Home 2020 October 03 Vizuizi vya Kuamini

Vizuizi vya Kuamini

Vizuizi vya Kuamini

Katika kufanya uinjilisti wa mtu kwa mtu ni lazima utakutana na vizuizi mbalimbali. Maana, tunajua kuwa kazi hiyo ni ya kiroho na mpinzani wa mambo ya kiroho yupo. 2 Wakorintho10:3-5 inasema, “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.”  Shetani hawezi kutulia na kuona wafuasi wake wanavuliwa na kuacha njia zake, lazima ainuke na kufanya bidii kuzuia mafanikio katika uinjilisti wetu. Ndiyo maana ni muhimu kazi ya uinjilisti ifanyike kwa kumtegemea Roho Mtakatifu, nguvu zake za kuokoa, na uwezo wake wa kumshinda adui. Katika sehemu hii tutajifunza jinsi gani Shetani anavyoleta vizuizi ili watu wasiamini Kristo. Kazi yetu ni kutumia silaha za roho ili tushinde vizuizi vya Shetani na watu wapate kumtii na kumkiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao.

Sasa tuangalie vizuizi vikubwa vitano tunavyoweza kukutana navyo tukiwa kwenye uinjilisti.

1.          “Ningependa kuokolewa, lakini nafahamu kwa hakika kwamba nitashindwa kuishi maisha mazuri ya Mkristo wa kweli.”

Mara nyingi mtu unayemshuhudia hawezi kukitamka kizuizi hicho wazi, anakataa kuamini lakini hasemi kwa nini. Ukigundua hicho kuwa ndicho kizuizi kwake, unatakiwa ufanye nini? Kwanza ni vizuri kwa kuwa mtu huyo tayari ameshafahamu nia ya Mungu ambaye hutaka watu wabadilike na kuwa watu wazuri. Tatizo la mtu huyu ni mtazamo aliyonao ambapo anaona kuwa atashindwa kubadilika akijua kuwa uwezo wake wa kufanya hivyo ni mdogo. Anachokosea ni kwamba hajagundua kuwa hakuna awezaye kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwa uwezo wake yeye mwenyewe binafsi. Kushinda na kubadilika kunategemea uwezo wa Mungu uliopo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mtu huyu anastahili kufundishwa juu ya kazi ya Roho Mtakatifu na jinsi Mungu anavyomwezesha Mkristo kubadilika baada ya kuokolewa na kuanza maisha ya kumfuata Kristo.

2.          “Marafiki na jamaa zangu watanicheka na kunidharau nikiwaambia nimeamini na kuokolewa.”

Yesu Kristo aliyajua mawazo haya alipowaambia wanafunzi wake katika Luka 9:26, “Kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.”

Kizuizi hiki kinaweza kuondolewa kwa kumweleza msikilizaji mambo yafuatayo:

  1. Kukubaliwa na Mungu ni jambo la muhimu zaidi kuliko kukubaliwa na wanadamu.
  2. Watu wasiomfahamu Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao daima hummdharau, na tena Biblia inasema kwamba habari ya Injili ni upuuzi kwao (1Wakorintho 2:14) kwa sababu
  3. Akumbuke kuwa, mwisho wa yote, atakufa peke yake na baada ya kifo hicho atakabiliwa na hukumu, yaani atasimama mbele za Mungu peke yake. Kama atamkubali Yesu atabadilishwa na atapata nguvu za kuwashuhudia na hata wale waliokuwa wakimcheka ili nao wapate pia kuamini habari za Yesu badala ya kupotea.

3.          “Mimi siyo mtu mbaya na siamini kwamba Mungu atanihukumu kama unavyonieleza.”

Mtu huyu ameziamini akili zake na mawazo yake binafsi kuliko neno la Mungu. Kumpokea Kristo hakupatikani kwa kujiamini kibinafsi bali ni kwa kumwamini Yesu Kristo na neno Lake. Mara nyingi kizuizi hicho utakisikia kwa wasomi na kwa wale wenye mali nyingi. Kristo mwenyewe alisema, “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani” (Yohana 5:24).

4.          “Mimi nimefanya dhambi nyingi na hata ile ‘dhambi isiyoweza kusamehewa’.”

Mtu huyu anahitaji kufafanuliwa juu ya “dhambi isiyoweza kusamehewa”, hii ilikuwa ni dhambi ya kusema kwamba uwezo na ishara za Yesu Kristo ziliwezeshwa/zilitokana na Shetani na kwamba hazikuwa nguvu za Roho Mtakatifu zilizokuwa zikifanya kazi ndani yake/pamoja naye. Yaani, ni dhambi ya kumwasi Kristo. Leo mtu anayekataa kumwamini Kristo, ndiye anayemwasi Kristo na akiendelea kufanya hivyo hadi kufa kwake, atapotea milele! Lakini ye yote anayemwamini na kumpokea Kristo anasamehewa dhambi zake zote na anapata kuwa kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17). Hakuna dhambi isiyosameheka, isipokuwa kutokuamini.

Soma Zaburi 103:3, 10, 12: “Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala kutulipia kwa kadiri ya maovu yetu. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.”

 VIZUIZI VINGINE VINAVYOSUMBUA

Vizuizi vingine vipo vingi, vifuatavyo ni baadhi ya vizuizi hivyo, visome kwa makini na jaribu kuandika jinsi ya kuvishughulikia na kuvijibu:

  1. Unaposhuhudia mtu mmoja, mwingine akaongezeka, na mwingine tena mpaka umati ukawa mkubwa; hivyo kumfanya msikilizaji wako akose kusikiliza vizuri na kuamini kwa kuwaogopa wale
  2. Mtu unayemshuhudia anakuwa na shughuli nyingi. Unapoendelea kumweleza Injili anaangalia saa yake na kutafakari juu ya mambo mengine, na hata kuinuka na kuanza kufanya mambo mengine badala ya kusikiliza kwa kina ujumbe
  3. Mtu anasikiliza Injili lakini inakuwa kuwa ni jambo geni kwake.
  4. Mtu anayaogopa mabadiliko magumu ya kuachana na maisha yake ya zamani na pengine hata marafiki zake na familia
  5. Mtu amezaliwa katika dini ya wazazi wake na hataki kuiacha dini yake wala kuamini ujumbe wako ingawa dini yake inakataa wokovu

NB: Unaweza kuongeza vizuizi vingine unavyovijua wewe………………………………………………………………………………….

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *