Home 2020 September 07 Yesu Alikula na Wenye Dhambi

Yesu Alikula na Wenye Dhambi

Yesu Alikula na Wenye Dhambi

“Wafuasi” wa kisasa wa Yesu wanaona hii ni kama haki ya kuhusika kwao katika shughuli za kiulimwengu, kwa sababu Yesu alikuwa karibu sana na wenye dhambi pia, na hata kula nao.

Hili sio kosa la Bwana Yesu kwamba wafuasi wake wamemwelewa vibaya. Hatutaweza kumfuata Yesu leo, hata kama tungejaribu!

Hata hivyo, ni kweli kwamba kulikuwa na watenda dhambi wengi na watoza ushuru waliokuwa katika ushirika na Yesu wakati wa huduma yake hapa duniani (katika mwili).

Alilaumiwa kuwa yeye pia alikuwa ni mmoja wao wa hao mwenye dhambi kwa sababu walikuwa ni wengi waliokuwa wakiandamana naye.

Hata hivyo, Yesu hakuwa akijaribu kujihusisha na mambo yao ili akubalike nao (ili wampokee/wamfuate). Hakuwa akingojea ‘wakati mzuri’ wa kuanza kufanya nao mazungumzo juu ya mambo ya kiroho (kuwashuhudia mambo ya Mungu).

Yesu hakuwafuata wenye dhambi, bali wao walimfuata yeye.

“…watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata” (Marko 2:15)

Walimfuata kwa sababu walisikia mahubiri yake na waliona miujiza yake na hivyo walitaka kusikia zaidi:

“Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize” (Luka 15:1)

Hii inaonyesha tofauti kubwa kutoka njia ya huduma ya wale wanaoitwa “wafuasi” wa Yesu ambao wanatafuta baa, madanguro, na sehemu za michezo (kama vile mpira n.k.) ili tu kuwa karibu (kuwafuata mahali walipo) na wenye dhambi na kukubaliwa nao.

Wanahalalisha yote kwa kudai kuwa wanafanya huduma kama vile Yesu alivyokuwa akifanya katikati ya wenye dhambi, kwa kufanya kile wanachokifanya. Sio sawa …, mara mbili!

Yesu kamwe hakuhudumu hivyo, wala huduma yake kwa watu wa tohara (Wayahudi) sio mfano wetu wa huduma ya kanisa leo. Mfano wetu unapatikana katika nyaraka za mtume ambaye Bwana alimteuwa kwa ajili ya kanisa (Warumi 15: 8; 15:16).

“Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi” (Wafilipi 3:17)

Wakati ni kweli kulikuwa na watenda dhambi na watoza ushuru waliomzunguka Bwana wakati ule, yeye lakini hakuwa kimya juu ya dhambi zao ili kuwafanya wahisi kukubaliwa pia.

Alikuwa akitoa wito kwa wenye dhambi hao kutubu dhambi zao. Kama ‘tabibu’ alijaribu kurekebisha tatizo lao la dhambi.

“Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu” (Luka 5:32)

Kwa sababu hiyo, makahaba wengi na watoza ushuru waliomfuata walikuwa ndio waumini ambao walikuwa wametubu na walikuwa wakimfuata Bwana katika ufalme (Mathayo 21: 32-33).

Hii ni tofauti kabisa na huduma ya wafuasi wa kisasa wa Yesu ambao hawako tayari kumkosea mtu yeyote yule kwa kumwita mwenye dhambi au kuinyooshea kidole dhambi yake (hata kama ni mashoga).

Haya yote yanapaswa kukufanya ushangae na kujiuliza maswali mengi juu ya uaminifu wa wafuasi hao wa Yesu kama kweli wanamfuata Yesu kwa dhati.

Njia ya Bwana ya kufanya huduma katika kila kipindi/majira hairidhiani, haikubaliani wala haichukuliani kamwe na uovu, bali inaeneza injili.

Yesu alikula na wenye dhambi, na aliwahubiria wenye dhambi pia. Lakini Yesu hakujaribu kujichanganya nao, KAMWE.

Kwa Utukufu wa Jina Lake

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *