Home 2021 July 06 JE! HAMKUSOMA?

JE! HAMKUSOMA?

JE! HAMKUSOMA?

Ni Yesu ndiye aliyeuliza swali hilo. Alitarajia watu wa wakati wake kumjibu swali hilo. Vivyo hivyo, anatarajia nasi leo kumjibu swali hilo: Je! Hatukusoma?

Swali hili Yesu aliliuliza mara sita (6) wakati anahudumu katika mwili na linapatikana kwenye Biblia zetu katika Mathayo 12:3, 5; 19:4; 22:31; na Marko 12:10, 26, kama ilivyoonyeshwa hapa chini:

“Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe?”

“Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia?”

“Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke”

“Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu …”

“Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni”

“Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?”

“Je! Hamkusoma?” Kila wakati Yesu alipouliza swali hili alikuwa akitoa hoja muhimu kuhusu Maandiko. Kila wakati, ilikuwa ni katikati ya mabishano ambayo yalimfanya aliulize swali lake hilo.

Je! Yesu angeweza kutuuliza swali hili leo kama nasi tukiwa katikati ya mabishano yenye utata juu ya mada ya Kibiblia? Yesu bila shaka angetusikia tukileta hadithi na nasaba zisizo na ukomo, tukisema “Sawa, nadhani hii ni…” au “Sioni ni kwanini hii …” Na kisha Yesu angekuja na swali lake hilo na kutuuliza, “Je! Hamkusoma?”

Wakati huu tulionao, ni wakati wa maendeleo makubwa ya ‘kidigitali’, nami nashangaa ni wangapi kati yetu tuna maandishi ya Biblia kwenye vifaa vyetu vya kielektroniki tulivyonavyo? Tunaishi katika ulimwengu wa “simu za viganjani” – iPads, Kindles na Smartphones!

Kusoma kitabu (kitabu – baadhi yenu mnaweza kukumbuka ni nini hasa maana yake; ni kile kitu chenye kifuniko na kurasa halisi ambazo unaweza kuzigusa na kuzigeuza kwa mkono) ambazo sasa zinaonekana kana kwamba zimepitwa na wakati na ni za zamani.

Hakuna ubaya wowote na ujio wa teknolojia mpya. Kabla ya Biblia kuwa katika mfumo wa kitabu, ilikuwa katika mfumo wa hati zilizoandikwa kwa mkono (scroll). Kurasa zilizochapishwa ulikuwa ni uboreshaji mzuri dhidi ya hati zilizoandikwa kwa mkono! Pamoja na ukweli kwamba hakuna kitu kibaya juu ya teknolojia tuliyonayo, lakini kuna kitu juu ya hisia ya kushika kitabu mkononi na kufungua kurasa zake ambayo haitabadilishwa na media za elektroniki.

Neno lililoandikwa ni zana muhimu ya mawasiliano. Lakini neno lililoandikwa halina maana bila ya kuwa na uwezo wa kulisoma – na bila ya kuwa na nia ya kulisoma.

Nadhani wengi wetu ambao tumefaulu kupita darasa la nne tuna uwezo wa kusoma na kuelewa – kwa kiwango kikubwa au kidogo.

Swali linabaki kuwa ni kama tuko tayari kusoma au la. Je! Tunaweza kutumia muda wetu vizuri katika kuweka juhudi zinazohitajika kusoma kwa ufanisi – au sisi tutabaki kufanana na wengi ambao wanapendelea na wameweka juhudi zao katika “kutazama tamthilia”?

Swali hili la Yesu ni jambo linalotupa changamoto na kutuhoji juu ya tabia yetu ya usomaji na uelewa wetu juu wa kile tunachokisoma.

Fundisho

  1. Mungu ametupa neno Lake tusome.

Kwa nini Mungu alifanya hivyo?

  • Kwa sababu neno lililoandikwa ndio njia pekee anayotumia kuwasiliana nasi.
  • Anazungumza tu kupitia neno lililoandikwa (ingawa waalimu wa uwongo wanapinga hilo), na sio kupitia ndoto, maono au uzoefu! Waebrania 1:1-2; Waefeso 3:3-5; 1 Wakorintho 14:37.
  • Angalia kwa uangalifu Mathayo 22:31. Yesu alisema, “… hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu…?” Alikuwa akimaanisha kile Musa alichokiandika katika kitabu cha Kutoka 3:6. Tunahitaji kuelewa kwamba maneno yaliyonenwa/yaliyoandikwa na Musa hayakuwa ni maneno yake Musa. Kulingana na Yesu, maneno ya Musa katika Maandiko yanaonyesha kile Mungu anazungumza na mwanadamu.

Yesu anataka kujua ikiwa hawa watu wamekuwa wakisoma yaliyosemwa na Mungu. Kwa wazi, walikuwa hawajasoma. Wanadamu wanapokataa kusoma Biblia, wanakataa kumsikiliza Mungu.

  1. Mungu anatutarajia kusoma neno Lake.

Hiyo yanaonekana kutokana na swali la Yesu, “Je! Hamkusoma?”

  • Kuna matarajio katika swali hilo. Lakini usidhani kwamba matarajio hayo yalikuwa ni kwa viongozi wa kidini wa Kiyahudi tu. Ilikuwa ni kwa wote – kwa wababa na wamama na wana na mabinti, (Kumbukumbu la Torati 6:4-9).
  • Timotheo aliagizwa “afanye bidii katika kusoma”, 1 Timotheo 4:13. Hii itajumuisha kusoma kwa namna zote, hadharani na faraghani.

Je! Unajua kuna baraka zilizotamkwa juu ya msomaji wa Maandiko? Angalia Ufunuo 1:1-3.

  1. Mungu anatutarajia kuelewa kile tunachosoma.

Yesu aliwakemea Masadukayo kwa makosa yao kwa sababu hawakujua maana ya Maandiko!

“Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko…” (Mathayo 22:29).

  • Pale ambapo hatujui Maandiko, tutafanya makosa mengi!
  • Ni wazi kwamba Masadukayo wa wakati ule walikuwa wako sawa tu na “Masadukayo” wengi wa sasa – ambao wamekuwa wakirudia-rudia tu yale waliyoyasikia kutoka kwa watu wengine juu ya mambo mengi ya imani bila ya wao kuyasoma. Utawasikia wakisema – “Wokovu ni kwa imani pekee”, lakini ukiwauliza maana hasa ya hicho walichokisema, hawawezi kukielezea! Hayo ni Makosa, ni makosa, ni makosa, tena ni makosa makubwa kabisa! Tatizo la Mafarisayo halikuwa ni kushindwa kusoma, bali KUELEWA WALICHOKISOMA…
  • Neno “makosa” (error) linamaanisha “kupotea, kudanganywa, au kutangatanga.”

Neno la Mungu lililoandikwa linaweza kusomwa na kueleweka – angalia Waefeso 3:3-5. “… myasomapo, mtatambua…”

  • Je! Tunayo shida ya kushindwa kuelewa baadhi ya mambo? Jibu lipo katika kuomba msaada kwa wengine wanaojua, wakupe ufafanuzi sahihi wa maandiko; na kuuliza sio jambo la aibu. Rejea habari za Filipo na Towashi wa Ethiopia katika Matendo 8:30-35.
  • Je! Ni jambo la aibu kutokujua yale ambayo Maandiko yanafundisha? Wala! Maana kila mtu huanza safari ya maisha ya kiroho akiwa hajui neno la Mungu sawasawa. Lakini ni jambo la aibu zaidi kubaki hivyo hivyo, katika ujinga, katika kipindi chote cha kuishi katika imani.
  1. Mungu anatutarajia tutii kile tunachosoma.

Angalia ubishi katika Mathayo 19:3. Yesu aliuliza, “Je, Hamkusoma…?”

  • Hakika Mafarisayo walikuwa wamesoma Mwanzo 1:27; 2:24, aya ambazo zilizonukuliwa na Yesu.
  • Lakini swali lao kwa Yesu juu ya talaka lilionyesha hawakuwa na moyo wa imani kutii mapenzi ya Mungu. Kama wanaume wengi walivyo leo, walitaka talaka iwe halali, na walitaka iwe halali kwa sababu yoyote ile ambayo wao wangeweza kuiota.
  • Baada ya kusikia jibu ambalo Yesu alitoa, (Mathayo 19:3-6), wao walibishana naye katika jaribio lao la kutaka kujipatia haki ya kutoa talaka kwa sababu yoyote ile (Mathayo 19:7-9)!

Yesu anatulazimisha leo, sisi sote tujiulize, “Kwa nini tunasoma Maandiko?” Je! Tunasoma ili kujihalalisha wenyewe? Au tunasoma neno la Mungu ili kuliamini na kulitii?

Je! Yesu angeweza kusema nini juu ya tabia yako ya usomaji? Mtu mmoja angeweza tu kujibu kuwa, “Sihitaji kusoma Biblia; ilimradi tu yupo mchungaji anayeisoma na kuielewa vyema na hivyo kuifundisha sawasawa, basi mimi niko SAWA.”

Si vyema kujisifia, lakini Bwana ametupa neema ya kuwa wahubiri wanaosoma Maandiko; na Roho wa Kristo ametupa uangazio katika hayo – kisawasawa; lakini ni lazima tukuelimishe kwamba imekupasa kusoma!

Watu wengi sana wanamwamini mhubiri ili kupata haki. Jipatie haki yako mwenyewe – kisha uwe na utii kwa yale unayosoma!

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

6 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *