Home 2020 September 09 Maandalizi ya Mwinjilisti

Maandalizi ya Mwinjilisti

Maandalizi ya Mwinjilisti

Katika kazi yo yote ambayo mwanadamu huifanya huwa inakuwa na maandalizi yake. Wengine huamini kwamba mtu akishajua Yohana 3:16 basi aondoke akaihubiri hiyo hiyo. Kama ingekuwa ni kuendesha gari, je tungeweza tu kumwambia mtu kuwa, “hiki ni kifaa cha moto (Accelerator), kanyaga gari itaenda”. Halafu tumpe funguo za gari na tumwache aondoke na gari letu la thamani? Hapana, maana atakanyaga na kwenda bila kujua kazi ya usukani wala ya breki. Mwisho wake atagonga kila kiumbe kilicho njiani na atashindwa kusimama hadi mafuta yatakapoisha! Basi, hali kadhalika tusikimbilie kufanya kazi ya uinjilisti hivyo. Maana, ajali nyingi zinatokea katika mambo ya kiroho kwa sababu hiyo na pia tufahamu kuwa ujumbe tuliokabidhiwa ni wa thamani kuliko thamani ile ya gari.

Kosa moja kubwa linalofanyika kwa wale walio na haraka kuieneza Injili bila kujiandaa, ni kwamba wainjilisti hawa wenyewe hawajapata kubadilika kuwa kielelezo cha ujumbe wao. Kristo aliwaita wanafunzi wamfuate ili wajifunze kwake kwanza kisha aliwatuma kuwahubiria wengine. Sisi hatuwezi kuwasaidia wengine kuhusu uzima wa milele mpaka uzima huo umekaa ndani yetu kabisa. Naamini kuna kazi mbili za mwinjilisti, ambazo ni, (1) Kutangaza na (2) Kuthibitisha habari njema ya wokovu. Kutangaza ni rahisi na inawezekana mara moja, lakini kuthibitisha ni kuonesha mfano kupitia maisha yako ya siku hadi siku jinsi wokovu unavyombadilisha na kumboresha mwanadamu. Kuthibitisha huku hufanya ujumbe unaotangazwa kuwa hai.

Mapendekezo yafuatayo yaweza kukuongoza unapojiandaa kwenda kufanya uinjilisti wa mtu kwa mtu:

Uwe Mtu wa Maombi

Ukisoma Warumi 10:1 utaona Paulo alisema, “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.” Paulo aligundua nguvu za maombi. Mungu hufurahi tunapompelekea hitaji la wokovu wa marafiki zetu, ndugu na watu wanaotuzunguka. Pia maombi ya kumsihi Mungu atuletee mtu sahihi tunayetakiwa kumshuhudia ni maandalizi muhimu ya kuyafanya. Maombi ndiyo nguvu ya uinjilisti kwa vile uinjilisti ni kazi ya kiroho siyo ya kimwili.

Uwe Mnyenyekevu

Mtu anayefanya huduma ya uinjilisti ili aonekane au atambulike atashindwa kufanya kazi yenye matunda. Wengi katika uinjilisti wa mikutano hufurahishwa na hali ya kuwa mbele ya watu. Lakini uinjilisti wa mtu kwa mtu ni wa siri ukilinganisha na ule wa hadharani. Maana hakuna mtu atakayekufuata ili akusifu au mtu atakayekurekodi video au kukupiga picha ya jinsi unavyofanya uinjilisti au ulivyoingia nyumbani mwa mtu fulani na kumwelezea Habari Njema za wokovu wa Mungu. Yohana Mbatizaji yu mfano mzuri sana kwetu. Alijiita, “Sauti ya mtu aliaye nyikani” (Yohana 1:23). Baadaye, wakati wanafunzi wake walipogundua kuwa watu wengi wanazidi kumwacha na kumfuata Yesu waliona wivu na wakamwuliza Yohana juu ya ja,mo hilo. Jibu lake linaeonesha unyenyekevu unaotakiwa kuigwa nasi, “Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye (Kristo) hana budi kuzidi, bali mimi kupungua” (Yohana 3:30).

Inatupasa sisi tujitambue kuwa tu watumishi wa watu tunapowashuhudia injili ya Kristo (1 Wakorinto 4:5). Watu wenye kiburi hawawezi kuthibitisha Injili kwa wale wanaowahubiria kwa kuwa ndani yao hujenga adharau kwa wale wanaowahubiria habari hizo za kristo. Sijajua ni kwa nini siku hizi wainjilisti wengi wanaongea kwa ‘ukali’ wanapohubiri ujumbe wa upendo huu wa ajabu, ambao Mungu ametuonyesha.

Uwe Mtu Mwenye Fadhili

Mtu mwenye fadhili hutafuta nafasi ya kuonesha upendo na fadhili kwa watu wanaomzunguka. Kwa njia hii anathibitisha ujumbe wake. Vilevile watu watakaposikia maneno yake watayathamini na kuyatilia maana kwa vile ameshawashuhudia kwa matendo yake mema (Mathayo 5:16).

Ushuhuda hauwezi kuwa kamili tukiwahubiria watu tu bila kuwasaidia pia. Kila wakati, kulingana na jinsi vile Mungu ametujalia, tunapaswa kuwasaidia mahitaji na matatizo yao mengine tukiwafariji na kuonesha uradhi wetu wa kuwasaidia kimwili. Tukiishi hivyo tutajulikana hivyo na mwisho tutakapopata nafasi kumshuhudia Kristo ujumbe wetu utasikilizwa na kukubalika kirahisi.

Uwe Mtu wa Kujikana na Kutanguliza Injili Mbele Kuliko Manufaa ya Kimwili

Mtu hawezi kufanya kazi ya kueneza Injili kikamilifu kama ana mawazo kuhusu faida yake binafsi. Maana huduma hiyo haina faida ya kimwili kwa ajili ya mwinjilisti mwenyewe. Bali, huduma inawalenga hasa wapotevu na Mungu. Mwinjilisti hawezi kusaidia mahitaji ya wengine ikiwa macho yake yanajiangalia yenyewe. Atakosa kugundua mahitaji ya wapotevu, nao hawataweza kuitikia ujumbe wake wa wokovu.

Paulo alisema katika 2 Wakorintho 12:15 kwamba alikuwa radhi kutapanya na kutapanywa kwa ajili ya roho za watu. Maana yake ni kwamba alijinyima kwa hiari yake ili watu wapate kusikia Injili na kuokoka. Tunapotanguliza furaha ya dunia hii hatuwezi kutazamia kufanya uinjilisti wenye matokeo yo yote. Yesu mwenyewe aliwaelezea wanafunzi wake kwamba mtu hawezi kushika plau kisha akaangalia nyuma. Mkulima wa namna hii atalima matuta yasiyofaa na kuleta uharibifu shambani kwake kuliko faida (Luka 9:23).

Uwe na Imani Kubwa Katika Uwezo wa Bwana Kuwaokoa na Kuwabadilisha Wenye Dhambi

Kutangaza habari hii ya nguvu, lazima sisi wenyewe tuwe tumeshakuwa na uhakika kuhusu uwezo wa Bwana kuokoa ili tuwe kama mtume Paulo aliyesema, “Siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16). Paulo aliamini kwamba Mungu hawezi kushindwa kumwokoa mtu ye yote yule anayeamini. Je, nasi tunaamini hivyo? Au mara nyingi tunawaza, “Huyu ni mbaya, hawezi kubadilika na kuokoka.” Kumbuka kwamba, “Mungu hapendi mtu ye yote apotee” (2 Petro 3:9).

Paulo mwenyewe alifahamu haya kwa sababu yeye alikuwa mwuaji aliyelitesa kanisa kabla hajaokoka. Lakini Mungu aliweza kumwokoa pamoja na ubaya wake wote. Kumbuka hata Musa na Daudi walikuwa wauaji, nao wakapata neema kutoka kwa Mungu wakasamehewa! Je, kuna dhambi kubwa kiasi gani Mungu hawezi kuisamehe? La! Hasha!

Uwe Tayari Kupiga Vita Kuwaonesha Watu Faida ya Wokovu kwa Mfano Halisi wa Maisha Yako

Kwanza lazima wewe mwenyewe uwe umeokoka kweli kweli na uwe na uhakika kuhusu wokovu wako. Pili, wokovu wako unapaswa kuwa umekubadilisha zaidi na zaidi ili uishi namna tofauti na jinsi ulivyoishi kabla hujaokoka. Watu wengi siku hizi hawahitaji maelezo zaidi kuhusu wokovu bali wanahitaji kuona kielelezo chenye kuonesha matokeo mazuri ya wokovu. Kama hatuwezi kuonesha maishani mwetu manufaa ya kuwa Mkristo wa kweli, basi maneno yetu hayatakuwa na maana kwa wengine. Yatupasa kumsogelea Bwana na kuongozwa naye ili wengine waone jinsi ushirika wetu na Bwana ulivyo mzuri.

Pamoja na hiyo, tujue hatuwezi kwenda mbele ya watu kama watu tuliokamilika kabisa. Bali, kazi yetu ni kuwaonesha kwamba tunayo nia ya kukua na kujifunza kwa Bwana. Maisha ya kikristo ni vita vya kiroho. Paulo alimwambia Timotheo, “Piga vita vile vizuri vya imani” (1 Timotheo 6:12). Lazima tuwe tayari kuvaa silaha zote za kiroho ili tuweze kushinda katika vita hivyo (Efeso 6:11-18). Tusiwe kama askari aliyeingia vitani bila kuvifahamu vita vyenyewe namna vilivyo wala hakuiandaa hata silaha moja; hakika huyu hataweza kushinda!

Nafikiri neno kubwa katika somo hili kuhusu maandalizi ya uinjilisti ni kujitoa kabisa kwa Bwana na kujitahidi kuimarika ndani yake ili Yeye aweze kufanya kazi yake ndani yetu na kupitia kwetu. Yote haya ni sawa na kusema tuyaangalie maisha yetu na mioyo yetu yawe kama apendavyo Yeye. Katika huduma hii tukijiendea hovyo hovyo tu, kamwe haiwezi kuleta mafanikio yo yote yale, bali tukiomba na kuutafuta hasa uongozi wa Mungu, Yeye ni mwaminifu hatakosa kuyatimiza mapenzi yake.

Kwa Utukufu wa Jina Lake

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *