Home 2021 June 26 Kanisa Ni Nini?

Kanisa Ni Nini?

Kanisa Ni Nini?

Ni ajabu lakini ni kweli kwamba watu wengi – hata wengi kati ya watu wa dini – hawajui kanisa kuwa ni nini. Muulize mtu yeyote wa kawaida kwamba kanisa ni nini, naye atakujibu kirahisi tu kuwa: “Mtu yeyote anajua hilo! Kanisa ni jengo ambalo watu huenda kumwabudu Mungu!”

Lakini hilo sio sahihi. Neno lililotafsiriwa kanisa, katika Biblia zetu, linamaanisha tu ‘kusanyiko’. Kanisa sio jengo, bali ni kusanyiko la waumini wanaoweza kukusanyika katika jengo fulani au mahala pengine popote pale.

Kitaalamu, kanisa linaweza lisiwe kusanyiko la kidini, kwa sababu neno hilo hilo limetumika katika Matendo 19:32 kumaanisha umati wa watu wenye ghasia (watu waliochafuka-chafuka) ambao walikuwa wamekusanyika, na mstari huu unasema kwamba kusanyiko hilo lilikuwa limechanganyikiwa na kwamba “sehemu kubwa haikujua kwa nini walikuwa wamekusanyika pamoja.” Pengine hii inaweza kutumika kuelezea sehemu kubwa ya ‘kanisa’ la leo, lakini ukweli ni kwamba kanisa sio jengo bali ni kusanyiko la watu.

Kanisa ambalo Biblia inalisema zaidi leo, ni “Kanisa la Mungu, ambalo amelinunua kwa damu yake mwenyewe” (Matendo ya Mitume 20:28), na Mtakatifu Paulo analiita kanisa hilo la kipindi hiki cha sasa, kuwa ni “Mwili wa Kristo, “Au” Kanisa ambalo ndilo Mwili wake “(1 Wakorintho 12:27; Waefeso 1:22-23).

Watu hawawezi kujiunga na Kanisa hili kwa ubatizo wa maji au kwa taratibu ya ibada nyingine yoyote ile, bali kwa kuwa na imani tu kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kuhusiana na waumini wa Kristo, Mtakatifu Paulo anatangaza kuwa: “Kwa Roho mmoja sisi sote tumebatizwa kuwa mwili mmoja” (1 Wakorintho 12:13). Na katika Warumi 12:5 Mtume huyu anasema kwamba “na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo.”

Watu wengi wanyofu wamekuwa na majina yao kwenye hati za kanisa la mahali pamoja kwa miaka mingi bila ya wao kuujua ukweli huu ‘mkubwa’ – kwamba Kanisa la kweli la Mungu sio jengo, bali ni kusanyiko la wale wanaomtumaini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao.

Bila shaka, watu waliomo ndani au nje ya mashirika mengi ya kidini tunayoyaita ‘makanisa’ ni wa Kanisa hili moja kuu la Biblia, wakati ambapo wengine, pamoja na taaluma zao zote za dini, hawamo.

Swali linabaki kuwa ni: Je! Tumemwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu?

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *