Home 2020 October 06 Ndivyo Tuhubirivyo

Ndivyo Tuhubirivyo

Ndivyo Tuhubirivyo

“Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini” (1 Wakorinto 15:11)

Mtume Paulo alihubiri SIRI ya Kristo (Warumi 16:25). Mitume kumi na wawili walimfundisha Kristo kulingana na UNABII (Matendo 3: 21-24). Walakini, wote wawili (makundi yote mawili) walikuwa ni mashahidi wa ufufuko wa Bwana wetu, Yesu Kristo!

Mashahidi wa Ufufuko

Wakati wale kumi na wawili walipomwona Bwana aliyefufuka, walipewa jukumu la kushuhudia ufufuko wake kama ishara ya kuwa Masihi kwa Israeli (Mathayo 12:40; Matendo 1:22).

“Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote” (Matendo 4:33)

Kwa upande mwingine, Paulo hakuwa na uhusiano wowote na huduma ya Bwana hapa duniani (katika mwili), wala utume wa wale kumi na wawili, kwa kuwa alikuwa katika kutokuamini mpaka wakati wa Matendo 8 na alikuwa akilitesa kundi dogo, lililokuwa likiongozwa na Petro, kwa kukufuru.

Hata hivyo, katika Matendo 9 Paulo naye alishuhudia ufufuko wa Bwana Yesu Kristo wakati alipomtokea yeye, akiwa njiani kuelekea Dameski.

Kuonekana kwa Bwana kwa Paulo hakukuwa kumetarajiwa na kulikuwa ni kwa kipekee. Paulo (ambaye alikuwa Sauli wakati huo) alikuwa akimkataa Bwana Yesu, na hakuwa na imani naye.

Haya yote yalibadilika wakati Bwana kwa neema yake alimtokea Paulo na kumwokoa, si kwa sababu ya matendo yake, bali kwa sababu ya neema ya Mungu (Waefeso 3: 1-2).

Ilikuwa ni kwa ufunuo ambako Paulo aliteuliwa kuwa mtume wa kuhubiri majira ya injili ya neema aliyopewa na Bwana kwa watu wa Mataifa (Wakolosai 1: 25-27).

Injili ya Paulo ya ‘kutotahiriwa’ ilikuwa tofauti na injili ya Petro ya ‘kutahiriwa’ (Wagalatia 2: 7).

SIRI ya Kristo aliyopewa Paulo ilifichwa kutoka kwa manabii, wakati ambapo ujumbe wa Petro wa utimilifu wa unabii ulikuwa ‘mada’ ya manabii.

Pamoja na hayo, wote wawili walikuwa ni mashahidi wa ufufuko wa Bwana!

Ndivyo Tuhubirivyo

Katika kukataa (kupuuza) ufunuo maalum uliopewa Paulo, 1 Wakorinto 15:11 inatumiwa kama ushahidi kwamba Paulo hakuhubiri chochote kilichotofautiana na Petro. Lakini kinyume na hilo, aya hiyo inaonyesha tu kwamba Paulo na Petro walihubiri baadhi ya mambo yanayofanana:

  • Wote Petro na Paulo walimfundisha Yesu kama Kristo.
  • Wote Petro na Paulo walifundisha kwamba Yesu alitimiza manabii.
  • Wote Petro na Paulo walifundisha wokovu kupitia Yesu Kristo.
  • Wote Petro na Paulo walishuhudia ufufuko wa Yesu.

Paulo anasema kwamba Petro hakuongeza chochote kwenye ujumbe wake, zaidi sana, Paulo alikuwa na mafunuo kutoka kwa Bwana ambayo Petro hakuwa ameyasikia hapo awali (Wagalatia 2: 6; 2 Petro 3:15-16).

“Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo” (Wagalatia 1:12)

  • Paulo alikuwa ni wa kwanza kufundisha SIRI ya Kristo kwa watu wa Mataifa.
  • Paulo alikuwa ni wa kwanza kufundisha UTUKUFU wa msalaba kwa watu wote (Wagalatia 6:14).
  • Paulo alikuwa ni wa kwanza kufundisha UUNDWAJI wa kiumbe kipya kinachoitwa Mwili wa Kristo ambapo hakuna tofauti kati ya Myahudi wala Mmataifa.
  • Paulo alikuwa ni wa kwanza kufundisha wokovu wa BURE kwa watu wote kwa kuzingatia sifa za kifo na ufufuko wa Kristo.

Petro na Paulo walikuwa na huduma tofauti, na injili tofauti, lakini wote walimtumikia Bwana mmoja, na Roho yule yule, kwa utukufu wa Mungu yule yule.

Tatizo la Ufufuo katika Korintho

Wakorintho walikuwa wanapingana kati yao, wenyewe kwa wenyewe, kuhusu utume maalum wa Paulo. Walikuwa pia wakihoji fundisho muhimu la ufufuo.

Takribani 1 Wakorintho sura ya 15 yote, ni utetezi juu ya fundisho la ufufuo halisi wa mwili. Paulo anaanza kwa kuirudia injili aliyowahubiria yeye mwenyewe hapo kwanza. Injili hiyo haikubiriwa kwao na wale kumi na wawili, au na mtume mwingine ye yote yule, isipokuwa yeye Paulo.

Mara tano neno “mimi” limetumika katika 1 Wakorinto 15: 1-3 kuwakumbusha Wakorintho kwamba ni yeye Paulo ndiye ambaye aliipokea injili hiyo na kuwahubiria wao Wakorintho na ambayo waliiamini.

Injili ya Paulo imeelezwa wazi katika 1 Wakorinto 15: 3-4:

“Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko”

Injili ya Paulo ni tofauti sana na injili ya wale kumi na wawili…

Baada ya kuitetea (kuifafanua) injili yake, Paulo anatoa kauli hii, kwamba, “ikiwa ni mimi au wao, ndivyo tunavyohubiri, na ndivyo mlivyoamini” (1 Wakorinto 15:11).

Ikiwa Paulo alikuwa na injili tofauti na Petro, ni nini basi wote wawili walikihubiri? Jibu linapatikana katika mstari ufuatao:

“Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?” (1 Wakorinto 15:12)

Petro na Paulo wote walihubiri kwamba Kristo alifufuka kutoka kwa wafu. Wote wawili walishuhudia ufufuko wake.

Hii ni kauli inayofaa kwa watu ambao walikuwa wakihoji utume wa Paulo na fundisho la ufufuo. Paulo anasema kwamba, “ye yote ambaye unadai kumfuata, ufufuo unafundishwa.”

Petro hakuhubiri siri ya Kristo, wala Paulo hakuhubiri kuja kwa ufalme hivi karibuni kwa Israeli. Itakuwa unafanya makosa makubwa kufikiria kwamba Paulo na Petro, wote walifundisha kila kitu sawa. Ni makosa vile vile kufikiri kwamba Paulo na Petro walifundisha kila kitu tofauti.

1 Wakorinto 15:11 inaonyesha kuwa wote wawili walikuwa ni mashahidi wa ufufuko wake halisi wa mwili kutoka kwa wafu.

Kwa Utukufu wa Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *