Siri Iliyofichwa Tangu Zamani
SIRI ILIYOFICHWA TANGU ZAMANI
Biblia inatumbia kwamba siri ya Mungu ni Yesu Kristo: “ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo” (Wakolosai 2:2-3)
SIRI, katika maana ya Agano Jipya, (ukiligawa sawasawa, yaani kulitumia kwa halali neno la Mungu – 2 Timotheo 2:15), ni jambo ambalo kwa wakati fulani lilifichwa lisifahamike kwa watu wa Mungu lakini sasa limefunuliwa lifahamike kwao. Yesu aliwahi kuongelea juu ya siri ya ufalme wa Mungu (Marko 4:11) na ambao kwa wakati ule alikuwa akiufunua kwa wanafunzi wake. Mtume Paulo, amelitumia neno hilo ‘siri’ mara 21 kwenye nyaraka zake kuonyesha umuhimu wa neno hilo kwa wale aliowakusudia, ambao kwa sehemu kubwa ilikuwa ni watu wa mataifa ambao yeye alitumwa kwao (Matendo 26:16-18). Kila wakati lilipotumika, neno hilo ‘siri’
lilibeba maana nzito katika ufunuo mpana wa kiroho ambao Mungu alipenda kuufunua kupitia Roho Mtakatifu na kuwajulisha wateule wake yale yaliyofichwa kwa watu wengine hasa katika kizazi kilichopita. “Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho” (Waefeso 3:15).
Siri ya kusudi la Mungu ni ile aliyokusudia katika Yesu Kristo tangu kabla ya kuwekwa kwa misingi ya dunia kwamba ije kutekelezwa wakati wa utimilifu wa wakati ambao Yeye Mungu aliukusudia – “akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na Uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo;” (Waefeso 1:9-10; 1 Wakorintho 2:7).
Siri ya Mungu ni utimilifu wa mpango wake wa ukombozi kwa mwanadamu (myahudi na myunani) katika kuuleta ukamilifu wa mpango huo wa uokovu kupitia Yesu Kristo kufikia utimilifu wake. Mpango wake huo ulishatabiliwa mara nyingi zamani hizo, lakini ni kwa namna gani na ni wakati gani wa utimilifu wake na ninani atayeutimiza haukuwa wazi, ulifichika, haukueleweka mpaka wakati wake Yesu kristo. Ni katika Yesu tu Mungu amejizihirisha kwa watu wote, kama Yesu mwenyewe alivyosema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba”, (Yohana 14:9).
Mtume Paulo alisema kwamba yeye amepewa jukumu la kuwa mhudumu wa kulihubiri ‘neno la Mungu’ ili lifikie utimilifu wake, hiyo ikiwa ni siri iliyofichwa kwa vizazi karne na karne, lakini wakati huu imefunuliwa kwa wateule wake ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yetu, tumaini la utukufu (Wakolosai 1:25-27). Kwamba, kupitia nyaraka za mitume, tumepewa ukulele wa maandiko na ambayo yote yanatuelekeza tumwangalie Kristo peke yake – kuonyesha ufunuo wa mwisho wa Neno la Mungu kwa watu wote.
Hakuna namna bora ya kumwelewa Mungu nje ya kuwa na uhusiano wa kipekee na mtoto wa pendo lake. (Wakolosai 1:13; Mathayo 12:50; Yohana 14:23; 2 Yohana 1:6). KRISTO ni ile SIRI iliyofunuliwa kwao wote waaminio kwamba Yeye ndani yao waaminio ndio tumaini lao la utukufu (Wakolosai 1:27). Wapate pia kujua Ufunguo wa kupata utajiri wote wa kufahamu kwa hakika na kupata kujua kabisa siri ya Mungu, yaani KRISTO, ni kuzaliwa upya (mara ya pili) kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ambaye huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu (1 Wakorintho 2:10)
Mtume Paulo anatuambia kwamba bila shaka, siri ya utauwa ni kuu. Anaendelea kusema, Yeye Mungu (Kristo) alidhirishwa katika mwili, akajulikana kuwa na haki katika roho, akaonekana na malaika, akahubiriwa katika mataifa, akaonekana katika ulimwengu, akachukuliwa juu katika utukufu (1Ttimotheo 3:16).
Maandiko matakatifu, kupitia Mtume Paulo, yanatuonyesha moyo wa Injili na siri ya utauwa. Siri ya kuwa mtauwa ilikuwa imefichwa lakini sasa imefunuliwa kwa wateule wake. Hawa ni wale wanaomwamini mwana wa Mungu na kazi yake kamilifu ya kumkomboa mwanadamu kupitia kifo chake, kuzikwa na kufufuka hao ndio siri hii imefunuliwa kwao.
Mungu amelifunua Neno lake kwa watakatifu wake (Wakolosai 1:26) ambao wamesikia na kjifunza Habari Njema (Yohana 6:45; Warumi 10:17; John 3:16-18), na ni wao tu ndio wanaoweza kufahamu maana ya ufunuo ule uliofichwa kwenye ile siri. Katika maana halisi, siri ya Mungu, ni mpango wa ukombozi kwa wanadamu kwa njia ya Kristo. Hatungeweza kuelewe njia sahihi ya ukombozi wetu mpaka pale tu Yesu alipokuja, kifo chake na hatimaye ufufuko wake.
Leave a Reply