Home 2021 May 15 Nenda Kauze Vitu Vyako Vyote!

Nenda Kauze Vitu Vyako Vyote!

Nenda Kauze Vitu Vyako Vyote!

Huu ni wakati mzuri wa kuwasisitiza marafiki zetu wale ambao hawataki kuigawa kweli ya neno la Mungu kutii maagizo ya Bwana wetu Yesu Kristo ya kuuza kila kitu walicho nacho na kumfuata (Luka 18:22):

“Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate

Nyumba zao zimejaa mali nyingi, tena mpya, na hata akaunti zao za benki zina amana za kutosha. Kama wewe ni maskini, unaweza ukawa ni mmoja wa wanufaikaji ambaye una haki na baadhi ya mali zao hizo kama Bwana alivyoagiza. Hivyo, ongeza ‘mashinikizo’ ili upate sehemu yako ya mgao wa mali zao unayoistahili…!

Kushindwa kwao huko kuigawanya kweli ya neno la Mungu sawasawa, kunawaongoza kwenye ‘injili ya maji’ ya Matendo 2:38 na kwenye ‘injili ya kijumuhiya ya Matendo 2:44-45:

“Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja”

Unaweza ukawa “kila mtu” kwa injili hiyo, na unaweza hata kuchukua ile iPad mpya ya Mchungaji wako au gari yake, vikawa vyako kuanzia sasa na hakuna atakaye kuuliza; we fanya tu hivyo, ujionee…!!!

Wakikukatalia, waambie wameikana imani yao (Luka 18:22), na kama kweli wanataka kuurithi uzima wa milele (Luka 18:18) inawapasa kuyakubali na kuyafuata maelekezo Bwana YOTE aliyoyatoa na waishi kijumuhiya kama ilivyokuwa wakati wa Matendo.

Ndugu wanaokuzunguka wanaweza kukucheka na kukuona ‘hamnazo’  kwa sababu unaweza ukaonekana kama unaleta ‘mzaha’ kwenye mambo ya msingi, lakini SIVYO; hii ni njia isiyo na madhara kwa kuyaanika (kuyafunua) makosa yao ya kufuata mfano (pattern) kama ilivyo kwenye Injili ya Mathayo mpaka kwenye Injili ya Yohana na Pentekoste katika majira haya ya neema ya kanisa la leo.

Mfano wetu, sisi Kanisa Mwili wa Kristo leo, sio kile waamini wa ‘ufalme’ walikuwa wakikifanya katika Matendo ya Mitume, Sura ya 2 mpaka ya 4, wakiwa katika kujiandaa kwa dhiki yao iliyotabiriwa.

Mfano wetu kama kanisa ni kile Bwana alichokifunua kuanzia katikati ya kitabu cha Matendo ya Mitume kwa Paulo, Mtume wa kanisa la leo.

Kutoka kwa Mtume Paulo tunajifunza kwamba sisi ni mabalozi wa neema ya Mungu, vinywa vyetu vina kazi ya kusihi kwa ajili ya Kristo; ili watu wote wapatanishwe na Mungu na sio ombaomba wa vitu vya watu. Tunapaswa kujipatia mahitaji yetu (1 Timotheo 5:8; 1 Timotheo 6:8):

“Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini”

“Ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo”

Ni vigumu kwa watu wengi kuachilia vitu vyao kuliko fundisho lao. Tumia huo mwanya kwa faida ya kweli ya neno la Mungu ili kuwafanya watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo (Waefeso 3:9).

Ikifika wakati wanataka kufuata mfano wa Paulo, watasikiliza injili ya Paulo.

Kwa Utukufu wa Jina Lake

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *