Home 2020 September 24 Ujumbe Wetu Katika Uinjilisti

Ujumbe Wetu Katika Uinjilisti

Ujumbe Wetu Katika Uinjilisti

Ukichunguza jumbe mbalimbali ninazohubiriwa siku hizi zinazoenezwa kwa jina la “Habari Njema” unaweza kushangaa sana. Kwa sababu hiyo, inatupasa kulichunguza suala hili kwa kina zaidi na inawezekana utakuta hata wewe umeingia kwenye mtego huo wa kubadilisha ujumbe unaotakiwa kushuhudiwa. Tuanze kwa kujiuliza, je, Injili tunayoshuhudia ni ipi, ndipo tuziangalie jumbe mbalimbali zinazohuburiwa siku hizi ambazo si Injili za kweli. Mwishoni, tutafafanua ujumbe wa kweli wa kushudia ili wote tuweze kuueleza na kuukumbuka bila kuubadilisha.

INJILI TUNAYOPASWA KUIENEZA

Paulo aliieleza Injili kwa kifupi katika 1 Wakorintho 15:1-4 akisema: “Nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyohubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko.”

Tena katika 1 Wakorintho 2:2 alijumlisha ujumbe huo kwa kusema, “Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.” Petro alitoa muhtasari mzuri sana wa Injili katika 1Petro 3:18 “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa.”

Tunafikiri tungeweza kuyaangalia/kuyapitia maandiko mengi zaida ya haya lakini msimamo letu umeshakwisha kujulikana kwamba ujumbe wetu hasa ni juu ya KRISTO YESU NA KUFA KWAKE KWA AJILI YA DHAMBI ZETU ILI TUPATE KUSHIRIKIANA NA MUNGU. Mambo mengine yanayochanganywa na habari hii siyo Injili ya kweli. Baada ya kujifunza hayo tuzichunguze jumbe mbalimbali zinazohubiriwa siku hizi ambazo zinaongeza au zinapunguza ujumbe huo tunaopaswa kuutangaza.

INJILI NYINGINE ZINAZOHUBIRIWA SIKU HIZI

Mtume Paulo aliowaonya sana watu wa mji wa Galatia alipokuta wameanza kuifuata injili nyingine. Hebu tujifunze umuhimu wa suala hilo kwa kusoma onyo lake: “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe” (Wagalatia 1:6-9). Baada ya kusoma onyo hilo tunapata sababu ya kujichunguza ili kuhakikisha injili tunayo ihubiri ni ya kweli. Maana hatutaki kuingia katika kosa la kuubadilisha ujumbe wa kweli. Kuna injili za aina mbalimbali zinazo hubiriwa na wainjilisti mbalimbali hivi leo ambazo si injili za kweli!

1. Injili ya Matendo (Sheria)

Injili hii inatangaza kwamba kazi ya Kristo Yesu msalabani haikutosha kulipia wokovu wetu. Inadai ni lazima uongeze masharti/matendo fulani yaliyowekwa na wanadamu ili uokoke. Kawaida masharti haya ni kama vile kutoa sadaka mbalimbali, kuhudhuria kanisani, kuungama dhambi, kubatizwa kwa maji, au kufanya matendo mengine ya haki. Lakini Biblia inaeleza wazi katika Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu” na Tito 3:5 “Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu” kwamba hakuna matendo yo yote yanayoweza kukuokoa wala kuchangia wokovu wako.

Baadhi ya viongozi wa makanisa hawapendi kumpa Kristo utukufu wake kamili katika uwezo wake wa kuokoa. Hawapendi kufanya hivyo kwa sababu wanaogopa waumini wapya wakifahamu Yesu peke yake amefanikisha wokovu wao, waumini hawa wapya hawatashiriki shughuli za kikanisa kikamilifu wala kuchangia kanisa kama shukrani yao kwa ajili ya mchango wa kanisa katika wokovu wao. Yaani, wanataka waumini wapya kuamini kwamba kanisa limechangia wokovu wao ili wajitoe kanisani kama shukrani. Lakini, kumbe, kanisa halichangii cho chote kwenye wokovu wa mtu. Wengine wanaweka sheria nyingi zinazohusu vyakula, siku, vinywaji, na hata nguo na nywele wakiwa wameshindwa kutambua kwamba, “Hakuna mwenye mwili atakayehesibiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria” (Warumi 3:20; Wagalatia 2:16). Hiyo ndiyo injili mbaya ambayo iliwapata watu wa Galatia na mtume Paulo aliwaonya vikari sana kuhusu hatari ya injili hiyo.

2. Injili ya Kuachana na Dhambi na Kuwa Mtakatifu

Tunaamini kwa moyo wetu wote kwamba wanaoihubiri injili hii hawana makusudi mabaya. Lakini wameshindwa kuelewa maana ya kuokoka. Ukiwauliza hawa jinsi ya kuokoka, bila shaka watajibu unahitaji kumwamini Yesu lakini pia wataongeza hitaji la kuachana kabisa na dhambi kwanza. Hapo juu tulieleza Injili ya kweli inasema Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Katika kuzifia dhambi zetu, aliweza kuondoa adhabu ya dhambi zetu (mauti ya milele) na pia aliweza kutupatia sisi tuliookoka nguvu ya kushinda dhambi tukimruhusu Roho Mtakatifu kutawala katika maisha yetu ya kikristo baada ya kuokoka (Waefeso 5:18). Wanapokosea katika injili hii ya uongo ni pale wanaposema waliookoka ni wale walioachana na dhambi kabisa. Hakuna mwanadamu anayeweza, katika nguvu zake mwenyewe, kabla hajaokoka, kuachana na dhambi kwanza ili amwamini Yesu na kuokoka. Ni lazima aokoke akiwa mwenye kutenda dhambi na baada ya kuhuishwa na Kristo katika wokovu wake, ndipo ataweza kutotawaliwa na dhambi.

Wengine wanaohubiri injili hii ya kuachana na dhambi, hudai kwamba baada ya kuokoka Mkristo hatatenda dhambi tena. Huu, nao, ni uongo mkubwa. Ni kweli mtu aliyeokoka siyo mtumwa tena wa dhambi na kwa kumtegemea Roho Mtakatifu katika maisha yake ataweza kupunguza kiasi cha dhambi katika maisha yake. Lakini mpaka Wakristo watakapopewa miili ya utukufu wataendelea kutenda dhambi mara kwa mara kutokana na asili yao ya dhambi.

Uongo huo, wa kusema Wakristo hawatendi dhambi, husababisha wengine kukataa kuokoka kwa sababu ni wazi hata anayewahubiria bado anatenda dhambi. Sababu hata Wakristo wanaendelea kutenda dhambi ni kwa sababu dhambi inafanyika katika mawazo, moyo, matendo, maneno, makusudi, na hata katika kutofanya kitu fulani kinachopaswa kufanywa (Yakobo 4:17). Dhambi ni kukosa kutimiza mapenzi na makusudi yoyote ya Mungu. Wakristo wanajitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu lakini kutokana na udhaifu wao wanashindwa katika sehemu nyingine mara kwa mara. Dhambi zinatendeka kila siku na watu wote duniani, hata Wakristo. Tazama 1 Yohana 1:8-10, “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

Kuhubiri injili hiyo inawakatisha tamaa wenye dhambi. Maana walevi na washerati wanakosa kuamini kwa vile wamekuwa watumwa wa tabia zao na hawawezi kuachana na dhambi zao ili waje kwa Yesu. Lakini tukiwaalika kwa Kristo kama walivyo na kuwaonesha kwamba Kristo anaweza kuwapa nguvu ya kushinda dhambi, Injili ya namna hii wataipokea. Tuangalie tusije tukabadilisha maana ya kuokoka na kumfanya aliyetufia awe mwongo!

3. Injili ya Raha (Starehe)

Injili hii inatangazwa sana kwa watu walio maskini na wenye kuhangaika na matatizo mengi. Injili hii huahidi kwamba shida zako zote zitaisha mara utakapomkubali Kristo kuwa Mwokozi wako. Injili hii mara nyingine inaahidi msaada wa kimwili na hata kutarijika na kuachana kabisa na umaskini. Lakini Yesu mwenyewe aliita watu kuachana na mambo ya kidunia akitaka wafuate mambo ya kiroho. Kwa mfano alimwambia yule tajiri kuuza yote alivyonavyo na kuwagawia maskini, kisha amfuate.

Ni udanganyifu mkubwa kumwaahidi mtu kwamba mume wake hatampiga tena kama atampokea Kristo. Ni kosa kubwa kumwambia mtu kwamba ataanza kula wali kwa nyama akimpokea Yesu Kristo badala ya ugali kwa maharage. Biblia haina injili kuhusu utajiri wala raha za kidunia. Tunachohubiri kutoka kwenye Biblia ni kwamba Kristo ataingia ndani yako na kukusaidia kupita katika shida nyingi ulizo nazo. Kristo, ukimruhusu, anaweza kukupa amani katika mateso na ugonjwa ulionao. Lakini Kristo hajaahidi Wakristo hawatakuwa na matatizo katika dunia hii. Mara nyingine mtu anapookoka ndipo shida zinaanza kuwa kali zaidi kwa vile Shetani amechukia wokovu wake na hutaka kumwangusha. Tusiwadanganye watu ili waumini kwa kuwa wasipotimiziwa ahadi hizo za kimwili watamwacha Kristo mara watakapokutana na ugumu maishani mwao.

4. Injili ya Ishara za Kimwili

Injili hii inahubiriwa sana na wahubiri wale Wakubwa wakubwa wanaofanya mikutano mikubwa. Mara nyingi wanahubiri vizuri sana, tena kwa usahihi, kuhusu wokovu ulio ndani ya Kristo Yesu bila matendo. Lakini baada ya kualika watu kumpokea Kristo kuwa Mwokozi wao, kwa njia ya imani, nyongeza zingine hutokea. Kwa mfano, mara nyingine wanasema kwamba watu wataponywa kimwili badala ya kuwaonyesha thamani ya jinsi Mungu alivyowaponya kiroho ili wasihukumiwe Jehanamu. Au, wanaanza kuwaombea watu wakitafuta ishara kama kunena kwa lugha ili ioneshe mtu amejazwa na Roho Mtakatifu. Lakini Biblia inafundisha karama hii ilitolewa kwa wachache wakati wa mitume, siyo kwa wote (1 Wakorintho 12:30).

Wanadamu wanao ugonjwa mkubwa sana wa kutaka kuona mambo ya kiroho kwa macho yao ya kimwili, wanataka kuamua wenyewe kuhusu ishara za Mungu. Tunaamini kabisa kwamba Mungu huponya watu wake pale anapotaka yeye. Lakini pia, tumeyaelewa Maandiko Matakatifu kwamba ishara hizo zimeisha kutokana na kukamilika kwa Biblia (1 Wakorintho 13:8-13). Hata wale wanaoamini kuwa ishara hizo bado zipo leo, wanakubali kwamba haieleweki kwa nini wengi hawaponi au kupata ishara hizo kama watakavyo!

Ubaya wa injili hii ni kwamba inapotosha wasikilizaji wengi, wasipoona au wasipopata ishara hizo wanaona hawajaokoka kweli kweli. Lakini wokovu hauwezi kuhakikishwa kwa mambo ya kimwili bali unahakikishwa na Roho Mtakatifu ndani yetu akitumia Neno la Mungu (1 Yohana 5:13; Warumi8:16). La kusikitisha zaidi ni kwamba injili hii inasisitiza sana mambo haya ya ishara na mara inaacha Neno la Uzima linalookoa.

5. Injili ya Kidhehebu

Injili hii inatangazwa sana ikiwa na kusudi kuu la kuongeza wanachama (washirika) wa kanisa au dhehebu fulani. Siku hizi badala ya kuzitanguliza habari za Kristo Yesu na kutaka kuona watu wakiingia katika Kanisa lililo Mwili wa Kristo, wainjilisti wanatangaza uzuri wa madhehebu yao na kujaribu kuonyesha jinsi yalivyo bora wakilinganisha na madhehebu mengine.

Wahubiri wa injili hii wanasema mtu atakuwa amekata shauri tu ikiwa amejiunga nao, hata kama mtu huyu ni mshirika wa kanisa lingine aliyeokoka tayari. Wanawabatiza upya kana kwamba wanapokea wokovu kwa mara ya kwanza, wakati wanachokifanya ni kubadilisha kadi ya chama chao tu. Wengine wanadai kwamba hakuna waliookoka nje ya dhehebu lao. Tuna uhakika kwamba wazo hilo linamsikitisha sana Mungu ambaye anataka waliookoka wote kuwa ndugu katika Bwana kwa sababu wote ni sehemu ya Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Waliookoka wanapaswa kuungana na kuzitumia nguvu zao kuwafuata na kuwaokoa waliopotea kwa kuwahubiria Injili ya kweli kuhusu Yesu Kristo. Mungu hakuanzisha dhehebu lo lote, wanadamu hupenda kutengana na kuvutana lakini Mungu hutaka umoja. Hatusemi kwamba tungeweza kuungana na kuwa dhehebu moja, bali tusaidiane katika kazi hii ya kuitangaza Injili ya kweli bila kujali mwongofu atajiunga na dhehebu gani, ikiwa tu amejiunga na Kristo mwenyewe!

Shetani hutumia aina zote hizi tano za injili za uongo kupunguza na kuondoa watu kutoka katika Injili ya kweli kwa kuwa amegundua uwezo wa Injili ya kweli (Warumi 1:16). Tujichunguze na kuhakikisha tunamhubiri Kristo na kazi yake ya kuokoa na siyo kuhubiri moja ya mitego hiyo iliyotajwa hapo juu.

UJUMBE WA KWELI UNAOFAA KUHUBIRIWA

Tunapenda kuelezea ujumbe tunaopaswa kushuhudia katika sehemu tatu ili kueleweka kiurahisi.

1. Watu wote ni wenye dhambi na wanastahili kuhukumiwa au kupata adhabu.

Mtu asipoweza kugundua upungufu wake na kukubali hali yake ya dhambi inayomfanya kupotea na kumtengana na Mungu milele, basi, hataweza kuona hitaji lake la kupata ukombozi. Vifungu vinavyoweza kumsaidia na kumwonesha haya ni: Warumi 3:10, 11, 23; Isaya 53:6; 1 Yohana 1:8, 10; Waefeso 2:1-3, 5; Warumi 6:23; Waebrania 9:27; Isaya 59:2.

Katika kushuhudia ni muhimu kuwa upande wa msikilizaji na kukubali kwamba wewe mwenyewe ni mwenye dhambi kama yeye. Kujionyesha kwake kuwa wewe huna dhambi itamfanya msikilizaji kujiweka hivyo pia ili afanane na wewe. Mara nyingi itabidi umfafanulie maana ya dhambi kwa kuwa watu wengi wanadhani dhambi ni makosa makubwa tu.

2. Yesu Kristo alikufa ili aziondoe dhambi zetu na atuokoe

Mtu akishaitambua hali yake ya kupotea na hali yake ya kuwa chini ya adhabu; ndipo utapaswa kumwonesha ukombozi wa Kristo. Mungu alifanya mpango wa ajabu kwa kumtuma Yesu Kristo kutuokoa wanadamu tuliopotea (Warumi 5:8; 8:1; 1 Petro 3:18; Yohana 3:16; 2 Wakorintho 5:17, 21; Waefeso 2:4-6; Yohana 14:6; Matendo ya mitume 4:12). Alifanya hivi kwa sababu mtu asingeweza kujiokoa mwenyewe kwa njia yo yote ile (Mathayo 14:12; Waefeso 2:8, 9; Tito 3:5; Isaya 64:6; Warumi 3:20, 28).

3. Mtu huokoka kwa kumwamini Kristo kama mwokozi wake binafsi

Hatua hiyo ni ya muhimu sana kuonesha kwamba mtu hupata kufaidika na kazi ya Kristo akigeuka na kumwamini Kristo kama Mwokozi wake binafsi. Kufanya hivyo kunafanya Injili iwe hai kwake. Mistari ya kusaidia ni: Warumi 10:9, 10, 13; Yohana 1:12; 1 Yohana 5:11, 12; Mathayo 11:28; 1 Yohana 1:9; Matendo 16:31.

Kwa kuzifuata na kuzijua sehemu hizi tatu za Injili, mwinjilisti atakuwa ameweza kulitumia neno la Mungu kumsaidia mtu ili aweze kuokoka. Katika maandalizi, ni vizuri kwa mwinjilisti kukariri vifungu vingine au kuweka alama kwenye Biblia yake na kuandika maelezo pembeni ya mistari.

Kwa Utukufu Wake Kristo

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *