Home 2021 June 13 Yesu Alimtuma Paulo

Yesu Alimtuma Paulo

Yesu Alimtuma Paulo

Katika salamu za utangulizi katika nyaraka zake zote, ni wazi kwamba Paulo alikuwa ni mtume au mtumishi wa Yesu Kristo.

Ni jambo lisiloepukika, licha ya uhusiano huu wa kitumishi kwa Yesu, pale tunapolinganisha ujumbe wa Paulo au Petro (Wagalatia 2:8-9), au pale tunapoyatafakari yale mtume huyu wa Yesu Kristo anayoyasema (2 Timotheo 2:7), au pale tunapoikuza ofisi yake kama mtume ya Yesu Kristo kwetu (Warumi 11:13), majibu ‘yenye hasira’ ya wasikilizaji wetu siku zote yamekuwa, sisi ‘tunamtukuza sana Paulo’.

Wanasema, “Tunapaswa kumtukuza Yesu sio Paulo.”

Paulo Anamtukuza Bwana Yesu

Je! Hawajui kuwa kati ya waandishi wote wa maandiko, Paulo anajisifu zaidi katika Yesu Kristo kuliko wengine wote?

“Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu” (Wagalatia 6:14)

Hii ni kwa sababu yeye Paulo alijua zaidi juu ya habari za Yesu Kristo kuliko hao wengine wote! Kujua kwake huko hakukutokana na kipaji chake cha kiakili bali ni kwa sababu ya habari ya siri iliyofunuliwa kwake na Bwana mwenyewe:

“Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo” (Wagalatia 1:11-12)

“Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele” (Warumi 16:25)

Ilikuwa ni fursa kwake “kutimiza neno la Mungu” kupitia ujumbe ambao hakuna mtu mwingine kabla yake alikuwa akiujua:

“Ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake” (Wakolosai 1:25-26)

Yesu Kristo ndiye aliyemfanya Paulo kuwa mtume na mfano wa wokovu kwetu sisi ambao “tutaamini baadaye”:

“Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele” (1 Timotheo 1:16)

Mtume Paulo kamwe hajiinui juu ya Yesu Kristo bali anamsujudia na kumwita mkuu (mtangulizi katika yote):

“Kwa hiyo nampigia Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo magoti” (Waefeso 3:14)

“Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote” (Wakolosai 1:18)

Kufuata kielelezo cha Paulo na maagizo kunahitaji kumtukuza Mungu kwa Yesu Kristo:

“Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina” (Warumi 16:27)

“Na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Wafilipi 2:11)

Maneno Matatu Mwanana

Madai kwamba “tunamtukuza Paulo” ni hoja ya kawaida ambayo inapaswa kutarajiwa na watetezi wote wa ujumbe wa neema ya Mungu. Hoja hiyo itatumika wakati wa majadiliano ya kifundisho, hasa pale inapotokea mtu wa upande mwingine wa mjadala huo hajui jinsi ya kukabili mafundisho. Wanahisi kutishiwa na hivyo kukimbilia kupata faraja katika maneno yaliyotamkwa na Yesu mwenyewe au kumhusu yeye hasa katika zile injili nne.

Kile ambacho hawakielewi ni kwamba Yesu hakuandika kwa mkono wake injili hizo nne. Mungu, kupitia Roho Mtakatifu, aliongoza maneno hayo yaandikwe kwa maana ile ile kama ambayo Musa aliandika na Paulo pia. Wanachotaka kusema ni kuwa “wao wanamfuata Yesu kupitia yale yaliyoandikwa katika Mathayo, Marko, Luka, na Yohana na sio kupitia yale Paulo aliyoyaandika.”

Wamefikia mwisho wa akili zao na wamechanganyikiwa. Kutokana na kuchanganyikiwa kwao huko, wanatarajia tuombe radhi kwa kudhani kwao kwamba hatumfuati Yesu. Kamwe haturudi nyuma; na wala hatubishani na mwanadamu yeyote. Bali badala yake, na kwa roho ya kuwafundisha tunawaambia maneno haya matatu tu, huku tukiwaachia wao kufikiria juu ya maneno hayo:

Wanaposema, “WAO WANAMFUATA YESU”,

Nasi tunawajibu kwa utulivu, “YESU ALIMTUMA PAULO”!

“Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo 9:15)

“Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia” (Matendo 22.14-15)

“Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi” (Matendo 26:15-18)

Kuna watu, ambao Mtume Petro aliwaita kuwa ni WAHALIFU kwa sababu ya kuyapotoa maandiko, wanadhani kwamba maandiko hayo katika Kitabu cha Matendo ya Mitume “yamechakachuliwa” kwa sababu tu mwandishi wake, Tabibu Luka, alikuwa ni mmoja wa washirika wa karibu wa Mtume Paulo na kwa hiyo yanakosa uhalali wa kuwa maandiko yenye uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Lakini, kinyume na uhalifu wao huo, tunao uthibitisho wa kutosha kutoka kwa Mtume, wao wanaomwamini zaidi, juu ya utume wa Paulo na ni vyema sana kwao wakiheshimu WOSIA wake:

“Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu” (2 Petro 3:15-17)

Kwa Utukufu Wake Yesu Kristo

Author: Festus Patta

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *