Home 2021 May 29 Jinsi ya Kubatizwa Bila Kulowa Maji

Jinsi ya Kubatizwa Bila Kulowa Maji

Jinsi ya Kubatizwa Bila Kulowa Maji

Watu wengi wanapofikiria kuhusu ubatizo, huwa wanafikiria kuhusu maji. Iwe ni kwa kuzamishwa, kunyunyiziwa au kupakazwa, fikra zao siku zote zinafikiri kuwa maji yana ‘mkono wake’ kwa namna moja au nyingine.

Je! Unajua kwamba Biblia inafundisha kuwa kuna uwezekano wa kubatizwa bila ya ‘kulowa’ maji?

Fikiria juu ya Yohana Mbatizaji. Kwamba alibatiza kwa maji ni jambo lililo wazi kabisa, na wala halina kipingamizi chochote (Yohana 1:31; Marko 1:5). Kwa hiyo, kila mtu aliyebatizwa na Yohana, alilowa!

Hata hivyo, katika Mathayo 3:11 mtu huyu pekee anayeitwa ‘Mbatizaji’ katika Biblia yote, anabainisha batizo nyingine mbili ambao hazijumuishi maji:

“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Mathayo 3:11)

Roho Mtakatifu ni wa kiroho na kwa hiyo hajatengenezwa kwa maji, na nina hakika pia ubatizo wa moto utakausha unyevu ulioachwa kwa mtu yeyote aliyeshiriki kwenye tanuru la moto (Isaya 4:4: Malaki 3:2).

Lakini pia, kuna ubatizo wa taifa la Israeli kwa Musa ulionenwa katika 1 Wakorintho 10:2. Waisraeli walitembea katika bahari kwenye nchi kavu na Wamisri ambao walikuwa wakiwafuata ndani ya bahari walizama maji.

Baada ya Yesu kubatizwa kwa maji na Yohana, alizungumzia ubatizo mwingine kwa ajili yake mwenyewe ambao ungeishia katika kifo chake. Maji pekee yaliyohusika katika kifo cha Yesu yalikuwa ni yale yaliyomtoka ubavuni mwake (Yohana 19:34):

“Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!” (Luka 12:50)

Ubatizo wa Aina Nyingi: Mwingine Mkavu, Mwingine Mnyevu

Kuna batizo mbali mbali katika Biblia na nyingi ni kavu.

“Ubatizo” sasa umekuwa ni sawa na ubatizo wa maji, ingawa ubatizo haumaanishi maji. Ufafanuzi bora zaidi utakuwa ni jinsi mtu anavyotambulishwa (identified) na kitu fulani/husika.

Hii ndiyo sababu Paulo anaelezea juu ya ubatizo katika mwili wa Kristo katika 1 Wakorintho 12:13. Kila mtu ambaye ameokolewa na injili ya Kristo leo ametambulishwa (identified) na Bwana katika ubatizo wake wa pili hadi kufa:

“Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja” (1 Wakorintho 12:13)

“Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?” (Warumi 6:3)

Ubatizo katika Kristo ni kutambulishwa (identification) na Kristo. Hivyo, tunasulubiwa pamoja na Kristo bila kugusa maji (Wagalatia 2:20).

Ubatizo wa maji kamwe haukuashiria kifo, bali utakaso, kama vile ondoleo la dhambi (Marko 1:4). Katika kipindi cha sasa cha neema, dhambi zetu zinasamehewa kupitia damu ya Kristo kupitia kifo chake.

Kuna ubatizo mmoja tu ambao Paulo anasema ni muhimu katika kanisa, na haujumuishi maji wala kuhani wa kuufanya. Ubatizo huu hufanywa na utendaji wa Mungu wakati tunaamini injili ya kifo na ufufuko wa Kristo Yesu (Waefeso 4:5).

“Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu” (Wakolosai 2:12)

Kama bado unafikiria kuwa ubatizo ni lazima ujumuishe maji kila wakati, basi wewe unalo tatizo kubwa…

Ubatizo hauhitaji maji, kuna mifano mingi katika Biblia juu ya hilo na ubatizo mmoja unaouhitaji, hauhitaji hata tone moja la maji.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *