Home 2021 April 04 Injili Nne Vs Injili ya Paulo!

Injili Nne Vs Injili ya Paulo!

Injili Nne Vs Injili ya Paulo!

Vitabu vya Agano la Kale vya Mathayo, Marko, Luka, na Yohana kwa kawaida hurejelewa kama Injili Nne. Biblia nyingi hata zina majina ya vitabu hivi, katika mlengo huo, kama vile: “Injili Kulingana na…, au Injili ya… ”Mathayo, Marko, Luka, au Yohana.

Vitabu vyote hivyo vinne vina injili sawa/moja: injili ya ufalme. Injili ya ufalme ilitangaza kutimizwa kwa ufalme wa kinabii kwa taifa la Israeli.

Yale ambayo hayamo (yanakosekana katika injili hiyo ya ufalme) ni injili ya msalaba ya wokovu. Yaani, Kifo cha Kristo, kuzikwa, na kufufuka wake havitokei hadi sura za mwisho za vitabu hivyo.

Yesu katika huduma yake ya kidunia alithibitisha ahadi za ufalme kwa watu wa tohara (Israeli):

“Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu” (Warumi 15:8)

Kila moja ya vitabu hivyo vinne huanza na huduma ya Yesu hapa duniani kwa watu wa tohara na kuishia na kifo chake na ufufuko. Hii inaelezea huduma na ujumbe wa Petro, Yohana, na wale kumi na wawili kulingana na unabii wa Kristo. Huduma zao huanza na unabii na kuishia na utimilifu wake katika Kristo.

Walakini, kuna injili ya tano! Injili ya Paulo, ambayo haikunakiliwa kutoka kwa Mathayo, Marko, Luka, wala Yohana. Hii ilifunuliwa kibinafsi na Bwana kwa Paulo Mtume pekee:

“Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo” (Wagalatia 1:11-12).

Kwa hivyo, injili ya Paulo kama ilivyonenwa katika 1 Wakorintho 15 ni tofauti na ‘Injili zile nne za kijadi’. Injili ya Paulo inajumuisha ‘kufunuliwa kwa siri ya Kristo’.

Mwanzo Mpya

Paulo hajaanza na huduma ya Yesu kwa watu wa tohara kama vile ilivyokuwa kwa Mathayo, Marko, Luka, na Yohana. Anasema mahali pengine kwamba hamjui Kristo kwa namna ya mwili:

“Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena” (2 Wakorintho 5:16)

Badala yake, jambo la kwanza katika injili ya Paulo ni jambo la mwisho katika zile ‘injili nne’: kifo na ufufuko wa Kristo:

“Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko” (1 Wakorintho 15:3-4)

Hii ndiyo kweli inayoonekana wazi kuwa ndio msingi wa injili ya Paulo ya neema ya Mungu ambayo haikutokana na ahadi za ufalme kwa wale waliotahiriwa, bali msalaba wenyewe (1 Wakorintho 1:18, 2:2, 3:10). Jambo la kwanza kabisa la injili ya Paulo sio hata ukoo wa Yesu wala uhusiano wa Yesu na unabii, bali ni kifo chake kwa ajili ya dhambi zetu.

Mwisho Mpya

Tofauti pia ipo katika jinsi ambavyo injili ya Paulo inavyoisha katika 1 Wakorintho 15: 1-10.

Zile zinazoitwa ‘Injili nne’ haziendelei mbele zaidi, bali zinakomea na kuonekana kwa Yesu mfufuka kwa wale mitume kumi na wawili. Ndio maana Paulo hapatikani popote katika Injili hizo nne. Paulo, sio kwamba, hapatikani tu bali ni ‘kafiri’ na ni adui namba moja wa injili hiyo ya ufalme:

“Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani” (Matendo 8:1-3)

Injili ya Paulo huenda zaidi ya ufufuko wa Yesu Kristo na kuonekana kwake kwa mabaki ya ufalme wake (kingdom remnant). Paulo anakuelezea kufunuliwa kwa siri ya Kristo kwake kuwa ni “mwisho wa yote”:

“Na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” (1 Wakorintho 15:8)

Akiwa amezaliwa nje ya wakati ‘unaofaa’ wa unabii, Paulo alipewa wokovu na Bwana mwenyewe na alichaguliwa kama msambazaji (dispenser) wa injili ya neema ya Mungu:

“Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache” (Waefeso 3:1-3)

na tena…

“Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili” (1 Wakorintho 9:17)

Injili ya ‘SIRI’

Ni jambo lililozoeleka kuzifuata hadithi za injili zinazopatikana katika vitabu vya Mathayo, Marko, Luka na Yohana kama ufunguo wa kuelewa Biblia. Wakati kuna ‘vito’ vya mafundisho na kweli mbalimbali za kiroho katika vitabu hivyo, lakini ni lazima tukumbuke Injili ya Paulo ili kuelewa vitu vyote (hii ni pamoja ni vitu vilivyo mbele ya ufufuko wa Yesu Kristo):

“Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote” (2 Timotheo 2:7)

Injili ambayo Kristo Yesu alimpa Paulo Mtume haipo katika vitabu vile vinne vya ‘Injili’ (yaani Mathayo, Marko, Luka na Yohana), na hivyo inaitwa Injili ya ‘SIRI’ (Warumi 16:25):

“Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele”

Badala ya kujaribu kujifananisha na kutaka kufuata huduma ya Bwana hapa duniani ambayo aliipasisha kwa wale Mitume wake kumi na wawili kwa taifa la Israeli, tunapaswa kuanza na Kristo aliyesulubiwa na kufanya huduma yetu kwa kufuata ujumbe kutoka mbinguni aliopewa mtume wa watu wa Mataifa (Warumi 11:13).

Tunapozingatia injili ambayo Mungu alimpa Mtume Paulo basi tutakuwa katika nafasi ya kukua katika neema ya Mungu kama Paulo, kulingana na injili yake:

“Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami” (1 Wakorintho 15:10)

Kwa Utukufu wa Jina lake KRISTO YESU!

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *