Home 2021 November 01 Neema ni Nini?

Neema ni Nini?

Neema ni Nini?

“Baba wa uwongo” sikuzote huchukia ukweli, lakini hapingi kwa kutumia njia zilezile mara zote. Ikiwa atashindwa kufanikiwa kwa kunguruma kama simba, anaweza kujionesha kama malaika wa nuru, akiwarubuni waliojikinai kwamba hakika Mungu wa upendo hatawahukumu milele wanaomkataa Kristo. Atashindana kutetea kwamba, watenda-dhambi, hawawajibiki kwa dhambi zao, kwani Waefeso 1:11 si inatuambia kuwa “[Mungu] hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake”? Na kwa hiyo Mungu Mwenyewe anapaswa kuwa na wazo la kuiona dhambi kama “njia ya neema ili kuufikia mwisho wenye utukufu,” na kwamba Yeye ndiye amesababisha mwanadamu kuanguka katika dhambi ili hatimaye amwokoe kutoka kwayo!

Kwa nini Mungu mweza wa yote, mwenye hekima yote, na mwenye upendo wote aliruhusu dhambi kuingia katika ulimwengu? Lazima, kwa sasa, hilo libaki kuwa fumbo lisilopenyeka kwetu, lakini jambo moja ni la hakika: Yeye si mwanzilishi wa dhambi, na kamwe hawezi kuwajibika kwa sababu ya dhambi hiyo – isipokuwa; katika neema na pendo, Alibeba adhabu yake kwa ajili ya mwanadamu.

Mungu huwaita watenda-dhambi kuwa ni “wana wa kuasi” na “watoto wa hasira” (Waefeso 2:2-3), akieleza kwa lugha iliyo wazi zaidi kwamba anachukia dhambi na kwamba hasira yake inawaka dhidi yake (Warumi 1:18; Waefeso 5:6; Yohana 3:36):

“Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu”

“Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi”

“Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia”

Lakini ikiwa Mungu alikusudia mwanadamu atende dhambi na kumsababisha atende dhambi; Je! Ni kwa namna gani mwanadamu hakuwa mtii na ni sababu ipi ingemfanya Mungu kuwa na hasira? Wale ambao wanahamisha jukumu lao la dhambi kutoka kwao wao wenyewe na kumsogezea Mungu, wanapaswa kukumbuka kwamba Yeye alitangaza viwango vyake vya uadilifu katika Sheria “ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu” (Warumi 3:19)

Mabishano ya kwamba wote hatimaye wataokolewa yanaweza kusikika mwanzoni kama neema iliyopindukia, lakini kwa kweli hakuna hata chembe moja ya neema ndani yake, kwa sababu imejengeka katika nadharia kwamba ‘kwa kuwa Mungu alituingiza katika dhambi ni haki pia kwamba Yeye atuokoa kutokana na adhabu yake.’

Lakini neema ni rehema na fadhili za Mungu kwa wasiostahili. Katika Waefeso 2, baada ya kuwaita watenda-dhambi “wana wa kuasi” na kwa hiyo “watoto wa hasira”, Mtume Paulo aendelea kusema:

“LAKINI MUNGU, kwa kuwa ni MWINGI WA REHEMA, kwa MAPENZI YAKE MAKUU aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, KATIKA KRISTO YESU; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe WINGI WA NEEMA YAKE UPITAO KIASI KWA WEMA WAKE KWETU SISI KATIKA KRISTO YESU” (Waefeso 2:4-7)

Kwa utukufu Wake Yesu Kristo

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *