Home 2020 February 11 Ukubwa wa Neema ya Mungu

Ukubwa wa Neema ya Mungu

Ukubwa wa Neema ya Mungu

Neema ya Mungu kwa wengi ni kile kinachoweza kuonekana kwa macho au kuelezeka kwa maneno; lakini neema ya Mungu kwa uhalisia wake ni kubwa sana na haiwezi kuelezeka kwa namna yo yote ile ya kibinadamu kwa sababu imezidi sana, inapita kiasi, ni kubwa mno; Wazungu wanaiita ‘hyper-grace’ (superabounding) na Wayunani wanaiita ‘huperperisseuo’! Hiki ndicho mitume, Yohana na Paulo, walikuwa wakikieleza na kukimaanisha pale walipokuwa wakizungumzia neema iliyorundikana na upendo wa Kristo unaopita ufahamu. Hiki ndicho pia Yesu alichokuwa akitueleza jinsi Mungu Baba alivyo mwingi wa neema na pendo kwa kutumia maneno, ‘je! Si zaidi sana?’

Neema ya Mungu iliyopindukia (iliyopitiliza) haiwezi kupunguzwa kwa kudharauliwa na kwa maneno ya kusemwa au mawazo ya kufikiriwa yanayolingana na uwezo wetu wa kufikiri. Neema ya Mungu ni kubwa sana! Njia pekee tunayoweza kuanza kuifahamu neema ya Mungu ni kwa kuona utukufu na ukuu wa Mungu ambao yeye ameufunua kwetu kupitia Mwana wake Yesu Kristo.

Tunaweza kujiuliza hapa kuwa, ni nini basi kinyume cha neema ya Mungu, iliyozidi sana? Na ni kwa nini ‘Wakristo’ wengi, kwa kujua au kutokujua, wamegeuka na kuwa wapinzani wakubwa kupindukia, tena waliopo mstari wa mbele kabisa kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo wakati wa Yesu, kuipinga neema hii ya Mungu iliyoachiliwa kwetu bure katika majira haya? Imenitokea, tena si mara moja, kupata upinzani mkali kutoka kwa watetezi wa sheria za Musa (cha kushangaza tu wanatokea Tanzania, ingekuwa wametokea Yerusalemu labda), ambao wanapinga vikali ujumbe wa neema ya Mungu na ‘kunikemea’ kwa sababu eti ‘naweka msisitizo mkubwa juu ya neema ya Mungu iliyozidi sana’. Hakika, nafanya hivyo! Ninacho sisitiza tena hapa ni kuwa neema ya Mungu ndiyo inayo tuokoa, na ndiyo inayo tutunza. “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Ni neema ya Mungu pekee, kuanzia mwanzo wa wokovu wetu mpaka mwisho wake. Lakini tatizo ni nini? Tatizo, inavyoonekana, ni sisi kutoihubiri sheria vyakutosha. Nilisoma makala moja sehemu fulani, mwandishi wa makala hiyo aliyaandika maneno haya: “Sheria sio inayotuokoa, lakini ndiyo inayotutakasa! Neema ya Mungu ndiyo ikusogezayo kwenye ufalme (akimaanisha kuokoka), lakini baada ya hapo, uwezo wako wa kuitii na kutunza Sheria ndio unaokudumisha hapo” Najua hakujua ni nini hasa alikuwa anakitenda, alikuwa kama ‘amekurupuka’ hivi.

Kwa sababu wapinzani wote wa Neema ya Mungu hawapendwi kuitwa ‘wanasheria’ (legalists), kwa sababu hiyo maneno ‘sheria’ nitayabadilisha na kuwa maneno ‘kazi’ ili kuukubali mtizamo wao ambao unasisitiza kwamba kuna vitu fulani ni lazima mtu avifanye ili aweze kuokolewa au  kutakaswa. Kutokana na hili, tunaweza kuzitambua injili za aina tatu (3) ambazo zinahubiriwa katikati yetu: Ya kwanza, ni injili isiyo na neema (graceless gospel); unaokolewa kwa matendo yako ya haki na unatakaswa kwa matendo hayo pia.  Ya pili, ni injili mchanganyiko (grace – law gospel); unaokolewa kwa neema lakini unatakaswa kwa matendo yako. Ya tatu, ni injili ya neema iliyozidi sana (hyper-grace gospel); unaokolewa kwa neema na unatakaswa kwa neema! Hii ya tatu ndiyo watu wa ‘dini’ hawataki hata kuisikia, kwa sababu unawaondolea ufarisayo wao, hawa ndio Yesu aliwafananisha na yule mtoto ‘mwaminifu’ aliyejidhania kuwa yeye sio mpotevu kama mdogo wake, kumbe ndiye alikuwa amepotoka zaidi kuliko yule aliyetapanya mali zake na makahaba (Luka 15:1-32).

Ni vyema ikifahamika, tena kwa herufi kubwa, kwamba hatuna injili isiyo na neema. Ni neema ya Mungu ndiyo inayoifanya injili iwe habari njema. Ukiondoa neema ya Mungu kwenye injili, injili haiwi tena habari njema, bali injili hugeuka na kuwa ni habari mbaya! Sio sahihi kabisa kusema kuwa ‘Neema ya Mungu’ ni kitu bora zaidi katika Ukristo, bali ‘Neema ya Mungu’ ni KITU PEKEE katika Ukristo; kwa sababu ‘Neema ya Mungu’ ni neno jingine linalomtambulisha Yesu.

Injili mchanganyiko ni ile injili inayoamini katika ‘bufe’ la neema ya Mungu na sheria ya Musa, vitu ambavyo, kama ilivyo kwa mafuta na maji, havichanganyiki kamwe. Kwenye sheria, neema haikai; na kwenye neema sheria haikai. Na maandiko yametuonya kutokuwatumikia mabwana wawili; huwezi kutekeleza sheria na ukawa chini ya neema kwa wakati mmoja, labda tu kama huelewi ni nini maana ya sheria na maana ya neema ya Mungu. Huwezi kuokolewa kwa neema na hiyo neema iliyokuokoa ikashindwa kukukamilisha (kukutakasa) hata uhitaji tena matendo yako ndiyo yakutakase. Hii inaitwa ‘neema kipande’, kwa sababu habari njema hapa ni nusu tu. Ya kwamba Yesu amekuokoa (hii ndio habari njema), lakini upande uliobakia unakutegemea wewe mwenyewe (hiyo ndiyo habari mbaya).

Neema ya Mungu ni Yesu pekee yake ametosha katika kila kitu, haitaji nyongeza wala kusaidiwa katika lile alilolitenda msalabani. Lilikamilika na Mungu alilipokea na kumkirimia jina lipitalo majina yote!

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *