Home 2020 October 09 Ufahamu Sahihi wa Wokovu

Ufahamu Sahihi wa Wokovu

Ufahamu Sahihi wa Wokovu

Kila anayetaka kwenda mbinguni na kujenga mahusiano mazuri na Mungu, lazima afahamu kwa usahihi yale ambayo Biblia inafundisha kuhusu wokovu. Ufahamu sahihi wa elimu ya wokovu ni muhimu kwa kila anayetumaini kuokolewa kwa sababu ni msingi wa imani ya kweli. Mtu akiukosa ufahamu sahihi wa wokovu, anaweza kufikiri kwamba ameokolewa, kumbe si kweli, bali amejidanganya. Atajutia siku ile atakaposimama mbele ya Kristo na kuambiwa, “Sikukujua, ondoka kwangu” (Mathayo 7:21-23). Pia, mbaya zaidi, anaweza kuwashuhudia watu Injili isiyo ya kweli (Wagalatia 1:6-9) hata na wao pia wakatupwa motoni pamoja naye. Shida nyingine inayosababishwa na kutoelewa wokovu kwa njia iliyo sahihi ni kwamba inaweza kusababisha mtu aliyeokoka kweli kuwa na mashaka juu ya wokovu wake na kukosa amani na raha ambazo ni matunda ya wokovu wa kweli.

Katika ukurasa huu ‘tutachunguza’ maandiko (Matendo 17:11) ili tujue kile ambacho Biblia inatufundisha kuhusu wokovu ili kila mmoja wetu awe na ufahamu sahihi wa wokovu. Ufahamu sahihi wa wokovu ni msingi muhimu wa maisha ya Kikristo. Ili Mkristo aweze kuishi kama anavyopaswa, anahitaji kuyajua yale yaliyofanyika alipookolewa na ajue uwezo alio nao katika kuishi maisha mapya. Pamoja na hayo, kupitia ukurasa huu pia, tutajifunza jinsi wokovu unavyomletea Mkristo maisha haya mapya.

Lakini pia, kwa sababu watu wengine wameyachanganya mafundisho ya wokovu, tutayachunguza mafundisho ya uongo kuhusu wokovu. Kwa mfano, hali ya kutegemea matendo mema ili kupata wokovu au utegemezi katika kifo cha Yesu pamoja na ubatizo. Tutaona, kupitia maandiko mbalimbali, kwa nini mafundisho haya ni ya uongo na kwa nini mafundisho haya hayawezi kumwokoa mtu ye yote.

Katika ujumla wake, maandishi kwenye ukurasa huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Katika sehemu ya kwanza tunazungumzia yale ambayo mwenye dhambi anapaswa kuyajua na kuyaamini ili aokolewe; na katika sehemu ya pili tunazungumzia jinsi wokovu unavyokuwa msingi wa maisha ya Kikristo.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *