Home 2020 September 29 Maana ya Ubatizo

Maana ya Ubatizo

Maana ya Ubatizo

Neno “UBATIZO” linatokana na neno la Kiyunani “βαπτιζω” ambalo herufi zake zinasomeka “BAPTIDZO”. Neno hili halimaanishi kunyunyizia (sprinkle) au kumwagia (pour). Neno hili linamaanisha Kuzamisha (to dip) au kutumbukiza (to immerse). Kumbe basi, neno “BAPTIDZO” lina maanisha “UBATIZO WA MAJI MENGI” ambapo mtu huzamishwa mwili wote.

Yesu alibatizwa ubatizo wa maji mengi, kwa kulithibitisha hilo tunaona katika Mathayo 3:16 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake”

Mitume nao waliwabatiza watu kwa maji mengi. Matendo 8:36-39. “Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? …wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha walipopanda Kutoka majini…”

Yohana alikuwa akibatiza hata baada ya Yesu kuanza huduma, alikuwa akibatiza katika maji mengi Yohana 3:22-23 ” Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji mengi; na watu wakamwendea, wakabatizwa.”

Je, Ili Tuokoke ni Lazima Tubatizwe?

Hapana! Tunapokea wokovu kwa kukiri kwa vinywa vyetu (Warumi 10:9-10). Kwa mujibu wa Neno la Mungu, Ubatizo siyo jambo linalohitajika ili mtu apate wokovu. Hatupati wokovu kwa matendo ya mwili, bali tunaupokea wokovu kwa Neema kwa njia ya Imani (Matendo 15:11; Warumi 4:1-25; Wagalatia 2:16; Waefeso 2:8-9; Wafilipi 3:9).

Kama UBATIZO wa maji ulihitajika ili watu waokoke (wapate wokovu), tungetarajia mahali pote ilipohubiriwa injili watu wangebatizwa. Paulo hataji UBATIZO kama hitaji muhimu katika wokovu (elements of salvation). Tunaona katika 1 Wakorintho 15:1-4 “…na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure…” Katika 1 Wakorintho 1:17 Paulo anasema “Kristo hakunituma ili nibatize bali nihubiri Habari Njema”. Andiko hili liko wazi kabisa kuonyesha tofauti ya UBATIZO na WOKOVU.

Kama ni lazima mtu abatizwe kwanza ndipo aokoke, ilikuwaje Paulo ahubiri Injili na si Ubatizo? Kumbuka Injili ndio uweza wa Mungu uletao Wokovu (Warumi 1:16)!

Mifano ya Watu Waliopokea Wokovu Bila Kubatizwa

1: Mwanamke Kahaba

Yesu alimwambia mwanamke kahaba katika Luka 7:37-50″…Umesamehewa dhambi zako…, imani yako imekuokoa”

2: Mwanamke Aliyepooza

Yesu alimwambia yule mwanamke aliyepooza katika Mathayo 9:2″ Jipe moyo mkuu mwanangu, umesamehewa dhambi zako”.

3: Mtoza Ushuru

Yesu alitoa mfano wa mtoza ushuru kuwa alisamehewa dhambi kwa kukiri kwa kinywa chake na si kwa kubatizwa (Luka 18:13-14).

4: Muovu Msalabani

Yesu alimwambia muovu msalabani “Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi (paradiso)”. Hapo hakuna ubatizo wa maji uliofanyika (Luka 23:39-43).

Mifano hii yote inathibitisha kuwa msamaha wa dhambi ni tofauti na UBATIZO wa maji. Kwa msingi huo basi, hatuna kumbukumbu ya mitume kubatizwa katika maji, ila badala yake Yesu anasema katika Yohana 15:3 “Mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia” na katika Luka 10:20 Yesu anawaambia wafurahi kwa kuwa majina yao yameandikwa mbinguni.

Kuna maandiko mawili yanayochanganya watu kwa jinsi UBATIZO na WOKOVU ulivyotajwa pamoja. Katika Matendo ya Mitume 2:38 Inasema “Tubuni mkabatizwe…, mpate ondoleo la dhambi, …” Inamaanisha kwamba ubatizo wa maji hauhitajiki ili mtu aokoke bali ni hatua ya pili ya nje baada ya hatua ya kwanza ya ndani ya kutubu dhambi. Hii ni hatua ya pili ya nje (kimwili) baada ya hatua ya kiroho!

Pia katika Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” Pia hapo tunaona asiyeamini ndiye atakaye hukumiwa na sio asiyebatizwa. Hapa napo ubatizo unatajwa kama hatua inayofuata baada ya kuamini kiroho.

Mambo Matatu Yahusuyo Ubatizo

Ubatizo hutupatia mambo matatu kutokana na Warumi 6:1-10 “…Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? …Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake…”

  • Ubatizo ni ishara ya kufa, kuzikwa na kufufuka kwa Kristo.
  • Ubatizo ni ushuhuda kwetu kuwa tumeoshwa dhambi zetu.
  • Ubatizo ni uthibitisho wa kuwa sisi ni Wakristo (Warumi 6:3-4)

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *