Home 2021 June 28 IMANI NI NINI HASA???

IMANI NI NINI HASA???

IMANI NI NINI HASA???

Imani ni moja ya hazina ya thamani sana ambayo mtu anaweza kuwa nayo. Ni jambo la kusikitisha kwamba ni wachache sana wanaofahamu yale ambayo Biblia inafundisha juu yake.

Imani mara nyingi inachanganywa na dhana, matumaini, dhamira, ushirikina na mawazo. Kimsingi, kuwa na imani ni kuamini tu; Husasani, kumwamini Mungu na kile anachokisema katika Neno lake! Hii ndiyo sababu tunasoma katika Warumi 4:5 kuwa:

“Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki”

Ni jambo lililo wazi kuwa, imani inamheshimu Mungu, wakati kuwa na mashaka na Neno Lake ni dhahiri kuwa kunamdhalilisha Yeye na hilo ni jambo lisilompendeza daima. Mtume Yohana aliandika:

“… Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe” (1 Yohana 5:9b-11)

Haishangazi kwamba tunasoma katika Waebrania 11:6 maneno haya:

“Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”

Lakini kwa nini Mungu aliitoa sheria, ikiwa wokovu unaweza kupatikana kwa imani tu? Mtakatifu Paulo ana majibu haya:

“Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani” (Wagalatia 3:24)

“Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria” (Warumi 3:31)

Tunapaswaje, sisi sote, kuwa na shukrani sana kwamba, Mungu katika Biblia, ametuambia juu ya ukombozi kupitia Kristo na jinsi tunavyoweza kuokolewa kwa kuwa na imani kwake?

“Ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki. Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 4:25; 5:1)

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *