Mitume 12 na Paulo
Katika kulinganisha huduma ya mitume kumi na mbili na ile ya Mtume Paulo, ni lazima tuchunguze kwa uangalifu sana, haya yafuatayo:
Wale kumi na wawili walichaguliwa na Kristo akiwa DUNIANI (Luka 6:13) wakati ambapo Paulo alichaguliwa baadaye na Kristo akiwa MBINGUNI (Matendo ya Mitume 9:3-5; 26:16).
Kabla ya uongofu wa Paulo wale kumi na wawili walikuwa wanamjua Kristo akiwa DUNIANI tu (1 Yohana 1:1). Hata wakati wa kupaa kwake mbinguni, walichokiona ni: “wingu likimpokea kutoka machoni pao” (Matendo 1:9) na hata wale malaika wawili waliojitokeza wakati wakiwa katika mshangao wao wa jambo hilo; waliwaambia hivi: “… Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni…”; kana kwamba ‘alibebwa na upepo wa kisulisuli’. Lakini Paulo alimjua Kristo akiwa MBINGUNI tu, kwa kuwa hakuwahi kumuona akiwa hapa duniani (Matendo 26:16; 1 Wakorintho 15:8).
Wale kumi na wawili waliwakilisha taifa lao. Namba kumi na mbili haina uhusiano wowote ule na “Mwili mmoja” wa Kristo. Kama tujuavyo, Mzee Yakobo wa zamani; mwana wa Isaka, mjukuu wa Ibrahimu, “aliwazaa mababu kumi na wawili”, wazee wa Israeli (Matendo 7:8). Kutoka kwao yalitokea makabila kumi na mawili ya Israeli. Makabila haya yalikuwa na wakuu kumi na wawili juu yao, wakuu wa kabila za baba zao; nao ndio walikuwa vichwa vya wale maelfu ya Israeli (Hesabu 1:16). Hata wakati ule ambapo Israeli ilitawaliwa na wafalme, bado kulikuwa na wakuu hao kumi na wawili (maakida wa kabila za Israeli) – mmoja juu ya kila kabila (1 Mambo ya Nyakati 27:16-22). Hivyo, Bwana wetu, Yesu Kristo, alipokwenda kutangaza “injili ya ufalme” kwa Israeli, aliwachagua wakuu kumi na wawili kwa viti vya enzi kumi na viwili katika ufalme ujao (Mathayo 19:28).
Kwa upande mwingine, Paulo, kama mtume mmoja, anawakilisha “Mwili mmoja,” Kanisa la leo (Warumi 12:5; 1 Wakorintho 12:13; Waefeso 4:4). Kwa sababu alikuwa vyote, mzaliwa wa Kiebrania na mzaliwa wa Kirumi, aliwakilisha wote, Wayahudi na Wayunani walioamini, “waliopatanishwa… na Mungu katika mwili mmoja kwa msalaba” (Waefeso 2:13-18).
Wale kumi na wawili walitumwa kutangaza ufalme wa Kristo (ufalme wa mbinguni) kuwa “umekaribia” (Mathayo 10:7), na baadaye ‘kutoa ofa’ ya kuanzishwa kwake duniani (Matendo 3:19-26). Lakini Paulo alitumwa kutangaza “injili ya neema ya Mungu” (Matendo 20:24), wakati kuanzishwa kwa ufalme ‘kukiwa kumeshikiliwa’.
Huduma ya wale mitume kumi na wawili ilijengeka juu ya ahadi za agano (Isaya 60:1-3; Luka 1:70-79; Matendo 3:22-26). Huduma ya Paulo haikujengeka juu ya ahadi za agano, bali ilijengeka juu ya neema ya Mungu tu kupitia Kristo (Warumi 3:21-28; 5:20-21; Waefeso 1:6-7; 2:7; n.k).
Kwa Utukufu Wake Kristo
Leave a Reply