Home 2020 February 12 Tunapaswa Kuibariki Israeli?

Tunapaswa Kuibariki Israeli?

Tunapaswa Kuibariki Israeli?

Katika Mwanzo 12:3 Mungu aliwapa mababa wa Israeli ahadi maalum kwamba wao watakuwa njia ya baraka ya Mungu na laana kwa ulimwengu:

“nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” (Mwanzo 12:3)

Kama mtu yeyote yule (ambaye hakuwa Mwisraeli) alitaka kubarikiwa alitakiwa kwanza kuibariki Israeli, na kama mtu yeyote hakufanya hivyo au angeilaani Israeli angewalaani. Israeli ilikuwa ni njia ya hukumu ya Mungu na baraka kuelekea duniani.

Watu, wafalme na mataifa walibarikiwa au walilaaniwa kulingana na jinsi walivyojisogeza au jishikamanisha na Israeli ambayo ndiyo mkondo wa baraka za Mungu: Wafikirie akina Abimeleki, Rahabu, Waedomu (Obadia), au yule akida mwaminifu ambaye alihitaji uponyaji katika huduma ya kidunia ya Yesu.

Yesu hakuwa ametumwa kwa Mataifa (Mathayo 15:24), lakini sikiliza jinsi huyu akida wa Mataifa alivyoelezwa kuwa baraka kwa Israeli:

“Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.” (Luka 7:4-5)

Mpaka leo bado tunapata barua za changizo za namna hii kutoka kwa “Wakristo-Wayahudi” kwa kuzingatia mstari huu!!!

Wakati ambapo wengi wanadai kuwa Biblia inaieleza Israeli kama njia ya baraka ya Mungu, hii inatokana na urahisi wa kudhani kwamba Mungu anafanya kitu kile kile wakati wote. Wakristo wengi waaminifu wanaendelea kuibariki Israeli kulingana na Mwanzo 12:3 katika kutafuta upendeleo wao ili waweze kuzipokea baraka za Mungu.

Hili limekuwa ni kosa kubwa na ni kushindwa kulitumia neno la Mungu kwa haki na kugawa neno la ukweli (2 Timotheo 2:15).

Baraka yetu leo ni kupitia Kristo sio Israeli

Tatizo la kujaribu kutii Mwanzo 12:3 ni kwamba juhudi hizo zinapuuza jinsi ya kupata utajiri wa neema ya Mungu kulingana na ufunuo wa siri ya Kristo. Kulingana na ufunuo wa siri hiyo, Israeli imeanguka na haina uhusiano mzuri wa kiroho na Mungu katika kipindi hiki (Warumi 11:11). Wanahesabiwa katika kutoamini, wote katika dhambi, kama watu wa Mataifa (Warumi 3:9; Warumi 11:32).

Katika Kanisa, Mwili wa Kristo, hakuna Myahudi wala Myunani (Mmataifa). Kuwa Mwisraeli hakumpi mtu huyo upendeleo wowote au uwezo wa kuwa karibu zaidi na Mungu au kupata baraka zake katika kipindi hiki (Wagalatia 3:28).

Paulo anaelezea katika Waefeso 2 kwamba Israeli ilikuwa ni njia ya upatikanaji wa baraka za Mungu kwa wakati uliopita, lakini sasa upatikanaji wa Baraka za Mungu kwetu, huja kwa kupitia mwili na damu ya Kristo.

“Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo” (Waefeso 2:13)

“Kwa maana kwa yeye [Kristo Yesu] sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja” (Waefeso 2:18)

Hata kama hakungekuwa na Mwisraeli hata mmoja katika Mwili wa Kristo, kila muumini bado angekuwa na baraka zote za kiroho katika Kristo (Waefeso 1:3). Mungu amebadilisha njia ya baraka zake kutoka kwa taifa la Israeli na kwenda kwa Mwili wa Kristo (Waefeso 3:1-6).

Atukuzwe Mungu kwa sababu kuna Wayahudi ambao wameokolewa kwa injili ya neema, lakini kuibariki Israeli kama taifa leo ni kupuuza mapenzi ya Mungu na hivyo kuwabariki watu wasiookoka kwa sababu tu ya mwili wao – kwa kuwa tu wao ni Waisraeli kwa kuzaliwa kimwili (Wagalatia 5:13; 6:15).

Laana Iliyohaidiwa

Njia ya Mungu ya kupitishia baraka zake imebadilika, lakini pia jinsi ya kushughulika na adhabu (laana) kumebadilishwa. Ahadi ya Mungu katika Mwanzo 12:3 inajumuisha si tu baraka bali pia na laana. Katika mstari huo wa Mwanzo 12:3, mtu yeyote atakayeshindwa kuibariki Israeli, mtu huyo atalaaniwa na Mungu. Kinyume na Mwanzo 12:3, Paulo anasema kwamba Kristo alituokoa kutokana na laana ya Sheria:

“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu…” (Wagalatia 3:13)

“ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo…” (Wagalatia 3:14)

Mwili wa Kristo hauwezi kuwekwa chini ya laana tena kwa sababu ya neema ya Mungu!!!

Kuweka laana kwa wale ambao hawakuibariki Israeli ni sawa na kumwita Kristo amelaaniwa na kuurejesha Mwili wa Kristo nyuma ya msalaba na kuuweka chini ya laana ambayo Kristo aliifia. Mwenyezi Mungu APISHE mbali; utukufu wetu haupo katika taifa la Israeli, bali katika msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kupitia kwake tumepokea kila baraka za rohoni na ukombozi kutoka kwenye kila laana.

Jinsi ya Kuibariki Israeli

Siri ya Kristo inaeleza jinsi baraka za Mungu zinavyoweza kuja juu ya mtu yeyote licha ya anguko la taifa la Israeli, na jinsi ambavyo laana inavyoweza kuondolewa kutoka kwa wenye dhambi ambao hawakustahili ukombozi kama huo. Siri hii imefunuliwa katika neema ya Kristo. Leo wanadamu wote wamepewa wokovu bure, sio kwa kupitia maagano, au taifa maalum, au sheria, bali ni kwa kupitia kazi iliyo kamilika ya Kristo (1 Timotheo 2:4).

Ingawa Israeli imeanguka, bado wanaweza kuokolewa. Katika siku zijazo, Israeli itarudi tena na kuwa taifa juu ya Mataifa katika ufalme wa Kristo duniani, lakini si leo (Warumi 11:26-28).

Kuibariki Israeli (au taifa jingine lolote lile) leo, ni kuwabariki kwa kuwapelekea injili ya Yesu Kristo. Wahimize kuweka imani yao katika Kristo Yesu kama njia pekee ya baraka zote za kiroho chini ya majira haya ya neema ya Mungu. Kwa bahati mbaya sana, kwa wengi wanaoshindwa kuuona ushirika wa ile siri, jambo hili linaonekana kama kosa la jinai. Kosa lililokuwepo katika siku za Paulo, na linaendelea leo:

“Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika” (Wagalatia 5:11)

“Bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu” (1 Wakorinto 1:23-24)

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *