Paulo, Mtangulizi wa Wenye Dhambi!
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. “Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele” (1 Tim 1:15-16)
Maelezo ya Msingi
Roho Mtakatifu, mara nyingi, alikuwa na makusudi katika Maandiko ambayo yalizidi uelewa wa mwandishi. Andrea Fernandez aliunda neno sensus plenior au – maana kamili – kuelezea ukweli huu. Sensus plenior inahusu maana ya ndani zaidi, iliyokusudiwa na Mungu lakini haikuwa wazi (haikukusudiwa au haikueleweka) na mwandishi wa ‘kibinadamu’ ambayo inaonekana katika maneno ya Maandiko wakati yanaposomwa.
Kwa mfano, waandishi wa Agano la Kale mara nyingi hawakugundua kwamba walikuwa wakizungumza juu ya Yesu Kristo wakati walipoandika Maandiko. Mifano ya ukweli huu iko mingi katika Biblia:
Hosea 11:1
“Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”
Bila shaka, Hosea aliamini kwamba alikuwa akiandika juu ya taifa la Israeli katika maandishi haya. Mathayo, hata hivyo, alitafsiri kifungu hiki kuwa na maana inayohusiana na Yesu Kristo!
Mathayo 2:13-15
“Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu”
Ndio maana tunasoma maneno katika maandiko ya Paulo:
“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu (is given by inspiration of God –theopneustos ), lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” (2 Timotheo 3:16-17)
Kwa hiyo, kila lililoandikwa katika Biblia lina kibali cha Mungu katika kutufundisha, kutuonya, kutuongoza na kutuadibisha katika haki!
Sasa na turejee andiko letu la msingi:
Mtume wa neema alijiita “mkuu wa wenye dhambi” au “wa kwanza wa wenye dhambi” (1 Tim 1:15-16), na tangu wakati huo Wakristo wamechanganyikiwa juu ya utambulisho wao. Wanasema mambo kama “mimi ni mwenye dhambi aliyeokolewa kwa neema” ingawa Biblia inasema kuwa wao ni watakatifu (Waefeso 1:1, Wafilipi 1:1).
Kwa hiyo, wewe ni nani?
Mtakatifu, mwenye dhambi, au ni mchanganyiko wa vyote viwili?
“Angalia tabia yangu ilivyoharibika. Mimi si mkamilifu. Kwa kweli mimi bado ni mwenye dhambi.”
Hiyo sio kweli! Biblia inatangaza kwamba katika Kristo wewe ni kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17). Wewe sio mtu ‘aliyeboreshwa’, bali ni mtu wa aina mpya kabisa, ambaye hukuwahi kuwa kabla.
“Lakini ikiwa nitajiita mtakatifu, hiyo itakuwa inanijaza kiburi ambacho kitanizuia kupata neema ile ninayohitaji.”
Mungu huwapa neema wanyenyekevu, sio wasiokuwa waaminifu. Unyenyekevu wa kweli unatokana na kukubaliana na Mungu na kile anachosema juu yako, na anakuita wewe kuwa ni mtoto wake mpendwa. Katika Kristo, wewe ni mtu asiye na dhambi tena.
Kwa nini basi Paulo alijiita kuwa ni mkuu wa wenye dhambi?
Hapa kuna kifungu katika muktadha:
“Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.” (1 Timotheo 1:12-16)
Je! Mtume Paulo alikuwa mtakatifu aliyechanganyikiwa? Je! Alijiona kama ni mwenye dhambi? Hapana kabisa! Ama hakika, anaweka mstari tenganishi kati ya utambulisho wake wa sasa na wa zamani.
Zamani za Paulo:
- Nilikuwa mtukanaji (mstari 13)
- Nilikuwa mnyanyasaji (mstari 13)
- Nilikuwa mtu mwenye mjeuri (mstari 13)
Sasa ya Paulo:
- Yesu aliniwezesha (au kunipa nguvu) (mstari 12)
- Yesu alinihesabu kuwa mwaminifu (mstari 12)
- Yesu aliniweka katika huduma (mstari 12)
Paulo alikuwa mtenda dhambi mbaya lakini kitu cha kushangaza kilimtokea:
- Nilipata rehema (mstari 13)
- neema ya Bwana wetu ilimwagwa juu yangu tele (mstari 13)
- iliambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu (mstari 14)
Ni dhahiri kulikuwa na mabadiliko makubwa katika maisha ya Paulo. Kwa nini basi anajitaja kama mtenda dhambi mkuu? Amefanya hivyo ili wewe uweze kutiwa moyo.
Kwanini nilionyeshwa rehema na neema? Kwa sababu Kristo alitaka kunifanya mfano, mimi niliyekuwa mbaya zaidi, ili ujue kwamba uvumilivu wake na fadhili zake ni kubwa kuliko ubaya wako. (Maneno yangu ya kifungu cha 15-16)
Paulo anasema kitu hicho hicho kimoja hapa ambacho anakisema katika Warumi 5:20; ambapo anasema kuwa dhambi inapozidi, neema ya Mungu inakuwa nyingi zaidi. Neema yake ni kubwa kuliko dhambi zako. Bora yake, ni bora zaidi kuliko mbaya yako.
Neema ni Kubwa Kuliko Dhambi
Mtu aliyevaa lensi ya utambuzi wa dhambi ataisoma aya ya 15 katika upekee wake na kuhitimisha kuwa Paulo alikuwa ni mtambuzi wa dhambi. Lakini mtu aliyevaa lensi ya neema atasoma muktadha wa kifungu chote na kuelewa kwamba Paulo alikuwa hajisifii juu ya ubaya wake wa zamani bali juu ya wema wa Mungu.
Je, Unaona? Ikiwa Mungu anaweza kuachilia neema yake nyingi juu ya mtu huyu ambaye alikuwa ndiye wa ‘kwanza wa wakosefu’, basi Mungu anaweza pia kuimiminia hiyo neema yake, juu yako. Wewe amini tu!
Unaweza kusema, “Sina hakika, sijashawishika! Kwa sababu Paulo alisema ‘mimi ndiye (wakati uliopo) mkuu wa wenye dhambi,’ na sio mimi nilikuwa (wakati uliopita).”
Usiogope kuutumia ubongo wako vyema. Mara tu Paulo alipozaliwa mara ya pili hakuwa tena mwenye dhambi mbaya kupita wote katika Dola ya Kirumi. Mara baada ya kukutana na Yesu aliacha kuwatukana na kuwatesa Wakristo. Mabadiliko yake yalikuwa ni makubwa sana!
“Sasa je, ni kwa nini anasema ‘mimi ndiye mtenda dhambi mkuu’?”
Kwa sababu hiyo hiyo Muhammad Ali alisema “mimi ndiye bondia mkubwa zaidi wa wakati wote!” Ukweli ni kwamba, Muhammad Ali sio bondia mkubwa zaidi leo, lakini aliwahi kuwa na ameshikilia taji hilo. Kama ungepata wasaa wa kumuuliza, “Ni nani bondia mkubwa kuliko wote,” hangesema, “nilikuwa” bali “mimi ndiye!”
Ni sawa na Paulo!
Anaposema, “mimi ndiye mkuu wa wenye dhambi,” anazungumzia jina baya alilopata kama mtukanaji na mtesaji mkuu wa Wakristo. Yeye, kwa hiyo hasemi, “bado nakufuru na kuwatesa Wakristo.”
Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele. (1 Timotheo 1:16)
Paulo anaandika kukutia moyo. Ikiwa umekata tamaa baada ya kusoma haya – ikiwa unaamini bado wewe ni mwenye dhambi licha ya neema kubwa ya Mungu kwako – umeukosa moyo wake! Umekizingatia zaidi kile ulichokifanya kuliko jambo kubwa zaidi ambalo Mungu amelifanya. Unahitaji kutubu, kumwamini yeye, na kuyapokea maisha yake ya utele.
Mara tu Paulo alipokuwa Mkristo, aliacha kuwa mkuu wa wenye dhambi. Ndivyo ilivyokuwa kwako! Haijalishi umefanya nini, mara tu ulipoingizwa ndani ya Kristo ukawa ni mwenye haki na mtakatifu kama yeye (1 Yohana 4:17):
“Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.”
Yote haya ni kwa ajili ya utukufu wa neema yake na upendo!
Leave a Reply