Home 2020 August 16 Kristo kwa Jinsi ya Mwili

Kristo kwa Jinsi ya Mwili

Kristo kwa Jinsi ya Mwili

Je, umewahi kujiuliza kama ingekuwaje kama ungetokea kuishi katika Israeli wakati ule Yesu naye alikuwa akiishi huko?

Kila mwaka, maelfu ya watalii kutoka kote ulimwenguni husafiri kwenda Israeli kutembea katika yale maeneo ambayo Yesu alitembea, kuona maeneo mbalimbali ya kihistoria katika Biblia, kuona maji ambayo Yesu alitembea juu yake, na kupita kwenye ile njia Yesu aliyopita kuelekea Kalvari.

Pengine unaweza ukawa unashangaa, hivi Yesu huyo alikuwa anafananaje katika mwili, au haiba yake ilikuwaje hasa wakati ule anatoa yale mahubiri yake pale mlimani. Kuna mambo mengi yameandikwa juu yake na waandishi mbalimbali, kuanzia utoto wake mpaka mwisho wa maisha yake msalabani, hata kwa yale ambayo Biblia haikuona vyema kuyatunza ili yawe kumbukumbu ya kudumu hasa katika utoto wake.

Kile tunachokijua kuhusu maisha ya Yesu na huduma yake hapa duniani, ni kusudi lililopo kwenye vile vitabu vinne vinavyoitwa Injili, yaani: Mathayo, Marko, Luka na Yohana. Vitabu hivi vinne, vinavyohusu maisha ya Yesu katika mwili, ndimo Wakristo wengi sana wanamotumia muda wao mwingi kuhubiri, kufundisha na kujifunza kuhusu Yeye.

Hata hivyo, Mungu si alikuja katika mwili na kukaa katikati yetu ndio ujumbe mkubwa kabisa katika Ukristo? Vizuri, si hasa! Ingawa imekubaliwa na wengi, lakini sio sahihi!

Kumjua Kristo Kwa Jinsi ya Mwili

Ujumbe mkubwa kabisa kwa Ukristo SIO maisha ya Yesu na huduma yake kwa jinsi ya mwili, BALI ni kile alichokifanya na kufunuliwa kwetu baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Nikualike hapa usome kile ambacho Mtume Paulo anakisema juu ya kumjua Yesu katika mwili:

“Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena” (2 Wakorinto 5:16).

Kumjua Kristo kwa jinsi ya mwili kunatokana na yale tunayojifunza kutokana na habari zilizoandikwa kwenye zile Injili nne; yaani, Mathayo, Marko, Luka na Yohana. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yohana 1:14). Kutungwa na kuzaliwa Kwake katika mwili kumeelezwa.

Kumjua Kristo katika huduma yake ya hapa duniani ni kumjua yeye kama Mwana wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu, Mwana wa Mariamu, na Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili. Ni kujua kwamba yeye alikula chakula, alilala usingizi, alilia, alitembea, aliishi, na alikufa. Alitahiriwa; alitunza na kufundisha sheria; aliheshimu siku takatifu, n.k. Katika mwili alikuwa ni Myahudi, na huduma yake katika mwili ilikuwa ni kwa ajili ya kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Mtume Paulo anasema hivi kuhusu huduma ya Kristo katika mwili:

“Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa mababa zetu” (Warumi 15:8).

na Yesu mwenyewe alisema hivi:

“… sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” (Mathayo 15:24).

Ilikuwa ni katika zile Injili nne ambamo ndo tunamwona Yesu akifanyika mfano wa mwili wa dhambi (Warumi 8:3), aliteseka katika mwili (1 Petro 4:1), na akifa katika mwili (1 Petro 3:18).

Je, bado unayakumbuka yale maneno aliyoyaandika Mtume Paulo? Ngoja nikukumbushe tena, alisema hivi:

“Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena” (2 Wakorinto 5:16).

Tambua jambo hili hapa, ya kwamba wakati Mtume Paulo anasema maneno hayo, huduma ya Yesu hapa duniani katika mwili ilikuwa imekamilika. Yale matukio yaliyoainishwa katika zile Injili nne, Mathayo, Marko, Luka na Yohana, yote yalikuwa yameshakwisha kutokea, yamekamilika.  Swali ni hili, Sasa je, kama hatumjui tena Kristo kwa jinsi ya mwili, sasa tutamjuaje?

Kumjua Kristo Kuanzia Sasa na Kuendelea…!

Kristo mfufuka aliifunua kwa Paulo njia mpya ya kumjua yeye na huduma yake, ambayo haikuwa kwa jinsi ya mwili. Paulo aliita njia hiyo kuwa ni SIRI YA KRISTO (Wakolosai 4:3), ambayo inahusu injili ya Kristo kwa watu wote (Warumi 1:16), Mwili wa Kristo (Kanisa) katika ulimwengu wa roho (Waefeso 3:4-12), na tumaini la utukufu wa milele kwa neema ya Mungu iliyotolewa bure kwa watu wote (Wakolosai 1:25-28).

Kanisa (Mwili wa Kristo) ni kiumbe kipya, ambacho hakikuwahi kuwepo mpaka pale Kristo alipoondoka katika mwili na kuwa katika ulimwengu wa roho:

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” (2 Wakorinto 5:17).

Badala ya kumjua Kristo katika mwili kama Masihi wa Kiyahudi aliyetabiriwa na manabii mbalimbali tangu mwanzo wa dunia, sisi hatumjui hivyo tena, bali tunamjua Yeye kuwa ndiye mwanzilishi wa viumbe vipya (Wakolosai 1:18, Ufunuo 1:5) ambavyo sasa vimeketishwa pamoja naye katika ulimwengu wa roho (Waefeso 2:6) uliyositirika tangu zamani za milele (Warumi 16:25).

Hatumjui Yeye tena kuwa ni Myahudi aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili (Warumi 1:3), kwa sababu katika Kristo hapana Myahudi wala Myunani (Wagalatia 3:28). Hatumjui tena Yeye kuwa ni Mfalme wa Wayahudi, bali tunamjua Yeye kuwa ni Kichwa cha Kanisa, aliyewekwa juu ya vitu vyote!

“juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa  vyote katika vyote” (Waefeso 1:21-23).

Kumjua Kristo kwa namna hii sio kwa jinsi ya kimwili, bali kama Bwana mfufuka na Mkombozi ambaye ameiachilia neema yake kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi ulimwenguni kote kupitia imani katika msalaba Wake.

Habari hii ya neema na siri ya Kristo ni habari kubwa kupita zote katika Ukristo na hazipatikani kwenye vile vitabu vinne vya Injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) ambavyo humdhihirisha Kristo katika mwili. Hii ni habari ya kipekee inayopatikana kupitia kwa Mtume Paulo peke yake kama ilivyofunuliwa kwake na Kristo mwenyewe baada ya kukamilika kwa huduma yake katika mwili; baada ya kufa, kuzikwa na kufufuka kwake:

“Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo” (Wagalatia 1:11-12).

“Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishia hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami” (1 Wakorinto 15:1-10).

Kuyatafuta maisha ya Yesu kwa jinsi ya mwili kama mtoto, kijana, n.k., au nini alikifanya katika huduma yake katika mwili kwa wale waliotahiriwa, kutaleta tu uelewa dhaifu kumhusu Yesu katika ulimwengu wa roho, aliko sasa. Kumjua Kristo, kama vile anavyotakiwa kujulikana sasa ni kumjua Yeye kama vile anavyotaka ajulikane: sawasawa na injili ya Paulo na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele!

“Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile iliyositirika tangu zamani za milele” (Warumi 16:25).

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *