Home 2021 May 03 Ukweli Kuhusu Zaka

Ukweli Kuhusu Zaka

Ukweli Kuhusu Zaka

1. Neno “zaka” ambalo kwa Kiebrania ni “ma`aser” na kwa Kiyunani ni “apodekatoo” linamaanisha sehemu ya kumi.

2. Makanisa mengi ya Kikristo yanahubiri kutoa zaka kama njia ya kusaidia kazi ya Bwana leo. Kuna tofauti nyingi za mada hii. Wengine hulipa kanisa la mahali pamoja sehemu ya kumi ya mapato yao baada ya kukatwa kodi na wengine kabla ya kukatwa kodi. Wengine wanadai kutoa zaka kwenye mafao ya uzeeni, mirathi, zawadi, na hata kutoka kwenye ushindi wa kamari. Suala la kutoa zaka limesababisha ugomvi mkubwa na mgawanyiko katika makanisa yetu kwa kipindi kirefu sasa.

3. Kifungu kinachojulikana zaidi juu ya kutoa zaka kipo katika kitabu cha Agano la Kale cha Malaki 3:8-10:

“Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la”

Maandiko haya yamesababisha mazoezi ya “kuleta zaka ghalani”. Kwa maelezo rahisi, kusanyiko linahimizwa kutoka kwenye mimbari kwamba wapitishe utoaji wao wote wa Kikristo kupitia kanisa la mahali hapo (ghala). Ikiwa wanataka kutoa kwa huduma au shirika lingine la Kikristo, redio au matangazo ya runinga, n.k., huwa ni lazima ipitie kwenye ‘mchakato’ wao wa kimadhehebu ili kanisa la mahali hapo lipate hiyo “sifa”. Lakini pia, mchungaji na wazee wa Kanisa husika, ni lazima wafanye uamuzi ikiwa sababu inayoungwa mkono na mtoaji na utoaji huo, kama “inastahili”.

4. Matumizi haya ya kifungu cha Malaki ni mfano mzuri wa Maandiko yanayochukuliwa nje ya muktadha wake wa kihistoria na wakati. “Taifa hili lote” katika mstari wa 9 ni taifa la Israeli lililorudi nyuma, na SIO kanisa la leo (Malaki 1:1; 3:6). Walikuwa chini ya sheria ya Musa, mfumo ambao ulikuwa na baraka zenye masharti. Waumini leo hawako chini ya sheria bali wako chini ya neema (Warumi 6:14). Ndiyo kusema, tayari tumebarikiwa na Mungu kwa baraka zote za rohoni katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo (Waefeso 1:3) na tuko chini ya mfumo wa baraka zisizo na masharti na utawala wa neema hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu (Warumi 5:21).

5. Hii inapaswa kumaliza mashtaka ya kawaida kwamba waumini ambao hawatoi zaka kuwa “wanamuibia Mungu” na “wamelaaniwa kwa laana.” Ghala lililotajwa katika mstari wa 10 sio kanisa la mahali pamoja bali ni ghala la kuhifadhia au ‘silo’ lililokuwa katika hekalu la Kiyahudi ambapo nafaka zilizotolewa zaka ya Kiebrania ilihifadhiwa (2 Nyakati 31:4-12).

6. Chini ya sheria ya Musa, ni bidhaa za kilimo tu ndizo zilikuwa zikitolewa kama zaka. Hii ilijumuisha nafaka, matunda, na mifugo (Walawi 27:30-34). Lakini pia, ni bidhaa zilizokuwa zinazozalishwa ndani ya mipaka ya ardhi ya Israeli TU ndizo zilipaswa kutolewa kama zaka. Wayahudi waliokuwa wanaoishi katika nchi za watu wa Mataifa walikuwa wamesamehewa kutoa zaka.

7. Wengine walioondolewa kwenye sheria ya kutoa fungu la kumi ni pamoja na walioajiriwa, wavuvi, wachimbaji madini, wafanyakazi wa mbao, wafanyakazi wa ujenzi, wanajeshi, wafumaji, wafinyanzi, watengenezaji, wafanyabiashara, wafanyakazi wa serikali, na makuhani. Kwa kifupi, wote ambao hawakuwa wakulima walisamehewa kutoa zaka!

8. Mkulima aliye na ng’ombe 9 tu hakutoa zaka kwa sababu sheria ilitaja wazi kabisa kuwa “kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa BWANA.” Vivyo hivyo, mkulima aliyekuwa na kondoo 19 alilipa kondoo 1 tu kuwa zaka ya Bwana.

9. Wakulima wa Kiyahudi katika ardhi wangeweza kukomboa (kununua tena) zaka ya mazao yao kwa adhabu ya kuongeza sehemu yake ya tano juu yake. Kwa maneno mengine, KAMA mkulima anataka kubaki na zaka yake ya nafaka yenye thamani ya shilingi 1,000, angeweza kulipa shilingi 1,200 (Mambo ya Walawi 27:31).

10. Mifugo haikuweza kurudishwa wala mkulima hangeweza kubadilisha mnyama ‘mzuri’ kwa ‘mbaya’ au kinyume chake. Jaribio lolote la kubadilisha mnyama mwingine yeyote isipokuwa yule wa kumi aliyepita chini ya fimbo, mkulima huyo angeadhibiwa na kupoteza sehemu yake ya kumi na huo mbadala wake (Mambo ya Walawi 27:33).

11. Mungu aliwateua Walawi wawe pekee ndio wapokea (wala) zaka (Hesabu 18:21). Hawa walikuwa ni moja ya makabila ya Israeli ambao hawakupewa urithi katika nchi yao. Bwana mwenyewe na zaka ya wana wa Israeli ilikuwa ndio urithi wao. Zaka ilitumika kwenye huduma ya maskani (baadaye hekalu) (Hesabu 18:20-28).

12. Ilikuwa ni haramu kwa mtu yeyote ambaye hakuwa wa kabila la Lawi kupokea (kula) zaka, kama vile manabii, mitume, wachungaji, wahubiri, wafalme au wainjilisti; wanavyopokea (kula) sasa.

13. Walawi nao walilipa sehemu moja ya kumi ya zaka zao kwa kuhani mkuu. Ikumbukwe kuwa SIO Walawi wote walikuwa makuhani isipokuwa wana wa Haruni tu. Makuhani hawa, hawakutoa zaka!

14. Bwana Yesu Kristo hakuomba wala kupokea zaka kama chanzo cha ‘mapato’ kwa ajili ya kuendesha huduma Yake. Yeye akiwa wa kabila la Yuda (sio Lawi) hangeweza kufanya hivyo bila kuvunja sheria (Waebrania 7:14; Ufunuo 5:5).

15. Petro (sio wa kabila la Lawi) wala Paulo (wa kabila la Benyamini) hawakuwahi kupokea zaka kwa ajili ya huduma zao.

16. Hata Wayahudi leo, hawaiishi zaka kama sheria ya Musa invyotaka, kwa sababu hakuna Walawi, makuhani, wala ibada ya hekaluni huko Yerusalemu. Marabi wa Kiyahudi wanajua sheria ya kibiblia vizuri vya kutosha na kujua kwamba utoaji wa zaka chini ya hali ya sasa ni haramu. Kulingana na wao, ni mpaka hapo wakati hekalu litakapojengwa upya huko Yerusalemu na madhabahu iliyowekwa wakfu na makuhani na Walawi wanaofanya kazi, Wayahudi wote wanaoishi ndani ya maeneo ya kutoa zaka sawasawa na sheria ya Musa, wataanza kutoa zaka.

17. Huduma nyingi za Kikristo leo zinaendelea kukusanya zaka, kwa kutumia hoja kwamba zaka ilimtangulia Musa na sheria. Lakini hoja hii haina uhalali, kwa sababu Sabato pia ilitangulia kutolewa kabla ya sheria (Kutoka 16:23-29) na bado haiwahusu watu wa Mungu leo ​​(Warumi 14:5-6; Wagalatia 4:9-10; Wakolosai 2:16-17).

18. Ibrahimu alitoa zaka kwa Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lakini hizi zilikuwa ni nyara za vita, sio zaka ya kisheria ya nchi ambayo Musa aliamuru. Pia, Mungu hakuamuru zaka, Ibrahimu alichagua kuitoa kwa hiari yake mwenyewe (Mwanzo 14:17-23; Waebrania 7:1-10).

19. Marejeleo mengine yaliyopo ya kimaandiko juu ya kutoa zaka kabla ya Musa ni Yakobo. Lakini tena, hapa hapakuwa na amri ya kutoa zaka. Kimsingi, Yakobo ndiye anayeweka masharti kadhaa ya kutimizwa na Mungu, kabla yeye hajamlipa Bwana zaka yake (Mwanzo 28:20-22). Hakuna ushahidi wowote wa Kibiblia kwa Yakobo aliitimiza nadhiri yake hiyo au kuiondoa…

20. Marejeleo ya kibiblia ambayo yanazungumzia masuala ya zaka ni: Mwanzo 14:20; 28:22; Mambo ya Walawi 27:30-32; Hesabu 18:20-28; Kumbukumbu la Torati 12:6,11,17; 14:22,23,28; 26:12; 2 Mambo ya Nyakati 31:5,6,12; Amosi 4:4; Malaki 3:8-10; Mathayo 23:23; Luka 11:42; 18:12; Waebrania 7:5-9.

21. Paulo mtume kwa watu wa mataifa kwa kipindi hiki cha Neema ya Mungu, hajataja popote kuhusu zaka ingawa anasema mengi juu ya utoaji wa Kikristo: Warumi 15:25-26; 1 Wakorintho 9:7-14; 16:1-3; 2 Wakorintho sura ya 8 & 9; Wagalatia 6:6-10; Wafilipi 4:10-19; 1 Timotheo 5:9-18.

NANI atoe kwa kazi ya Bwana? Mkristo! Yeye hutoa kwa utaratibu, kwa kujitolea, na kwa furaha.

ANATOA KWA NANI? Kwa Kristo!

ANATOA KWA NINI? Kwa sababu ya Kristo!

SIO kwa mtu au kwa kanisa, sio kwa faida, BALI KWA INJILI!

Utukufu una YEYE, Milele na Milele, AMINA.

Author: Festus Patta

4 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *