Home 2022 April 02 Uaminifu Kwa Utume Wetu

Uaminifu Kwa Utume Wetu

Uaminifu Kwa Utume Wetu

Katika siku za Paulo, ‘kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri’ kulikabiliwa na upinzani mkali kila upande. Kwa sababu ya kutangaza kwake kwa uaminifu ujumbe huo mtukufu ambao ulikuwa umekabidhiwa kama amana kwake; Paulo, mara kwa mara, aliingia katika lawama na kupata dhiki nyingi.

Katika mojawapo ya nyaraka zake za awali, tayari tunapata kuijua orodha ndefu ya hatari na mateso ambayo Paulo wakati huo alikuwa ameitwa kuyastahimili (2 Wakorintho 11:23-33) na upinzani huu, uchungu na kutokuchoka, kuliendelea katika huduma yake yote.

Katika barua yake ya mwisho, iliyoandikwa kutoka gerezani huko Rumi, Paulo anahimiza uangalifu kwenye tabia bainifu ya ujumbe wake, na akaongeza kusema:

“Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote. Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.” (2 Timotheo 2:7-10)

Mateso haya ya karibu mara kwa mara ambayo mtume huyu wa neema alitiishwa, kwa kawaida yalikuwa na matokeo yake juu ya roho zenye woga. Wengine, walioona ukweli na utukufu wa ujumbe wake, lakini walikosa ujasiri wa kusimama pamoja naye katika kuutangaza. Wengine, ambao walianza naye pamoja walijaribiwa pia – na wengine walikengeuka – wakarudi nyuma.

Aliposimama kwa mara ya kwanza mbele ya Nero, Mtume Paulo alilazimika kusema haya:

“Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.” (2 Timotheo 4:16)

Kutokana na haya yote, si ajabu kuwa Paulo analazimika kumwandikia kijana wake Timotheo maneno haya:

“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu” (2 Timotheo 1:7-8)

Wala si ajabu pia kwamba katika 2 Timotheo 2:1-3 mtume analazimika tena kumhimiza mwanawe huyo katika imani “awe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu” na “ashiriki taabu pamoja naye, kama askari mwema wa Yesu Kristo,” hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye mwenyewe alihitaji msaada wa mara kwa mara katika suala hili.

Mkristo wa kawaida anaweza kudhani ni vigumu kufikiria kwamba Paulo alihitaji maombi ili kumpa ujasiri; lakini kinyume na hilo, Paulo anafunga waraka wake wa Waefeso kwa ombi hili:

“Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.” (Waefeso 6:18-20)

Je! Ingekuwaje, kama watu wote waliokuja kuuona utukufu wa injili ya neema ya Mungu wangeomba ombi hili la ujasiri?

Wengine wanaweza kudhani pia kwamba inahitaji ujasiri mdogo tu leo hii kutangaza neema ya Mungu katika usafi/ukamilifu wake wote. Wanahoji; Ni nani anayeteswa leo, hasa katika nchi zetu hizi zenye uhuru, zilizo na nuru, kwa ajili ya kuhubiri neema ya Mungu? Huko ni kujidanganya!

Shetani hakuwa mtendaji dhaifu katika upinzani wake kwa ile kweli wakati Konstantino alipoliinua lile lililojiita Kanisa kuwa maarufu kuliko wakati watangulizi wake walipolitesa Kanisa hilo na kuwapeleka washiriki wake magerezani na wengine kuwahukumu vifo kwa moto na upanga.

Hakika, shetani bila shaka, alifanikiwa zaidi katika siku za Konstantino kuliko alivyokuwa wakati mateso yalipopamba moto. Na je, mwamini yeyote wa Neno la Mungu anadhani kwamba Shetani amejitoa katika upinzani wake kwa kweli ya Mungu leo, kwa sababu tu wanadamu, angalau wako katika nchi huru, hawachomwi moto au kutupwa kwenye matunda ya simba? Umepotoshwa!

Uadui wa Shetani dhidi ya Mungu na Neno Lake unaendelea vile vile bila kupungua. Kuchukia kwake “injili ya neema ya Mungu,” ni kuchungu sana, na upinzani wake juu yake upo kama ulivyoamuliwa, kama ilivyo wakati wote. Lakini anajua vyema kwamba kuvunjika moyo daima kunakohusiana na kuwa miongoni mwa wachache, mara nyingi kunafanikiwa kuwanyamazisha wale ambao wangesimama imara dhidi ya manyanyaso ya kimwili.

Hebu, sisi tunaoijua na kuipenda kweli ya Neno la Mungu, tuamue kwa neema ya Mungu kwamba hakuna kitu chochote kitakachotufanya tusiwe waaminifu kwa utume wetu huu mtukufu; kwamba, kwa gharama yoyote ile, tutawatangazia wengine kwa uaminifu na kwa ujasiri injili isiyoghoshiwa ya neema ya Mungu, nayo ni “kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri.” (Warumi 16:25)!

Utukufu na Wema na Uweza Vina Yeye Milele Yote; AMINA.

Author: Festus Patta

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *