Home 2021 June 20 Mlioshwa, Mlitakaswa, Mlihesabiwa Haki

Mlioshwa, Mlitakaswa, Mlihesabiwa Haki

Mlioshwa, Mlitakaswa, Mlihesabiwa Haki

“Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu” (1 Wakorintho 6:11)

Mistari iliyotangulia mstari huu wa 11 katika 1 Wakorintho 6, ina orodha ndefu ya dhambi mbalimbali mbaya na maovu ambayo watu wameanguka kwayo, na Mtume Paulo anaongeza kwa kusema:

“Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii.” Kanisa la Mungu halijaundwa na “watu wazuri” ambao hawajawahi kuanguka katika dhambi. Badala yake limeundwa na watu wenye dhambi, waliookolewa kwa neema, kupitia malipo bora, yasiyo na kipimo, yaliyofanywa kwa ajili ya dhambi na Kristo Yesu kwenye msalaba wa Kalvari.

“Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii.” Laiti kama Mtume huyu angezijumuisha dhambi “zilizosafishwa” zaidi, kama vile kiburi, kujiona, kujihesabia haki, n.k. angelazimika kusema hivi: “Na nyinyi nyote mlikuwa watu wa namna hii.”

Lakini hata hivyo, Mtume Paulo anasema hivi: “Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii.” Mungu ni wa kushukuriwa, hasa kwa kile anaendelea kukisema Mtume huyu juu ya wale ambao wamechafuliwa na dhambi: “Lakini mmeoshwa, lakini mmetakaswa, lakini mmehesabiwa haki, katika jina la Bwana Yesu, na katika Roho wa Mungu wetu.”

Maneno haya matatu yana ‘ufahari’ wake, ni maneno yenye uzuri usioweza kuelezeka, unaopita maelezo: “Lakini mmeoshwa, lakini mmetakaswa, lakini mmehesabiwa haki”!

Neno “lakini” linaloonekana kabla ya kila maneno hayo matatu, linaonyesha kuwa kila neno moja linapaswa kuzingatiwa kipekee kabisa. Viumbe hao waovu, walikuwa ni baadhi yenu, “lakini mmeoshwa,” mkasafishwa kutoka kwenye dhambi zilizowachafua. “Lakini mmetakaswa.” Baada ya kuwa mmesafishwa, sasa mmetengwa kuwa watakatifu kwa utukufu wake. “Lakini mmehesabiwa haki.” Je! Mungu akituhesabia haki, ni nani awezaye kutulaani?

“Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki” (Warumi 8:33)

Yote haya hufanywa kwa kila mwenye dhambi anayeamini kazi kamilifu ya Yesu Kalvari, kama mstari wetu unavyosema, “katika jina la Bwana Yesu, na katika Roho wa Mungu wetu.”

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *