Home 2020 February 10 Injili Ipi?

Injili Ipi?

Injili Ipi?

INJILI IPI?

Biblia inapambanua Injili za aina mbalimbali ambayo waumini wengi wameshindwa kuzitofautisha na hivyo kuwafanya washindwe kuelewa maana halisi ya Injili na ni Injili gani hasa wanatakiwa kuifuata hasa kipindi hiki cha neema ya Bwana iliyoachiliwa kwetu bure kwa kumwamini Bwana Yesu tu kuwa Bwana na Mwokozi wetu.

Injili maana yake ni habari njema. Lakini swali linafuatia ni kwamba habari ipi ni habari njema kwa mfuasi wa Yesu Kristo? Kama hilo halitoshi, swali jingine ni kwamba, je kuna Injili (Habari Njema) zaidi ya moja? Na je kama jibu ni sio, Je, Habari Njema ya Ufalme (Mathayo 4:23), Injili ya Yesu Kristo (Marko 1:1), Habari Njema ya Mungu (Marko 1:14), Injili ya waliotahiriwa na wasiotahiriwa (Wagalatia 2:7), Habari Njema ya Uokovu wetu (Waefeso 1:13), Habari Njema ya Neema ya Mungu (Matendo 20:24), Injili ya Milele (Ufunuo 14:6), n.k., zote hizo ni sawa sawa?

Roho wa Mungu kupitia andiko la Paulo katika Kitabu cha Wagalatia 1:6-9, analalamika wazi kwamba kuna Injili (Habari Njema) zaidi ya moja na kwamba yeyote anayeihubiri hiyo Habari Njema kinyume na yeye Paulo alivyoihubiri na alaaniwe, tena alaaniwe milele…

‘Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo Yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata injili nyingine, ambayo kwa kweli si injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi huyo mtu na alaaniwe! Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu ye yote atawahubiria injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

Ni vyema kujiuliza hapa kwamba, ni Habari Njema gani Paulo alikuwa akiihubiri? Maandiko yamefafanua kwa namna nyingi ujumbe wa Paulo kwa Mwili wa Kristo, kama ifuatavyo:

1 Wakorintho 15:1-4

Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyo wahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili. Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemayo Maandiko, ya kuwa alizikwa na alifufuka siku ya tatu,

1 Timetheo 1:16

‘Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakao mwamini baadae, wapate uzima wa milele.’

 Matendo 20:24

‘Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ni kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.’

 1 Wakorintho 1:23

lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kikwaza na kwa Wayunani ni upuzi.’

Paulo, katika maandiko yaliyotajwa, anajipambanua kwamba yeye ndiye alikuwa wa KWANZA kupewa na Bwana Yesu, wajibu wa kuihubiri Injili ya Neema ya Mungu, ambayo inashuhudia kazi ya Msalaba ya Bwana Yesu (Mateso, Kufa, Kuzikwa na Kufufuka) kuwa ndiyo suluhisho pekee la dhambi ya mwanadamu na kwamba yeyote anayetaka kuokolewa na dhambi, inampasa kuangalia utimilifu, ukamilifu, utoshelevu na ukuu wa damu ya Yesu iliyomwagwa pale Msalabani kwa ajili ya dhambi ya ulimwengu.

Itizamwapo Injili ya Yesu Kristo, yaani Habari Njema ya Ufalme wa Mbinguni, ilikosa katika ujumbe wake, mauti ya Msalaba, kama sehemu muhimu ya ujumbe huo. Tangu mwanzo mwa huduma yake, ujumbe wa Yesu ulikuwa “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia” (Mathayo 4:17).

Vitabu vyote vya historia ya huduma ya Yesu Kristo (Mathayo, Marko, Luka na Yohana), vinamwonyesha Yesu Kristo na wanafunzi wake wakiwa na ujumbe kwa wana wa Israeli ukiwaandaa kwa ajili ya kuupokea ufalme wa mbinguni ambao ulikuwa unawajiria punde na kwamba ujumbe huo haukuwa kwa ajili ya mataifa (gentiles) ambao hawakuwa sehemu ya Taifa teule na Waisraeli na hawakuwa na Mungu duniani (Waefeso 2:11-12).

Mathayo 10:1-8 kwa mfano, tunamwona Bwana Yesu akiwaita wale wanafunzi wake 12 na kawapa amri juu ya pepo wachafu na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Lakini pia akawaagiza wasiende katika njia ya mataifa na akawapa ujumbe wa kusema kwa “hubirini mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia” (mstari wa 7).

Muda ulipowadia Yesu alianza kuwafunulia wanafunzi wake juu ya kifo chake, lakini hawakumwelewa kwa kuwa kwao ilikuwa na Injili nyingine, tofauti na ile walifundishwa na Bwana Yesu mwenyewe na kuwatuma sehemu sehemu kuihubiri. Angalia Mathayo 16:21-23, Petro anaonekana akimkemea Yesu pale tu alipowaambia kwamba imempasa kufa, na Yesu naye akamwona Petro anataka kutumika na shetani kuzuia kusudi la Mungu kwake! Soma pia, Marko 9:9-10; 9:31-32 na Luka 9:44-45; 18:31-34.

Katika mistari yote hiyo, wanafunzi wa Yesu wanaonyesha kutokuelewa kabisa pale Bwana Yesu anapouzungumzia Msalaba kama njia pekee ya ukombozi kwa wanadamu kuanzia na Mwisraeli.

Kufumbwa huko kwa ufahamu wao tunaona unaendelea hata baada ya Yesu kufufuka katika wafu. Bado kulikuwa na wingu nzito kwenye fahamu zangu na hilo lilimfanya Yesu awafafanulie UPYA maandiko yaliyomhusu Yeye, tangu Torati ya Musa, Manabii na Zaburi mambo yaliyoandikwa kumhusu Yeye kwamba atakufa na kufufuka kwa ajili ya dhambi ya ulimwengu. (Luka 24:25-26; 24:44-46).

Marko16:15-20 tunaona Yesu anawapa wanafunzi wake agizo kuu la kwenda ulimwenguni mwote, kuihubiri Injili kwa kila kiumbe, na kwenye ule msitari wa 20 maandiko yanasema ‘nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote’. Lakini ‘kotekote’ yao ilikuwa bado ni kwa wayahudi kama walivyoagizwa pale mwanzo kabla ya Yesu kusulubiwa (Matendo 11:19 – wasilihubiri lile neno isipokuwa kwa Wayuhudi peke yao). Ikumbukwa hii ni baada ya Stefano kupigwa nawe na kuuwawa (Matendo 7) na kulifanya Taifa la Israel kumkataa Masihi wao (Yesu Kristo) mara ya tatu. Kwa sababu hiyo, Mungu akawageukia mataifa, Warumi 11:11-14:

“Hivyo nauliza tena, je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu. Basi ikiwa kujikwaa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi. Sasa ninasema nanyi watu Mataifa. Maadam mimi ni mtume kwa watu Mataifa, naitukuza huduma yangu ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao”

Na ndipo Bwana, kwa neema yake, akamwokoa Sauli (Paulo) katika Matendo 9 kwa ajili ya kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu kwa mataifa kama alivyojieleza mwenyewe katika Matendo 26:12-18, ndiyo Injili pekee ambayo mataifa tunatakiwa tuifuate katika kipindi hiki cha neema ya Bwana:

“Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nikiwa na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. Ilikuwa yapata adhuhuri, Ee, Mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, iking’aa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’ “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’ Naye Bwana akajibu, “Ni Mimi Yesu unayenitesa. Lakini sasa inuka usimame, kwa miguu yako, kwa sababu nimekutokea kwa kusudi hili ili kukuweka utumike na kushuhudia juu ya mambo ambayo umeyaona na yale nitakayokutokea kwayo. Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, uyafungue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni na kutoka kwenye nguvu za shetani, wamgeukie Mungu ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini Mimi.’

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *