Home 2020 October 09 Hatuwezi Kujiokoa!

Hatuwezi Kujiokoa!

Hatuwezi Kujiokoa!

Kwa Nini Wenye Dhambi Hawawezi Kujiokoa?

Katika mahusiano baina ya watu ni kawaida kwa mmoja kumkosea na kumwumiza mwenzake. Inapotokea migongano kama hiyo, mahusiano yanaweza kuyumba, na wakati mwingine yanaweza kuvunjika kabisa. Kama aliyemwumiza mwenzake anataka kupatanishwa, kawaida anatakiwa amwendee na kumwomba msamaha yule aliyeumizwa na kama kuna kitu chochote cha kufidia atatekeleza matakwa hayo.

Wapo watu wanafikiri wanaweza kutengeneza uhusiano wao na Mungu kwa njia kama hiyo. Kwa mfano, wakiona shida yao ni dhambi wanazozitenda, wataomba msamaha kwa Mungu na kujitahidi kutozitenda tena. Pengine wakiona wamevunja sehemu ya sheria ya Mungu, wataomba msamaha na kujitahidi katika kutii sheria hiyo. Yaani wakiona shida kati yao na Mungu ni matendo yao mabaya, wataomba msamaha na kujaribu kurekebisha matendo yao yawe matendo mema.

Je, tunaweza kutengeneza uhusiano wetu na Mungu kwa njia hiyo? Hapana. Hakuna tunachoweza kufanya kutengeneza uhusiano wetu na Mungu! Kwa maneno mengine – hatuwezi kujiokoa. Labda utauliza, “Ikiwa Mungu anatuagiza kusamehe wengine wanapoomba msamaha kwetu, je, kwa nini Mungu hatatusamehe sisi tutakapomwomba msamaha?” Majibu yetu ni haya yafuatayo:

1. Wenye Dhambi Hawawezi Kujiokoa kwa Sababu Wenyewe ni Wafu Kiroho.

Ukweli ni kwamba shida ya wenye dhambi ni shida ya kiroho ambayo inahitaji jibu la kiroho. Kwa sababu wenye dhambi ni wafu kiroho ina maana hawawezi kufanya cho chote kujisaidia kama vile maiti haiwezi kujisaidia. Mfu kiroho hana uwezo wa kujihuisha kuwa hai. Lazima aliye hai amsaidie.

2. Wenye Dhambi Hawawezi Kujiokoa kwa Sababu Mungu ni Mtakatifu.

Isaya 6:3 – “Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.”

Tunamaanisha nini tunaposema kwamba Mungu ni mtakatifu? Katika Biblia, neno “utakatifu” lina maana mbili:

(i) Utakatifu wa Mungu ni jinsi anavyojitenga na vilivyo vichafu

Maana ya kwanza ya utakatifu wa Mungu ni: “Kutengwa (kuwa mbali) na vyote vilivyo vichafu au najisi.” Maana hii ni muhimu kwa kuwa inahusika katika wokovu. Kwa sababu Mungu ni mtakatifu, hawezi kuwa na ushirikiano na kiumbe cho chote kilicho kichafu au kisicho kitakatifu kikamilifu.

  • Mungu mtakatifu hawezi kushirikiana na mwanadamu mchafu

Tukiiangalia hali ya wanadamu, wanadamu wanazaliwa wakiwa na asili ya dhambi. Dhambi imetuchafua kabisa mbele ya Mungu. Hata matendo yetu ya haki ambayo mtu anaweza kudhani ni safi, yamechafuliwa na dhambi zetu (Isa 64:6). Kwa sababu Mungu ni mtakatifu, hawezi kuwa na ushirikiano na mtu ye yote mchafu wala kumkubali mtu mchafu. Inambidi mtu ye yote anayetaka kukubaliwa na Mungu awe mtakatifu. Mwanadamu asiye na utakatifu kamili mbele za Mungu hawezi kukubaliwa na Mungu wala kuwa na tumaini lo lote la kuwa na ushirikiano na Mungu.

  • Matendo mema ya mtu asiye mtakatifu hayawezi kumpendeza Mungu

Mtu fulani akisema, “Nadhani nitaokolewa kwa sababu nimejitahidi kumpendeza Mungu”, anaonyesha wazi kwamba haelewi maana ya utakatifu wa Mungu. Mwanadamu anayejitahidi kumpendeza Mungu, au anayetenda matendo mema ili ampendeze Mungu, au anayeziacha dhambi, bado ni mchafu mbele ya Mungu kwa sababu ya dhambi zake alizozitenda tayari pamoja na asili yake ya dhambi. Mungu mtakatifu hawezi kushirikiana na mtu kama huyo.

  • Mfano wa chombo cha alizeti kilichotiwa Petroli

Mfano unaofuata unaeleza kwa nini Mungu anatuona kuwa wachafu. Mtu fulani alitafuta chombo cha kuwekea mafuta ya alizeti. Alipata chombo ambacho ndani yake kulikuwa na nusu lita ya petroli. Akasema, “Kuna nusu lita ya petroli tu, na nina lita 20 ya mafuta ya alizeti. Petroli haitaharibu kitu.” Hii ni kweli? Hapana! Ingawa mafuta ya alizeti yanazidi sana kiasi cha petroli, wote tunafahamu kiasi kile cha petroli kitaharibu radha ya mafuta yale. Vivyo hivyo na dhambi pia! Matendo mema mengi hayawezi kufuta matendo mabaya machache au hata tendo baya moja. Lakini je, akimwaga nusu lita ile na kuweka mafuta ya alizeti bila kusafisha kile chombo? Tena, wote tutakubali hata kama chombo kile ni kitupu, kama kiliwahi kutunza petroli, kitaharibu mafuta yale ya alizeti. Hakuna atakayetaka kula mafuta hayo. Ndivyo ilivyo katika maisha yetu. Dhambi, hata kama ni moja tu, inachafua kabisa matendo yetu mema na maisha yetu mbele ya Mungu.

(ii) Utakatifu wa Mungu ni wema wake kamili

Maana ya pili ya utakatifu wa Mungu ni “wema kamili”. Mungu hana kosa wala kasoro yo yote. Ndiyo hali ya Mungu na hali inayotakiwa kwa wote wanaotaka kushirikiana naye Mungu. Kama mtu anataka kushirikiana na Mungu anatakiwa kuwa mtakatifu; anatakiwa kuwa mtu aliyekamilika katika wema wake, yaani asiwe na kosa wala kasoro yo yote.

Lakini ni wazi kwamba kila mwanadamu analo angalau kosa moja. Hivyo hawawezi kuitwa “mwema kamili” wala hawawezi kuitwa watakatifu.

Kwa nini hatuwezi kujiokoa? kwa sababu mwanadamu hawezi kujifanya kuwa mtakatifu na Mungu hashirikiani na asiye mtakatifu

Mungu aliye mtakatifu hashirikiani wala hawezi kumkubali kamwe mwanadamu asiye mtakatifu. Sisi ni wenye dhambi na hatuwezi kujifanya kuwa watakatifu kwa sababu dhambi zetu zimetuchafua kabisa. Hata haki zetu na matendo yetu mema ni najisi mbele ya Mungu. Hatuna tumaini la kujifanya kuwa watakatifu ili tujipatanishe na Mungu na kushirikiana naye. Hatuwezi kujiokoa!

3. Wenye Dhambi Hawawezi Kujiokoa kwa Sababu Mungu ni Hakimu Mwenye Haki.

Zaburi 7:11 – “Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.”

Mungu ni mwenye haki

Tunamaanisha nini tunaposema kwamba Mungu ni mwenye haki? Tunamaanisha kwamba yote Mungu anayoyawaza na kuyatenda ni sahihi. Tena tunamaanisha kwamba Mungu hawezi kulivumilia wala kuliachilia kosa lo lote wala uovu wo wote kwa kuwa ni lazima atende kwa usahihi na kwa haki. Mungu ataziadhibu dhambi zote. Mungu, mwenye haki, hawezi kusamehe dhambi kabla hazijaadhibiwa. Adhabu kwa ajili ya dhambi yo yote ni moja – ni mauti (yaani kutengwa na Mungu milele.)

Watu wengi wanajaribu kuhonga, kudanganya, au hata kuelewana na pepo, roho za mababu, au hata mahakimu kupata yale wanayoyataka. Lakini Mungu, aliye mwenye haki, hayuko kama hawa. Mungu, kama hakimu mwenye haki, hawezi kupokea hongo wala kushawishika kufanya cho chote kisicho haki. Daima Mungu atatenda haki (Kum 10:17).

Mfano wa hakimu mwenye haki

Tunajua hakimu mwenye haki anatakiwa kuwaadhibu wote walio na hatia kwa kuwa wamevunja sheria. Kwa mfano, John na Joseph walifika mbele ya hakimu kutetea misimamo yao. John alileta mashtaka kwamba Joseph aliiba ng’ombe wake. Baada ya kuwasikiliza mashahidi wote, hakimu aliamua kwamba Joseph ana hatia na adhabu yake ni kulipa fidia ya shilingi 245,000/=. Joseph alianza kulia na kumsihi hakimu amhurumie kwa sababu mke wake alihitaji matibabu na hakuwa na hela ya kuyalipia matibabu yake. Hakimu akimhurumia Joseph na kusema kwa sababu ya shida yake, asilipe adhabu yake, je, atakuwa ametenda haki? Hapana! Ni lazima hakimu mwenye haki amwadhibu mwenye hatia. Ndiyo maana ya mfano huu, kama Joseph ni mwenye hatia, hana budi kuhukumiwa na hakimu huyu ili haki itendeke.

Haki ya Mungu inamlazimisha kuhukumu hata yule mwenye kosa moja tu

Watu wengine wanadhani wanaweza kumwomba Mungu ayaangalie matendo yao mema na kuyasamehe makosa yao madogo madogo. Yaani wanataka wapimwe kwenye mizani wakiweka matendo mema upande mmoja na matendo mabaya upande wa pili. Wanadhani kama matendo mema yatazidi yaliyo mabaya, wanastahili kusamehewa. Mawazo kama hayo hayalingani na haki ya Mungu. Mtu akimwomba Mungu kumsamehe hata kosa moja bila adhabu, anaomba Mungu asitende haki. Mungu anaweza kukubali kutenda kisicho haki? Haiwezekani! Mawazo haya yatawafanya watu watupwe motoni kwa sababu Mungu ataiadhibu hata dhambi ndogo moja. Na je, adhabu ya dhambi moja ndogo ni nini? Jibu ni mauti; yaani kutengwa na Mungu milele kwenye adhabu.

Isitoshe, Mungu anasema katika Yakobo 2:10, “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.” Pengine wewe na mimi tungeweza kumsamehe mtu aliyekosea sheria moja tu (ingawa kufanya hivyo kusingekuwa haki). Lakini wote tungekubali kwamba mtu aliyevunja sheria yo yote ile anastahili adhabu. Ndivyo Mungu anavyoona makosa yetu hata kama ni moja. Kukosa mara moja tu, machoni pa Mungu, ni sawa na kuvunja sheria zake zote.

Kwa nini hatuwezi kujiokoa?

Kwa sababu Mungu mwenye haki ataziadhibu dhambi zote. Hatatuhurumia sisi wenye dhambi bila dhambi zetu zote kuadhibiwa. Sisi hatuwezi kufanya cho chote cha kujitetea mbele ya Mungu hata kama tumetenda matendo mengine mema. Sababu ni kwamba adhabu ya dhambi, hata moja ndogo, ni kutengwa na Mungu milele. Matendo mema hayafuti dhambi zetu wala adhabu yake. Hatuwezi kujiokoa!

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *