Home 2020 February 10 Onyo la Siku za Mwisho

Onyo la Siku za Mwisho

Onyo la Siku za Mwisho

ONYO LA SIKU ZA MWISHO

 Mwili wa Kristo (Kanisa) wakati huu unapitia changamoto nyingi hasa kwa kukosa mafundisho ya msingi yanayo ujenga mwili huo juu ya mwamba ambao hautabomolewa na nguvu yoyote ile, Mathayo 7:24-27:

“Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, lakini haikuanguka kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

Badala yake, watu wa Mungu wamegeukia mafundisho yanayomtukuza shetani kwa maana sehemu kubwa, kama si yote, katika Ibada zao, kumhubiri yeye na jinsi alivyowakandamiza watu na sio kutumia muda huo mwingi  katika kuyafunua mamlaka tuliyonayo katika Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa Yeye ndiye ukamilifu, utimilifu na utoshelevu wa Imani yetu.

Roho wa Mungu aonya waziwazi juu ya nyakati hizi za mwisho, kwamba watu wataicha Imani na kufundisha mafundisho ya mashetani (seducing spirits and doctrines of devils), 1 Timetheo 4:1:Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.”

Imani yetu ni kuwafundisha waamini juu ya maana ya kazi ya Yesu Kristo Msalabani kwa ajili yetu na sio vinginevyo. Kwamba Yesu Kristo alikufa, alizikwa na alifufuka siku ya tatu kwa ajili ya uokovu wetu na kuhesabiwa haki kwetu kwa ufufuko wake, (1 Wakorintho 15:1-4). Mfano wa mafundisho ya mashetani ni yale ambayo yanalinganisha nguvu za Mungu na za mapepo, kwamba yanajenga ulinganifu wa nguvu za madhabahu mbili, yaani Madhabahu wa Mungu aliye hai na zile madhabahu za kipepo na kichawi. Mafundisho ya namna hii ni yale yanayojenga hoja kwamba kwakuwa mtu alipeleka ‘kuku’ kwa mganga wa kienyeji, basi itampasa mtu huyo kuleta sadaka kama hiyo kwenye madhabau ya Mungu aliye hai ili akombolewa. Kwamba sadaka kama hizo zinalenga ‘kuisaidia’ sadaka ya ukombozi wa wanadamu aliyoifanya Yesu pale Msalabani, kwakuwa ‘haitoshi’ kuwakomboa watu hao mpaka waje na sadaka ya ukombozi…!

“Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu. Wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo. Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. Wakijifunza sikuzote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli. Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili.” (2 Timetheo 3:1-9)

“Nao kwa kuwa walikataa kumkubali Mungu, Yeye akawaacha wafuate akili zao za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.” (Warumi 1:28-32)

Nia ya Mungu wetu kutuokoa ni kwa kila anayeamini kuufikia ujuzi wa kweli na kutembea katika hiyo kweli bila kuchukuliwa na upepo wa mafundisho yanayowatoa watu kwenye mamlaka na uwezo wa Jina la Yesu Kristo kama ilivyonenwa kwenye Wafilipi 2:9-11. Kwa sababu hiyo, Mungu wetu anamtaka kila mmoja wetu anayeamini, afikie kuijua kweli. “Jambo hili ni jema tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani, mwanadamu Kristo Yesu, aliyejitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wanadamu wote, jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake.” 1 Timotheo 2:3-6.

Maagizo ya Mungu ni haya, “Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja Kwake na ufalme Wake kwamba: Uhubiri Neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima, badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.” (2 Timotheo 4:1-5)

Mungu hakutupa maagizo tu, bali alitupa maagizo na hayo maagizo yalikuwa na ujumbe, ambao ulikuwa ni AMRI, kwamba ndio ujumbe pekee wa kuhubiri. “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamwua kwa kumtundika msalabani. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyetiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina Lake.” (Matendo 10:39-43)

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *