Home 2020 August 16 Kujitahidi Kutunza Wokovu

Kujitahidi Kutunza Wokovu

Kujitahidi Kutunza Wokovu

Sababu iliyomfanya Mungu amtume duniani mwanae wa pekee Yesu Kristo aje afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, ilikuwa ni kwa sababu tulikuwa hatuwezi kuishi maisha ambayo yangetuwezesha kutupatia haki ya Mungu kwayo. Kwanini sasa, tunadhani kwamba, baada ya kupata huo wokovu tunaweza kuisha maisha, NJE YA KRISTO, yatakayo tupatia haki mbele ya hukumu ya Mungu? Mtume Paulo amewahi kulizungumzia jambo hili, ili kuwaonya watakatifu wasitoke kwenye ile neema ya Mungu iliyowaokoa pale mwanzo, kwa kutafuta namna nyingine ya kutunza wokovu wao wenyewe.

Anachowaambia Mtume Paulo ni kwamba, kama ilivyokuwa kwa jinsi walivyookolewa, vivyo hivyo ndivyo, wokovu wao utatunzwa! Kama waliokolewa kwa neema, mbona sasa wanataka kuutimiza wokovu huo wao wenyewe?: “Je, Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?” (Wagalatia 3:3). Hakutaka wasiijue maana ya neema, wasije wakatengwa na Kristo: “Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema” (Wagalatia 5:4).

Baada ya kuipokea neema ya Mungu na kupata wokovu, Wagalatia hawa waligeuka nyuma na kuitafuta sheria ya Musa ili waweze kumpendeza Mungu kwa kuyatimiza yale yote sheria ilivyoagiza, ikiwa ni pamoja na kutahiri magovi yao. Wakasahau kwamba walipata wokovu huo bila ya wao kutimiza sheria, sasa wakatamani kuitimiza sheria ili wokovu wao huo uthibitike! Mtume Paulo aliwaonya kuwa kwa kufanya hivyo walikuwa ‘wametengwa na Kristo’, walikuwa ‘wameanguka’ na kutoka katika hali ya neema. Ilikuwa ni hasara KUBWA kwao kwa kutaka kwao kuutunza wokovu wao wenyewe kwa njia ya sheria. Jambo hili sio dogo, ni kubwa sana, hata kwenye Kanisa la Kristo la leo.

Mtume Paulo mara kwa mara, tena kwa msisitizo, amerudia kusema kwamba sio kwa sababu ya matendo yetu ya haki ndiyo yaliyotupatia wokovu huu tulionao. Na kama tulikombolewa kwa sababu ya hayo matendo yetu ya haki, basi Kristo alikufa BURE…! Anasema hivi: “Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure” (Wagalatia 2:21). Ndiyo kusema, kwa sababu hatukuokolewa kutokana na matendo yetu ya haki mbele za Mungu, haupo uwezekano wa kuupoteza wokovu wetu kwa sababu ya kukosekana kwa matendo hayo ya haki kwetu.

Kwa sababu tumeokolewa kwa neema ya Mungu, mwenye jukumu la kufanya matendo ya haki yanayohitajika kwa ajili ya wokovu wetu, ni Yesu Kristo pekee na ufaafu (efficacy) wa kifo chake pale msalabani. Imani yetu peke yake isingekuwa na maana kwa ajili ya wokovu kama Mungu asingeweza kukitimiza kile alichokihaidi (Warumi 4:21). Msingi mzima wa wokovu wetu ni imani katika malipo kamili ya Kristo kwa ajili ya dhambi zetu (Waefeso 2:8; Warumi 3:22).

Kwa hiyo, kama tumeokolewa kwa neema na baada ya kuokolewa huko tunajiona tena tunaweza kuipoteza ile hali yetu ya kukubalika, eti ni kwa sababu tu hatukuitafuta haki; kimsingi tunaukataa msalaba, na kukipuuza kile Kristo alichokuja kukifanya! Zaidi sana, kunaikataa hali yetu ya sasa katika Kristo, katika miili yetu iliyosulibiwa.

Kama vile Mtume Paulo alivyowaambia Wagalatia, ‘Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria’, utakuwa na mafanikio yanayofanana kwa kujaribu kujiokoa mwenyewe bila ya msalaba wa Kristo kama ilivyo kwa kujaribu kuutunza wokovu wako bila ya neema ya Mungu kufanya kazi kwa niaba yako. Suala la nini kinatokea katika wokovu ni muhimu sana kulijua, lakini limefunikwa na wingu kubwa na nguvu za giza za ulimwengu huu, ili watakatifu wasijijue wao ni akina nani na wamepata nini kwa kuikubali ile zawadi ya wokovu Mungu aliyowapatia bure kwa neema yake, na hivyo kuwafanya wahangaike kukitafuta kile ambacho wanacho tayari.

Kuelewa kile ambacho Kristo alikifanya msalabani kwa ajili yetu ni muhimu sana na ni ufunguo kwa ajili ya uzima wa milele. Bila neema ya Mungu, hakuna mwanadamu ambaye angekuwa na majibu mbele ya Mungu katika ile siku ya hukumu, na kwa hiyo, sehemu yetu ingekuwa ni kwenye ziwa la moto wa milele, SISI SOTE! Usibweteke, kaa ukijua hivyo, kwamba umeokolewa kwa neema ya Mungu tu, na KAMWE sio kwa matendo yako na unao uthibitisho kupitia damu ya Kristo.

“Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu” (2 Wakorinto 1:20-22)

“Nami niliaminilo ni hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6)

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *