kwa sababu wako waumini wengi sana wanamuonea aibu Paulo leo. Hawataki kushirikiana naye au ujumbe wake ambao Kristo Yesu alimkabidhi; ujumbe wa Injili ya Neema ya Mungu. Wengine huchagua kufuata mafundisho yaliyopo ya dhehebu lao na wengine wameamua kumfuata Petro badala ya kumfuata Paulo (1 Wakorintho 11:1). Walakini, Onesiforo ni mfano wa kutia moyo na ni mfano wa kuigwa na kila mmoja wetu hasa kwa ule ujasiri wake wa kuamua kusimama na Mtume Paulo. Na haya ndiyo mapenzi ya Mungu.

“Bali, alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii akanipata” (2 Timotheo 1:17)

Onesiforo alifanya kuwa ni jukumu lake kumtafuta Paulo huko Rumi. Waumini walikuwa wakishutumiwa kwa uwongo, walijaribiwa, na kuteswa hadi kufa huko Rumi wakati huo, lakini bila kujifikiria yeye mwenyewe, na bila kumuonea aibu Paulo, Onesiforo alihatarisha maisha yake, na kwa bidii akipita katika magereza mbalimbali, moja baada ya lingine mpaka pale alipomkuta Paulo.

Wale wa Asia waliomwacha Paulo walionyesha mfano wa sifa ambazo Paulo alimwonya Timotheo dhidi yazo: woga na aibu. Kinyume chake, Onesiforo alionyesha sifa ambazo Paulo alimwelekezea Timotheo na Mwili wa Kristo: “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” (mstari wa 7).

Bwana na ampe kuona rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana” (2 Timotheo 1:18)

Paulo, akiwa mfungwa katika kifungo cha kifo, hakuweza kumlipa chochote rafiki yake huyo katika Kristo, kwa msaada wake wote huo; Lakini Bwana angeweza! Na kwa sababu ya huruma hiyo, ambayo Onesiforo alikuwa ameionyesha, Paulo aliomba kwamba Bwana amwonyeshe Onesiforo rehema na kumlipa “katika siku hiyo“, siku ya Kiti cha Hukumu cha Kristo (2 Wakorintho 5:10). Onesiforo ni ukumbusho kwetu kwamba, katika siku hiyo, mtu atapewa thawabu ya uaminifu na msimamo wa bila aibu wa ujumbe wa neema ambao Kristo alimkabidhi Mtume Paulo:

“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya”

Kwa Utukufu Wake Kristo Yesu

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *