Kuanguka Kutoka Kwenye Neema
Wagalatia 5:4
“Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema”
Je, ni nini hasa kinamaanishwa inaposemwa kuanguka kutoka katika hali ya neema, hasa kama kifungu hiki kilivyotumika katika Wagalatia 5:4? Tafsiri sahihi ya aya hiyo ina matokeo (athari) muhimu kwa Mkristo.
Baadhi ya Tafsiri Zisizokuwa Sahihi
Kwa bahati mbaya sana Wagalatia 5:4 imeeleweka vibaya na baadhi ya watu (wengi). Moja ya tafsiri mbaya ni kudhani kwamba kifungu hicho kinaelezea juu ya kitendo cha mtu asiyeamini kuikataa Injili ya Kristo. Ingawa ni wazi kwamba Mtume Paulo alikuwa anawaandikia Wakristo wa Galatia katika waraka huu. Katika muktadha wa karibu, anatangaza kwamba wameweka huru na Kristo (5:1) na anawaita “ndugu zake” (5:11). Biblia inaposema kuwa, “ninyi mtakao kuhesabiwa haki,” haina maana ya watu wasioamini ambao wanajaribu kuokolewa, bali inadhibitisha kwamba chini ya sheria mtu anachoweza kufanya zaidi ni “kujaribu kuhesabiwa haki”, kwa sababu mwisho wa yote “hakuna mtu awezaye kuhesabiwa haki kwa sheria” (3:11). Tafsiri nyingine isiyojitosheleza ni kwamba Paulo alikuwa akiwaandikia waumini ambao walikuwa wamepoteza wokovu wao (eternal salvation). Sio kana kwamba tu hii ni kinyume dhidi ya mafundisho yote ya kimaandiko kuhusu usalama wa wokovu (security of salvation), bali pia ni uelewa m-baya wa dhana ya neema kuhusiano na wokovu pamoja na hoja hasa ambayo Paulo anaiwakilisha katika Wagalatia. Ufuatao hapa chini, ni ufafanuzi mfupi wa aya hiyo katika muktadha wake!
Mwendelezo wa Muktadha
Muktadha unaonyesha kwamba Paulo anaichukulia hali ya wasomaji wake (Wagalatia) kuwa wameokoka kutoka mwanzo wa waraka wake huo (1:2-4) na zaidi sana anawakumbusha kwamba waliitwa “katika neema ya Kristo” (1:6). Dhana ya neema ipo katikati ya tafsiri sahihi kwa Wagalatia, na ipo katikati pia ya Wagalatia kushindwa kuelewa uhusiano waliokuwa nao na Mungu wao. Kimsingi Wagalatia hawa hawakuelewa matokeo yote ya wokovu wao walioupata kwa neema na walichanganywa kirahisi na walimu wa uongo (1:6-9; 3:1; 4:17; 5:7,12). Paulo anafanya juhudi ya kuwazuia waumini walioko Galatia kuacha kuweka imani yao katika sheria za Agano la kale kama njia ya wao kupata utakaso. Hiyo ilikuwa ni kinyume na kanuni ya wokovu kwa neema na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Paulo amkosoe Petro kwa sababu hakwenda sawasawa na kanuni hiyo ya wokovu kwa neema (2:11-14) na kuhusu hilo Paulo alisema ” Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure” (2:21). Tangu Wagalatia walianza maisha yao ya Kikristo “katika Roho” haikuwapasa tena kufikiri kwamba wangeweza kukua na kufikia ukomavu kwa juhudi zao za ‘kimwili’ katika kuishika (kuitunza) sheria (3:2-3). Sheria huleta laana (3:10). Kama waumini ambao wamekuwa waadilifu kwa njia ya imani, Wagalatia sasa ni “wana wa Mungu” (3:26) na sio tena watumwa wa sheria (4:5-7). Wanahitaji “kusimama imara” katika uhuru wao huo na wasinaswe tena chini ya kongwa la utumwa wa sheria (5:1). Kama wao wameamua kuirudia sheria, Kristo hatawafaidia kitu chochote katika utakaso (5:2), kwa sababu kutunza kwao kwa mahitaji ya ‘nje’ ya sheria kwa juhudi za kimwili kamwe kusingeweza ‘kumsogeza’ mtu yeyote karibu na Mungu. Ili waweze kukubalika na Mungu, kupitia juhudi zao hizo, iliwapasa kuzishika sheria zote kikamilifu – yaani, kuitimiza torati yote (5:3), jambo ambalo wasingeweza kulifanya.
Tafsiri ya mstari 4
Katika mstari wa 4, Paulo anafafanua kwamba waumini wanaoirejelea sheria wamefarakanishwa (wametengwa) na Kristo. Neno “kufarakanishwa” limetafsiriwa kutoka neno la Kiyunani katargeo, ambalo lina maana ya kutengwa au kuachanishwa kutoka kwenye kitu kilichokuwa kimeshikamana nacho, au kukiondolea kitu fulani ufanisi wake, au kukifanya kitu hicho kisiweze kufanya kazi, au kukiondolea nguvu yake, n.k. Wasomaji wa waraka wake huo, walikuwa wamefarakana katika uhusiano wao na Kristo (na sio kukatwa katika nafasi yao kama Wakristo) kwa kuwa neema yake isingeweza kufanya kazi kwao kama wao wanarudi nyuma na kuwa chini ya sheria tena, hicho ndicho tohara ilikuwa ikidhihirisha (5:2). Wao walikuwa katika Kristo, lakini walikuwa hawaishi katika nguvu ya neema yake. “Kitenzi” kutafsiriwa “kuanguka” ni neno ekpipto ambalo lina maana zaidi ya moja, lakini kwa kawaida lina maana ya kuanguka kutoka kwenye kitu fulani au kupoteza kushikilia kitu ulichokuwa umekishika. Wagalatia walikuwa wamepoteza kuishikilia neema, sio Kristo, wala wokovu, na au kuhesabiwa haki. Muumini hawezi ‘kuvuliwa’ tena haki aliyopewa bure kwa neema kwa imani (Warumi 8:30), ingawa muumini anaweza kuishi katika utata akipingana na kanuni ya Mungu ya wokovu na utakaso kwa neema.
“Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza” (Warumi 8:30)
Katikati ya kiini cha hoja ya Paulo ni tofauti kati ya neema na sheria. Neema na Sheria zipo kinyume (zimepeana migongo) na KAMWE haziwezi kuchanganya – hazichangamani; inaposimama neema, sheria haisogei na inaposimama sheria, neema haisogei – kila moja ya haya mambo mawili ni ya kipekee (mutually exclusive). Mtu anatakiwa achague kimoja, ama awe na imani katika neema ya Kristo katika kupata haki, au katika sheria. Kuambatana na mfumo mmoja, kunaikataa mfumo mwingine, kwa sababu mifumo hiyo ‘haipikiki’ kwenye chungu kimoja! Ni kwa kupitia tu njia ya imani katika ‘utoaji’ wa Mungu katika yote mawili, kinafasi (positional) (3:24) na haki ya vitendo (practical righteousness) (5:5) ndivyo yanavyopatikana, na sio kwa njia ya kazi ya sheria. Kwa hiyo, kwa kifungu hiki ” kuanguka na kutoka katika hali ya neema ” Paulo hashughuliki na “nafasi” ya Wagalatia katika Kristo; bali Paulo anashughulika na jinsi wanavyotembea katika Ukristo wao (yaani mtembeo wao wa neema). Nafasi ya Mkristo ni hakika: kila mwamini anasimama katika neema (angalia Warumi 5:2) kama mtoto wa Mungu (3:26) aliyewekwa huru kutoka kwenye utumwa wa sheria (5:1). Lakini Wakristo wanaweza kuhatarisha nafasi yao kwa kufuata njia isiyolingana kwa kujaribu kutimiza masharti ya sheria au mfumo mwingine wa nje katika juhudi zao wenyewe.
Matumizi
Sisi Wakristo tukiwa tunaishi katika utiifu na unyenyekevu wa nje kwa misingi ya sheria yoyote au mifumo ya dini, hatuwezi kukuza kiroho chetu, zaidi sana tunakishusha kwenda chini. Utii kama huo wa sheria na mifumo ya dini hakuwezi kutufanya tuwe karibu na Mungu, zaidi sana hujenga ‘pengo au ufa’ katika uhusiano wetu na Mungu. Tunaanguka kutoka kwenye neema, kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa tunakuwa “tumeanguka nje” ya Mungu, kwa sababu tunakuwa tumeidharau zawadi yake ya neema aliyotupa bure – neema hiyo hiyo ndiyo ambayo imetuokoa – kwa sababu ya kutumainia mafanikio yetu au uwezo wetu sisi wenyewe! Roho hii ya kushika/kupenda sheria huenda mbali zaidi ya kufuata au kushikamana tu na sheria ya Agano la Kale. Kwa mfano, kama tunaabudu ili kuwapendeza wengine, hatuwezi “kumpendeza” Mungu. Ikiwa tuna ibada za kila siku ili tu tukidhi ratiba zetu, hatuwezi “kumridhisha” Mungu. Kama tunaamini katika huduma zetu za kutoa dhabihu ili kupata upendeleo wa Mungu, basi tunapuuzia zawadi ya dhabihu ya Mungu kwetu. Maisha katika Roho pekee chini ya neema ya Mungu ndiyo yanaweza kuleta uzima wa haki ambao Mungu anataka.
Kwa Utukufu Wake Kristo
Leave a Reply