Home 2020 October 09 Tunahitaji Kuokolewa!

Tunahitaji Kuokolewa!

Tunahitaji Kuokolewa!

Kwa Nini Wanadamu Wanahitaji Kuokolewa?

Kujibu swali hilo tutaanza kwa kumchunguza mwanadamu wa kwanza, Adamu, na jinsi alivyokuwa mwanzoni. Wakati Adamu alipoumbwa alikuwa na ushirika na Mungu, yaani uhusiano mzuri. Alikuwa mkamilifu; hakuwa na kosa lo lote. Alikuwa hai kiroho na alikuwa chini ya utawala wa Mungu. Mungu alihitaji utiifu kutoka kwa Adamu ili Adamu aendelee kukaa katika uhusiano na Mungu. Mungu alimwonya Adamu kwamba kutokutii kwake kutaleta adhabu. Mwanzoni Adamu alimtii Mungu na aliendelea kuwa na ushirikiano na Mungu. Wakati huo Adamu alikuwa akitimiza makusudi mawili ya Mungu kumwumba Adamu (mwanadamu); Adamu alimtukuza na kumtumikia Mungu.

Wakati huo, Shetani alitaka kuwa mtawala wa Adamu. Alijua kama atafaulu kumshawishi Adamu kumtii yeye badala ya kumtii Mungu, uhusiano wa Adamu na Mungu utavunjika na Adamu atahamia na kuwa chini ya utawala wa Shetani. Hivyo siku moja Shetani alimwendea Hawa (mke wa Adamu) akiwa na kusudi la kumjaribu (Mwanzo 3:1-5). Adamu alichagua kumtii Shetani na kutomtii Mungu (Mwanzo 3:5-6). Uasi huu wa Adamu ulisababisha mabadiliko mabaya katika maisha yake. Alipata kuwa mwenye dhambi na matokeo yake alikufa kiroho, alitenganishwa na Mungu, na alihamia na kuwa chini ya utawala wa Shetani. Aliacha kuishi kwa makusudi ya Mungu ya kuumbwa wake. Badala yake, aliishi katika hali ya kujitukuza na kumtumikia Shetani huku akiendelea katika dhambi.

Baada ya Adamu kutenda dhambi, hitaji lake kuu lilikuwa ni nini? Hitaji lake kuu lilikuwa kutaka ushirikiano wake na Mungu urejezwe ili aweze kuishi tena katika makusudi ya Mungu kwa ajili ya maisha yake. Ili aweze kuhusiana tena na Mungu alihitaji kufanywa tena mkamilifu, alihitaji kufanywa hai kiroho, alihitaji kuokolewa kutoka katika utawala wa Shetani na kurudishwa na kuwa chini ya utawala wa Mungu, na mwisho wa yote, alihitaji mshahara au adhabu ya dhambi yake kushughulikiwa. Mahitaji hayo yote yanatimizwa katika wokovu.

Sisi sote ni wazao wa Adamu, na kwa sababu hiyo sisi sote tumerithi asili yake ya dhambi. Vilevile sisi ni watenda dhambi (Warumi 5:12). Wote, tulizaliwa tukiwa tumetenganishwa na Mungu kiroho, tena tukiwa chini ya hukumu Yake na pia chini ya utawala wa Shetani. Sawa na hitaji la Adamu, hitaji kuu la kila mwanadamu ni nini? Hitaji letu kuu, sisi sote, ni kutengeneza uhusiano wetu na Mungu tukiingia tena katika ushirika naye ili tuweze kuishi kufuatana na makusudi Yake kwa ajili ya maisha yetu na kukwepa hukumu zake.

Sasa tuangalie kwa undani zaidi maana ya sisi kuwa wenye dhambi na uharibifu wake mkubwa katika maisha yetu.

Watu wengi wanadhani kuwa mwenye dhambi siyo jambo baya sana. Wakati mwingine wanasema, “Ndivyo tulivyo tu”, au “Ni tatizo lakini siyo tatizo kubwa.” Watu hawa, hakika wanakosea! Biblia inasema kuwa mwenye dhambi ana tatizo kubwa sana, tena liletalo adhabu ya milele na milele. Sasa tuangalie jinsi Biblia inavyoeleza juu ya hali ya wenye dhambi.

A. Mwenye Dhambi ni Mfu Kiroho

Waefeso 2:1-2 – “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi”

Wakolosai 2:13 – “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote”

Tangu wakati ule Adamu alipomwasi Mungu, yeye na wazao wake wote wamekufa kiroho; yaani wametengwa na Mungu. Kila mmoja wetu amerithi asili ya dhambi (Warumi 5:12) na kuzaliwa akiwa mfu kiroho. Kwa nini Biblia inalitumia neno “wafu” kuielezea hali yetu mbele ya Mungu? Je, unaweza kuwa na uhusiano na maiti? Hapana! Je, unaweza kuwa na urafiki gani na maiti? Hamna! Je, maiti inaweza kufanya nini ili ikupendeze? Haiwezi! Je, kama mtu alikukosea alipokuwa hai, afanye nini ili asuluhishe kosa lake nawe akiwa maiti (baada ya kufa)? Hakipo cha kufanya! Hiyo ndiyo picha ambayo Mungu anataka kutupatia kuhusu hali yetu mbele yake. Kwa sababu sisi tumerithi asili ya dhambi na tumezaliwa tukiwa wafu kiroho, hatuwezi kufanya cho chote ili kumpendeza Mungu, wala kujipatanisha na Mungu, wala kuitafuta suluhu ya makosa yetu mbele ya Mungu.

Aliye mfu kiroho anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kuhuishwa, yaani, kufanywa hai tena kiroho.

Je, mtu aliye mfu kiroho anaweza kujihuisha awe hai kiroho? Hapana kwa kuwa hana uwezo huo kama ilivyo maiti.

B. Wenye Dhambi Wako Chini ya Utawala wa Shetani

1 Yohana 5:19 – “Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu.”

Adamu alipomwasi Mungu kwa kuufuata ushauri wa Shetani, alijiweka chini ya mamlaka ya Shetani. Shetani ni mtawala wa ulimwengu huu (Yohona 14:30; 16:11) na ni mdanganyifu asiyependa wanadamu. Anawatakia mateso, hofu, hata kifo. Kwa hila, anazitumia nguvu zake kuwalaani watu na kuwasababishia matatizo katika maisha yao. Wakati mwingine anaweza kutumia uwezo alionao kama-kuwasaidia, kwa mfano katika kuponya magonjwa (kama inavofanywa na waganga wa kienyeji). Lakini kwa dhati, Shetani hana nia hiyo ya kuwasaidia wanadamu. Anapomsaidia mwanadamu, daima ana kusudi lake la kutaka kumvuta mbali na Mungu ili amtegemee Shetani kuliko Mungu. Nia yake ni uharibifu kwa mwanadamu huyu kwa kuwa mwisho wa kumtegemea Shetani ni uangamivu wa milele.

Mtu aliye chini ya utawala wa Shetani anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kuondolewa kutoka chini ya utawala huo wa Shetani.

Je, mtu aliye mfu kiroho anaweza kumshinda Shetani na kujiweka huru naye? Hapana kwa kuwa mtu mfu huwa hana uwezo.

C. Mwenye Dhambi ni Adui wa Mungu

Warumi 5:10 – “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.”

Shetani ni adui wa Mungu, na tunapokuwa katika ufalme wa Shetani, chini ya mamlaka yake, nasi pia tunakuwa maadui ya Mungu.

Adui wa Mungu anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kupatanishwa na Mungu.

Mtu aliye mfu kiroho, aliye chini ya utawala wa Shetani, aliye adui wa Mungu, anaweza kufanya nini ili ajipatanishe na Mungu? Hakuna analoweza kufanya.

D. Mwenye Dhambi ni Mtumwa wa Dhambi

Yohana 8:34 – “Yesu akawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.’”

Warumi 6:6 – “Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi.”

Sisi sote, wenye dhambi, tunakuwa chini ya utawala wa Shetani, na pia tunakuwa watumwa wa dhambi. Hivyo, hata dhambi inatutawala. Hatuwezi kufanya cho chote ila kuwatii watawala wetu Shetani na dhambi.

Mtu aliye mtumwa wa dhambi anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kuwekwa huru na utumwa huo.

Je, Mtu aliye mfu kiroho na adui wa Mungu ambaye naye ni mtumwa wa dhambi na Shetani, anaweza kujiweka huru? Hapana!

E. Mwenye Dhambi ni Mtumwa wa Utu wa Kale (yaani “Mwili” au tamaa za dhambi)

Warumi 6:6 – “Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.”

Warumi 7:5 – “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.”

Warumi 8:5, 8, 9 – “Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho…Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu… Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”

Wenye dhambi wanatawaliwa na udhaifu wa miili yao. Miili yao inawafanya wawe watumwa wa dhambi. Biblia inatumia maneno haya kutuonesha hali yetu halisi kabla hatujaokoka. Tulikuwa wafu kiroho. Tulitawaliwa na utu wa kale (au mwili) uliotufanya kuwa watumwa wa dhambi.

Mtu anayetawaliwa na mwili wake wa dhambi anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kuwekwa huru na utawala wa mwili wake (au utu wake wa dhambi).

Mtu aliye mfu kiroho, aliye adui wa Mungu, aliye mtumwa wa dhambi, Shetani, na hata mwili wake wa dhambi anaweza kujiweka huru? Haiwezekani.

F. Mwenye Dhambi Yuko Chini ya Ghadhabu na Hukumu ya Mungu

Yohana 3:18 – “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Yohana 3:36 – “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.”

Kwa sababu tumemkosea Mungu, tuko chini ya ghababu na hukumu yake. Hukumu ya Mungu kwa ajili ya dhambi ni nini? Hukumu ya Mungu kwa ajili ya dhambi ni kifo, yaani kutenganishwa na Mungu milele (Warumi 6:23). Hatuna njia ya kujitoa kutoka chini ya ghadhabu na hukumu ya Mungu.

Mtu aliye chini ya ghadhabu na hukumu ya Mungu anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kutuliza ghadhabu ya Mungu na kukwepa hukumu Yake.

Mtu aliye mfu kiroho, aliye adui wa Mungu, aliye mtumwa wa dhambi na wa Shetani, anaweza kufanya nini ili atulize ghadhabu ya Mungu na hukumu Yake? Hana uwezo wa kufanya cho chote.

G. Mwenye Dhambi Yuko Chini ya Laana ya Sheria

Wagalatia 3:10 – “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.”

Sheria ya Mungu inaonesha kiwango kikamilifu cha Mungu. Watu wote wamepungukiwa kulingana na kiwango hicho kwa kuivunja angalau sheria moja ya Mungu. Kwa sababu hiyo wote wako chini ya laana ya sheria. Laana hiyo ni hukumu ya Mungu milele.

Mtu aliye chini ya laana ya sheria za Mungu anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kukombolewa na laana ya sheria hizo za Mungu.

Je, mtu aliye mfu kiroho, aliye adui wa Mungu, aliye mwenye dhambi iletayo laana ya sheria anaweza kufanya nini ili ajikomboe na tatizo hilo? Hanacho chochote cha kufanya.

H. Mwenye Dhambi ni Mchafu Machoni pa Mungu

Isaya 64:6 – “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.” Dhambi zetu zimetuchafua mbele ya Mungu. Mungu mtakatifu hawezi kuwa na ushirikiano na kitu kichafu. Dhambi zetu zinatuchafua kabisa hadi matendo yetu mema yamechafuliwa na dhambi. Tena uchafu huo hutufanya tusiwe na uwezo wo wote wa kumkaribia Mungu na kuwa na ushirika naye. Ndiyo maana Isaya anasema matendo yetu mema yamekuwa kama nguo chafu.

Mtu aliye mchafu machoni pa Mungu anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kusafishwa au kutakaswa.

Je, mtu aliye mfu kiroho, aliye adui wa Mungu, aliye mtumwa wa dhambi, Shetani na Mwili wake wa dhambi, anaweza kujitakasa? Hawezi.

I. Mwenye Dhambi Ametenganishwa na Kristo

Waefeso 2:12 – “Kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani”

Kutenganishwa na Kristo ina maana kutokuwa na ushirika au uhusiano naye. Ina maana mtu huyu anakuwa chini ya hukumu ya Mungu. Wenye dhambi wote wametenganishwa na Kristo.

Mtu aliyetenganishwa na Kristo anahitaji nini ili aokolewe? Anahitaji kuunganishwa na Kristo.

J. Mwenye Dhambi Hana Tumaini (Waefeso 2:12)

Kwa sababu tulizaliwa wafu kiroho, chini ya utawala wa Shetani, tukiwa watumwa wa dhambi, na adui za Mungu, tena chini ya laana na ghadhabu Yake, kweli, hatuna tumaini hata kidogo la kujiokoa.

Mtu asiye na tumaini la kujiokoa anahitaji nini? Anahitaji tumaini litokalo kwa Mungu.

Kwa nini wanadamu wanahitaji kuokolewa?

Tunahitaji wokovu kwa sababu sisi sote tulizaliwa tukiwa wenye dhambi, wafu kiroho, na katika hali ya kutenganishwa na Mungu. Vilevile tunahitaji wokovu kwa sababu mwenye dhambi ni adui wa Mungu aliye chini ya ghadhabu na hukumu ya Mungu. Zaidi ya hayo, mwenye dhambi yuko chini ya utawala wa Shetani, wa dhambi, na wa mwili wake wa dhambi. Yeye ni mchafu aliyetenganishwa na Kristo na wala hana uwezo wala tumaini la kuweza kujiokoa.

Haya ni matatizo makubwa sana. Wenye dhambi wanahitaji nini hasa? Wanahitaji matatizo yao hayo yote yatatuliwe. Wanahitaji kuhuishwa kuwa hai kiroho, wanahitaji kupatanishwa na Mungu, wanahitaji ku-kombolewa na laana ya sheria za Mungu, na wanahitaji kukwepa hukumu ya Mungu. Zaidi ya hayo, wanahitaji kuokolewa na utumwa wao kwa Shetani, dhambi, na miili yao ya dhambi. Wanahitaji kutakaswa na kuunganishwa na Kristo. Hivyo matatizo yao hayo yote yanatatuliwa na wokovu wa kweli unaopatikana katika Kristo Yesu.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *