Home 2020 February 11 Neema ya Mungu (i)

Neema ya Mungu (i)

Neema ya Mungu (i)

Pendo la Mungu ni kubwa sana kuliko vile tunavyoweza kufikiria. Ukuu wa pendo hilo umepita akili za kibinadamu zinavyoweza kutambua, kama vile zisivyoweza kuupima ukubwa wa ulimwengu ndivyo ambavyo ufahamu wa mwanadamu usivyoweza kulielezea pendo la Mungu lilivyo kubwa kwetu. Upendo wa Mungu hauna mipaka na wala hauwezi kuelezeka wala kufafanuliwa kwa akili za kawaida za kibinadamu; hizi za kutumia milango mitano ya fahamu!

Neema, ni jinsi Mungu anavyolidhihirisha pendo lake hilo kwetu. Neema ya Mungu ni ya ajabu na haiwezi kamwe kuelezeka kibinadamu; inajitosheleza na inapita kila aina ya ‘ndoto’ mwanadamu anayoweza kuwaza kuiota. Na hii, Neema ya Mungu, ndio kitu pekee kinachoifanya imani ya Kikristo kuwa ya kipekee, ya namna yake; tofauti kabisa na imani zingine zote. Ndiyo kusema, Ukristo unatenganishwa na imani zingine zote duniani kwa sababu hiyo moja tu, uwepo wa NEEMA YA MUNGU; na wala sio kuacha dhambi, maombi, kutubu, au kuisha maisha ya utauwa, kwa sababu haya yote yanapatikana kwenye imani hizo zingine zote, kwa namna tofauti tofauti.

Neema ni upendeleo wa kipekee kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu Baba mwenyewe kwetu kwa sababu ya upendo na wema wake. Neema ni kitendo cha Mungu ‘kutuzawadia’ yeye mwenyewe (Yeye Mungu kujitoa mwenyewe kwetu) bila sababu yo yote ile zaidi ya kwamba ilimpendeza yeye mwenyewe kufanya hivyo. Je! Unahitaji ushahidi kudhibitisha hilo? Angalia msalabani ambako Kristo Yesu alikufa kwa sababu ya wasio na haki, wenye dhambi; wewe na mimi: “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu” (Warumi 5:6) tena walipokuwa wangalipo katika kutenda dhambi zao: “Bali Mungu aonyesha pendo lake mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8).  Kristo kamwe hakufa kwa ajili ya wenye haki, watakatifu ambao hawakuwahi kumkosea Mungu, wale ambao walikuwa kileleni, watu wakuu, wasiokuwa na doa wakiwa juu ya ngazi. Kristo alikufa kwa ajili ya watu wanyonge na waliopotea na masikini na wahitaji.

Kristo Yesu aliutoa uhai wake pale msalabani kwa wale wote waliokuwa wakiuhitaji huo uhai. Kwa wale waaminifu vya kutosha ambao wanaweza kusema, “Nisaidie mimi Bwana, Sina namna nyingine ya kujisaidia mwenyewe”, na Mungu anajibu kwa kusema, “Mimi ndio msaada wako mkuu.” Hiyo ndiyo neema! Neema sio fundisho (doctrine) bali ni Mtu na Jina lake ni Yesu Kristo. Neema sio moja ya baraka za Mungu bali ni jumla ya baraka zote zilizofungwa pamoja katika (ndani ya) Kristo. Neema ni zawadi ya zawadi zote kutoka kwa Mtoaji wa watoaji wote. Neema, kama ilivyo kwa hewa ya ‘oxygen’, hatuwezi kuishi bila yenyewe na kwa hakika ye yote aliyeikosa hana uhai mbele za Mungu. Ni neema ya Mungu ndiyo iliyotuleta hapo tulipo na neema hiyo hiyo ndiyo itakayotufikisha kule tuendako, katika Kristo.

Maandishi haya ni juhudi zangu za kumwambia kila mtu juu ya habari hii njema ya neema ya Mungu. Nakuandikia ili uweze kujua kwamba Mungu anakupenda vile ulivyo kwa sababu yeye ni Baba yako; haijalishi umefanya nini au umetenda mabaya kiasi gani, Baba yako wa mbinguni hakuhesabii hukumu kwa lolote lile, ikiwa tu umeamua kugeuka na kumwangalia Yeye. Anatamani akukumbatie na kukubusu na akutunze na kuwa na wewe milele yote (Luka 15:11-24).

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *