Home 2021 September 14 Biblia Ni Kwa Ajili Yako!

Biblia Ni Kwa Ajili Yako!

Biblia Ni Kwa Ajili Yako!

Kwa kadiri tunavyoichunguza Biblia jambo linajitokeza dhihiri na kwa msisitizo wa uwazi zaidi ni kwamba: Biblia iliandikwa kwa ajili ya watu; kwa ajili ya watu wote kwa ujumla wake, na wala sio kwa ajili ya ‘kundi maalumu’ tu la watu kati yao, kama ambavyo inaonekana leo.

Mtume Paulo alizielekeza nyaraka zake kwa “waumini” na “wachungaji”:

“Kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo” (Warumi 1:7)

“Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu” (1 Wakorintho 1:2)

“… Kwa makanisa ya Galatia” (Wagalatia 1:2)

“… Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi” (Wafilipi 1:1),

na kadhalika…

Hata kipindi kile Paulo alipohubiri injili huko Beroya wasikilizaji wake ‘hawakulibeba kijuu-juu’ neno lile kutoka kwa mtume huyu mkuu, bali “waliyachunguza Maandiko kila siku, ili waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo”, na kwa sababu hiyo Mungu aliwaita “waungwana” (Matendo 17:11). Hakika, hawa walikuwa waungwana wa kweli wa kiroho wa siku zao, na hayo ndiyo maagizo kwa Kanisa leo, sawasawa na 2 Timotheo 2:15. Bwana wetu, Yesu Kristo, wakati ule akiwa duniani, aliwahimiza – na hata kuwatia changamoto wasikilizaji wake kuwa “wayachunguze Maandiko” wenyewe ili waweze kuona jinsi maandiko hayo wanavyomshuhudia Yeye na si vinginevyo (Yohana 5:39).

Kimsingi, kwa kuwa Mungu amejifunua mwenyewe na mpango Wake wa wokovu katika Neno lake lililoandikwa; sote tunawajibika, kila mmoja wetu kwa ajili yake mwenyewe, kusoma Maandiko. Angalia kwa mfano; Wakati ule, yule Tajiri alipomsihi Ibrahimu amruhusu Lazaro aende kuwaonya ndugu zake watano juu ya matisho ya mateso ya Kuzimu, Abraham alimjibu kwa kusema: “Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao” na yule Tajiri aliposisitiza kwamba neno kutoka kwa mtu atokaye kwa wafu (Lazaro) litafaa zaidi nao (hao ndugu zake) watatubu, Ibrahimu naye alimjibu kwa kusisitiza kwamba: “Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishika hata mtu mmoja akifufuka katika wafu” (Luka 16:29-31).

Usimtegemee sana mchungaji wako akutafsirie Maandiko bali ‘jionee’ wewe mwenyewe yanasemaje, kwani siku inakuja ambapo “kila mmoja wetu atatoa hesabu zake mwenyewe kwa Mungu” (Warumi 14:12), na ‘haitatosha’ katika hiyo siku kusema: “Lakini Mchungaji wangu ndivyo alivyoniambia…” – Hilo ni lako, peke yako! Kumbuka; Unalo jukumu la “kuyachunguza Maandiko” wewe mwenyewe ili uweza “kuona mambo hayo ndivyo yalivyo.”

Kwa Utukufu Wake Yesu Kristo

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *