Home 2023 April 19 KIKOMO KWA MUNGU ASIYE NA UKOMO

KIKOMO KWA MUNGU ASIYE NA UKOMO

KIKOMO KWA MUNGU ASIYE NA UKOMO

Ni mara ngapi umesikia kuhusu hilo? Je! Umewahi kumwambia mtu kwamba Mungu hawapi tena wanadamu uwezo wa ‘kunena kwa lugha’ au ‘kuponya wagonjwa’, na ukajibiwa kwamba: “Unamwekea Mungu mipaka? Mungu anaweza kufanya chochote anachotaka!” Kama huna uhakika wa jinsi ya kujibu hoja kama hii, hapa kuna ‘hoja-mbinu’ inayoweza kukupatia msaada na ambayo ni muhimu:

Mungu anajiwekea mipaka mwenyewe; Amejiwekea mipaka kwa namna mbalimbali. Kwanza, Mungu amejiwekea mipaka kutokana na utakatifu Wake. Mungu anaweza kufanya chochote anachotaka, lakini hawezi kutenda dhambi (rejea Tito 1:2). Haki ya asili yake takatifu inamzuia kufanya jambo lolote ambalo hata udhalimu wake unaonekana kuwa ni mdogo mno. Ndio kusema; Mungu wetu asiye na mipaka, anayo mipaka inayotokana na asili yake takatifu.

Lakini pia Mungu wetu amejiwekea mipaka kwa Neno Lake. Ingawa Mungu anaweza kufanya chochote anachotaka, lakini hawezi kuugharikisha ulimwengu tena kwa sababu ameshatamka ‘Neno Lake’ kwamba hatafanya hivyo tena. Unakumbuka ahadi aliyompa Nuhu?

Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi.” (Mwanzo 9:11)

Baada ya miaka takribani elfu tatu kupita, bila mafuriko ya ziada duniani kote, Mungu alilinganisha uaminifu wake huo na ahadi yake hiyo kwa uaminifu wake kwa Israeli:

“Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea. Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye” (Isaya 54:9-10)

Wale wote wanaofundisha kwamba Mungu alinawa mikono yake kwa Israeli baada ya taifa hilo kumuua Mwanawe, na kwamba Israeli hawatawahi kuwa na uhusiano wowote Naye tena, na Mungu amezipokonya ahadi zake zote alizowapa na kutupa sisi Mataifa, wana hatia ya kumshtaki Mungu kwa kuvunja nadhiri yake hiyo nzito (Tazama Isaya 49:15; Yeremia 31:35-37). Mungu anaweza kufanya chochote anachotaka, lakini hawezi kuwaacha Israeli, kwa kuwa ametoa Neno Lake kwamba hataliacha taifa hilo, na siku moja watakuwa watu wake tena (Hosea 1:9-11 linganisha na Warumi 9:25-26).

Na Mungu pia, hawezi kumpa mtu ye yote karama za kiroho, kama vile unabii na lugha, baada ya kuweka nadhiri kwamba karama hizi “zingekoma” na “kutoweka” katika kipindi hiki cha wakati Biblia itakapokamilika (1 Wakorintho 13:8-10). Kwa hivyo usiruhusu mtu yeyote akuambie kwamba unamwekea Mungu mipaka wakati unaposisitiza kwamba karama hizi, ambazo kwa njia dhahiri hazipo katika kipindi hiki cha wakati, zimetoweka. Kwa kusema hivyo, tunakiri kwa urahisi kikomo cha ugawaji ambacho Mungu amejiwekea!

UTUKUFU UNA YEYE MUNGU MILELE NA MILELE AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *