Tunaweza Kupoteza Wokovu Tulioupata kwa Neema?
Ili tuweze kupoteza kitu chochote kile kutoka kwenye himaya yetu, ni lazima kwanza tuwe na jukumu la kukitunza! Vinginevyo, sio sisi tuliyekipoteza, bali ni mtu mwingine aliyekuwa na jukumu la kukitunza ndiye aliyekipoteza. Ni lazima tuwe makini sana tunaposoma maandiko matakatifu ili tuweze kujua na kutofautisha juu ya nini kilichoandikwa na kwa nani kimeandikwa. Tusikisome kwenye mstari wa Biblia kitu ambacho hakipo, wala hakikutegemewa kwenye mstari huo, na ni lazima tutafsiri kila mstari kutokana na muktadha halisi uliokusudiwa. Hii ndiyo sababu inayofanya, kuigawa kweli ya neno la Mungu sawasawa, kuwa na msaada mkubwa katika kulielewa kusudi la umilele la Mungu Baba.
Kuhusiana na wokovu wetu kwenye majira haya ya uachilio wa neema ya Mungu, tunaona kwa uwazi kabisa kwamba tumepokea kupitia kwa Mtume Paulo habari njema ya ‘wokovu kwa neema’. Kitabu cha Warumi ni kitabu bora kabisa kinachotuwezesha kuelewa maana ya ‘wokovu kwa neema’ katika majira haya. Tunajifunza katika Warumi 1-3 kwamba watu wote ni waovu mno na hakuna hata mmoja mwenye haki mbele za Mungu. Katika ukweli huo, Mtume Paulo anawaita ni watu waliokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, wenye dhambi, waovu, watenda mabaya na ni watu wanaostahili ghadhabu ya Mungu. Kila mmoja wetu, Myahudi au Mmataifa, amevunja sheria ya Mungu ya haki na anayo hatia mbele za Mungu mwenye haki ambaye ndiye atakayezihukumu kazi zetu katika maisha haya kama ni njema au ni za uovu.
Ni kwa kutumia utambuzi wa ufahamu wa wanadamu na sheria ya Mungu, Mtume Paulo anatanabaisha kwamba kila mmoja wetu hafai mbele za Mungu na hawezi kupata haki ya Mungu kupitia juhudi zake mwenyewe. Anahitimisha katika Warumi 3:10-12 kwa kusema maneno haya, “kama ilivyoandikwa, ya kwamba Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.” (Ni vyema sana ukiyatafakari maneno hayo kwa kina, maana hizo ‘Hakuna’ zote zimeanza na ‘H’ kubwa, ikisisitiza kwamba ni HAKUNA HATA MMOJA MWENYE HAKI MBELE ZA MUNGU. Najua kuna watu wanajihesabia haki zao wenyewe, hawayaamini maneno hayo kwa sababu wao wana haki walizojiwekea wenyewe, na ndio maana watu hawa kamwe hawawezi kuielewa NEEMA YA MUNGU!)
Kwa sababu Mungu anadai haki kamili (perfect righteousness) kwa ajili ya wokovu na uzima wa milele, sisi sote tumehukumiwa kifo na makazi yetu ni kuzimu kwa sababu ya makosa yetu. Lakini, pamoja na ukweli huo, Mtume Paulo alipewa ufunuo maalumu kutoka kwa Mungu ambao una ukweli mkubwa zaidi kuliko huo, ambapo sasa tunaweza kupata haki kamili na wokovu nje ya sheria (bila sheria).
“Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii” (Warumi 3:21). Zaidi sana, kusudi la sheria, au kazi ya sheria haikuwa ni kwa ajili ya kuokoa watu, bali ilikuwa na kusudi la kuwaonyesha watu kwamba wao ni wakosaji na walikuwa na hatia mbele za Mungu: “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria” (Warumi 3:19-20).
Na hapa ndipo watu wengi wanapokosea na kushindwa kulielewa kusudi la sheria kwa wenye dhambi. Sheria siku zote, mpaka leo, ina kazi moja tu, nayo ni kuleta ufahamu wa dhambi! Yaani, kama sheria isingesema ‘usizini’, kuzini kusingekuwa dhambi! “Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani” (Warumi 7:7). Kumbe, haki ya Mungu inapatikana tu kupitia imani kwa Kristo Yesu. Leo hii, tumepewa haki bure kwa neema yake kupitia ukombozi uliomo katika Kristo Yesu!
“ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hamna tofauti; Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu” (Warumi 3:22; 26).
Kutambua ni kwa namna gani tulipata wokovu wetu ni muhimu sana ili mtu aweze kuelewa kama tunaweza kuupoteza wokovu huu tulioupata bure kwa neema kwa imani ya Kristo Yesu. Mtume Paulo kwa uwazi kabisa anatufundisha kuwa wokovu wetu ni kwa imani katika haki iliyo ya Yesu Kristo ambaye alifanyika awe mbadala wetu kwa ajili ya dhambi, kifo na hukumu: “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorinto 5:21). Kwa kuwa Yeye ndiye aliyetulipia deni letu, na kwamba tumeweka matumaini yetu kwake Kristo, Mungu kwa neema yake, ametutangaza sisi ni wenye haki wake na kutupatia wokovu, “Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu” (Waefeso 1:13).
Leave a Reply