Home 2020 September 06 Tofauti Kati ya REHEMA na NEEMA

Tofauti Kati ya REHEMA na NEEMA

Tofauti Kati ya REHEMA na NEEMA

Rehema ni kitendo cha kuzuia adhabu inayostahili, wakati Neema ni kitendo cha kupewa kibali/kipawa kisichostahiliwa. Kwa sababu ya Rehema yake, Mungu hatupi adhabu inayostahili, yaani kututupa kuzimu; wakati kwa sababu ya Neema yake, Mungu hutupatia zawadi ambayo hatustahili, ambayo ni kutufanya wa mbinguni.

Rehema na Neema ni sifa kuu za upendo wa Mungu. Kiini cha Biblia ni upendo wa Mungu wa kuwapenda watu kupitia lensi ya Yesu Kristo. Matendo mawili makuu ya Mungu yameonyesha asili Yake yenye – nguvu, neema, na rehema: UUMBAJI na UKOMBOZI.

Wakati kazi ya Mungu ya uumbaji ilionyesha nguvu zake kuu, kazi ya Mungu ya ukombozi ilifunua upendo wake wa ajabu, ulioonyeshwa kupitia rehema na neema Yake. Upendo huu wa Mungu ni muhimu sana kwa uwepo wa maisha na wokovu wa wanadamu.

“Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma; Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.” (Zaburi 145: 8-9)

Neema na Rehema: Ufafanuzi na Tofauti

Neno la Kiyunani lililotafsiriwa ‘rehema’ mara nyingi ni neno eleos (lenye maana ya huruma) na ‘neema’ ni neno charis (neema). Rehema na Neema, zinaweza kutofautishwa kama ifuatavyo: Rehema ni kitendo cha kuzuia adhabu inayostahili, wakati Neema ni kitendo cha kupewa kibali/kipawa kisichostahiliwa. Kwa huruma yake, Mungu hatupi adhabu inayostahili, yaani kuzimu; wakati katika neema yake, Mungu hutupatia zawadi ambayo hatustahili, ambayo ni kutufanya wa mbinguni.

Rehema na Neema ni kama pande mbili za sarafu moja – na ‘sarafu’ hiyo ni UPENDO wa MUNGU. Rehema ni upendo wenye huruma kwa wanyonge, na Neema ni upendo wa ukarimu kwa wasiostahili. Wanadamu ni wadhaifu na hawafai – sisi sote tunahitaji REHEMA na NEEMA ya MUNGU. Rehema hutupeleka kwenye njia ya msamaha, wakati Neema inatuongoza kwenye upatanisho.

Mifano ya Rehema na Neema ya Mungu katika Biblia

Rehema na Neema mara nyingi hufikiriwa kimakosa kuwa ni dhana ya Agano Jipya pekee. Lakini kwa kweli, Rehema na Neema zimeonyeshwa katika Maandiko yote; katika Agano la Kale na Agano Jipya.

Biblia imejawa na habari za Mungu akiwatumia watu wasiostahili (wasio kamili) kutimiza kusudi Lake. Kuna mifano mingi ya Rehema na Neema ya Mungu katika Agano la Kale. Daudi labda ndiye anaweza kuwa mfano mashuhuri zaidi kuliko wote: aliitwa “mtu anayeupendeza moyo wa Mungu” (Matendo 13:22) licha ya dhambi zake nyingi zinazofahamika na kuandikwa kwenye Biblia. Daudi alikuwa na tamaa, aliua, na alifanya uasherati. Ibrahimu alikuwa mwoga na alisema uwongo, Sara hakuwa na subira, Yakobo alikuwa tapeli, Musa alikuwa mkaidi na mwenye mashaka, Rahabu alikuwa kahaba, na Waisraeli walimwasi Mungu mara nyingi – lakini Mungu bado aliwatumia wote kutimiza kusudi Lake, pamoja na mapungufu yao hayo.

Mungu alikuwa ni mwaminifu na ahadi zake hakushindwa kuzitimiza (Kutoka 34:6, Kumbukumbu la Torati 4:31, 7:9, Maombolezo 3:22-23, Hesabu 6:24-26).

Mifano zaidi ya Rehema na Neema za Mungu katika Agano Jipya:

– Sauli alikuwa mnyanyasaji na mtesaji wa Kanisa la Mungu, lakini Mungu alimgeuza kuwa Paulo, Mtume wa Kristo, mwandishi wa zaidi ya nusu ya Agano Jipya (14/27).

– Petro alikuwa mwenye tabia kali na alimkana Yesu mara 3, lakini Mungu alimtumia kuhubiri na takribani zaidi ya 3,000 waliokolewa kwa mahubiri kutoka kwenye kinywa chake.

– Thomaso alikuwa mtu mwenye mashaka, lakini Mungu alimtumia kuhubiri Injili huko India/Indonesia (kulingana na taarifa mbalimbali),

– Maria Magdalene aliteswa na mapepo, lakini Mungu kwa neema yake alimpa nafasi pekee ya kuwa shahidi wa kwanza kumwona Kristo aliyefufuka, nafasi ambayo hata Thenashara wa Yesu hawakuipata.

– Martha hakuwa na utulivu, lakini Mungu pia alimruhusu awe kati ya mashahidi wa kwanza wa ufufuo wa Kristo (pamoja na Lazaro, kaka yake).

– Baraba alikuwa mhalifu, lakini Mungu alimruhusu aachiliwe badala ya Yesu.

– Mwizi alisamehewa msalabani na kuahidiwa kuwa Paradiso na Yesu.

Kwa uwazi kabisa, Biblia imekuwa ni kumbukumbu ya Mungu ambaye amekuwa akiwasamehe mara kwa mara wanadamu wenye dhambi – na zaidi sana, imeonyesha Mungu mkamilifu anavyofanya kazi, ndani ya na kupitia kwao, vyombo vilivyovunjika, kwa faida yao wenyewe na mwishowe kwa utukufu wake yeye Mungu! Rehema na Neema ya Mungu ndivyo vitu pekee vinavyoweza kuwaokoa na kuwadumisha wanadamu (Tito 2:11, 3: 7, Waefeso 2: 4-9, Zaburi 103: 1-5, 8).

Ikiwa Mungu ameweza kuonyesha upendo wake kwa watu hapo zamani, ni lazima awe na uwezo wa kufanya hivyo katika maisha yetu leo. Kwa hiyo, tunalo jukumu la kuitikia upendo huo wa Mungu!

Kuitikia Rehema na Neema za Mungu

  1. Kutambua mahitaji yetu ya Rehema na Neema.

Kuikubali (kuikumbatia) Rehema na Neema ya Mungu, tunahitaji tuwe na unyenyekevu (Yakobo 4:6, Mika 6:8). Inatakiwa kwanza ni lazima tukubali kuwa wanadamu wote ni wenye dhambi, HAKUNA mtu awezaye kufikia kiwango cha ukamilifu anachokitaka Mungu (Warumi 3:23, 5:20), na ulimwengu huu tunaoishi umevunjika/umeharibika, kwa hiyo tusijishughulishe na kujihangaisha na mambo yetu sisi wenyewe na vitu vilivyomo katika ulimwengu huu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumebadilisha mwelekeo wetu kutoka katika uwezo wa kibinadamu na kuuelekea uweza wa Mungu kwa kutambua enzi yake juu ya vitu vyote.

Rehema na Neema hutukomboa kutoka kwenye kujiwazia ukamilifu wa kibinadamu, moyo wenye kiburi na uasi. Ni kwa Rehema na Neema yake Bwana tu, ndizo zinazotufanya tuweze kuishi leo.

  1. Kukubali Rehema na Neema za Mungu.

Kuna shauku kubwa katika ubinadamu la kutaka uhuru. Kwa kawaida, watu huwa wanakuwa na furaha sana pale wanapopokea kitu kizuri bure bila ya wao kutumia gharama yoyote ile (kwa mfano, ni nani asiyependa chakula cha bure?) na kinyume chake, watu hao hao wanaopenda vya bure, ni wagumu sana kwao kulipa gharama husika au kujitolea. Habari njema ni kwamba Mungu ametoa REHEMA na NEEMA Yake BURE, bila gharama yoyote. Mwana wa Mungu amefanya YOTE YALIYOHITAJIKA kwa niaba yetu kwa ajili ya wokovu wetu (Warumi 6:23, Waefeso 1:7). Tumeokolewa sio kwa sababu sisi ni WEMA SANA, lakini kwa sababu Mungu NDIYE MWEMA SANA. Yeye amelipa GHARAMA yote muhimu INAYOTAKIWA kwa ajili ya wokovu wetu kwetu.

Zaidi sana, kwa kuongezea, Mungu anajua kwamba sio tu tunapenda kitu cha bure, lakini pia tunapenda kitu kipya. Asante sana Mungu wetu, kupitia kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, tumepewa kitu kipya – maisha mapya, matakatifu (1 Petro 1: 3, 2 Timotheo 1: 8-9) na fursa kubwa ya kuishi kwa ajili yake (2 Wakorintho 5: 15). Kwa kadiri tunavyotembea katika njia zake, tutaendelea kupata neema na utukufu wake (Zaburi 84:11) na kupata msaada wakati wa uhitaji (Waebrania 4:16).

  1. Kujua Utambulisho Wetu Katika Kristo na Kuushirikisha Upendo Wake kwa Watu Wengine.

Tulikuwa kipindi fulani watoto wa ghadhabu kwa sababu ya dhambi zetu, lakini katika Kristo, sasa tumekuwa watoto wa Mungu (Yohana 1:12). Na kwa sababu tumekuwa watoto Wake, tunapaswa kushukuru kwamba Baba yetu amejaa neema na kweli (Yohana 1:14); ingawa hatupaswi kulichukulia pendo lake hilo kwetu kuwa rahisi (poa). Ni lazima tukue katika mahusiano yetu naye, tumjue na kumpenda zaidi.

Shauku yake ni kutuona na sisi tunawarehemu (tunawahurumia) na wengine (Hosea 6:6, Mathayo 9:13, 5:7, Luka 6:36). Kama vile Bwana alivyopanda mbegu ya upendo ndani ya mioyo yetu kwa neema yake ya kutosha, tunapaswa nasi kuzaa matunda zaidi katika kazi/huduma zetu (2 Wakorintho 9:8, 12:9).

Paulo alitambua vyema umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kwa Bwana kama mwitikio UNAOFAA kwa neema Yake, na sio kama juhudi ya kupata KIBALI chake (1 Wakorintho 15:10). Basi, sisi nasi, kama watu waliochaguliwa na wapendwa wa Mungu, tuendelee kufanya kazi njema aliyotupatia (Wakolosai 3:12), tuwe wenye rehema na neema katika kuwahukumu wengine (Yakobo 2:13), na tufanye mambo haya yote katika kweli na upendo (2 Yohana 1: 3).

Utukufu Una Yeye Milele Yote; AMINA

Author: Festus Patta

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *