Je ni wapi uanzie kusoma Biblia
Kwanza ni muhimu kutambua kwamba Biblia si kitabu cha kawaida ambacho husomwa tu toka ukurasa moja mpaka mwingine kama vile visomwavyo vitabu vya hadithi au riwaya. Ni vyema kutambua pia kwamba Biblia ni kama maktaba au kusanyiko la vitabu vilivyoandikwa na waandishi mbalimbali katika lugha tofauti kwa kipindi cha zaidi ya miaka 1,500. Ni vyema pia kujua kwamba Biblia ni kitabu chenye ujumbe mmoja tu kwa sababu historia yote ya Biblia na unabii wake unalenga kumtambulisha Yesu na mwishowe unakamilika katika Yesu. Kwa hiyo, msomaji anayeanza kusoma kwa mara ya kwanza Biblia inashauriwa kuanzia na Injili. Injili ya Marko ni ya haraka na ina ufahamu wa kutosha na ni sehemu nzuri ya kuanzia. Baada ya hapo unaweza endelea na Injili ya Yohana, ambayo inaangazia katika mambo yote Yesu aliyosema juu yake mwenyewe. Marko anaeleza juu ya yale yote Yesu aliyofanya, wakati Yohana anaeleza kuhusu kile Yesu alichosema yakuwa yeye alikuwa nani. Katika Injili ya Yohana kuna baadhi ya vifungu ambavyo ni rahisi na wazi, lakini pia baadhi ya vifungu vya ndani sana na vizito zaidi. Kusoma vitabu vyote vya Injili (Mathayo, Marko, Luka, Yohana) kutakufanya uweze kuifahamu vizuri historia ya maisha ya Yesu na huduma yake.
Baada ya hapo, soma Nyaraka pamoja na Metendo ya Mitume, maana vitabu hivi vinatufundisha jinsi ya kuishi maisha yetu kwa njia ambayo ni ya kumheshimu Mungu tukiongozwa na Roho Mtakaifu. Nyaraka hasa zinalenga kulifundisha Kanisa la Kristo na kuliwekea misingi ya namna ya kuendea wokovu wetu. Unapoanza kusoma Agano la Kale, soma kitabu cha Mwanzo ambacho kinatuonyesha jinsi Mungu alivyoumba ulimwengu na jinsi watu walivyoanguka katika dhambi, na athari za anguko hilo zilivyokuja juu ya dunia.
Vitabu vya Kutoka, Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati vinaweza kuwa vigumu kusoma kwa sababu vinahusisha sheria zote ambazo Mungu alihitaji Wayahudi kuishi kwayo. Hupaswi kuepuka kuvisoma vitabu hivi, kama huvielewi ni bora zaidi ukaviacha kidogo ili uvirejelee baadaye na kuvisoma upya katika macho ya ufunuo wa Agano Jipya. Katika hali yoyote ile ni vyema uwemakini usije kujikuta umekwama kwenye vitabu hivyo.
Soma kuanzia kitabu cha Yoshua mpaka Mambo ya Nyakati ili uweze kuelewa vizuri historia ya Israeli. Soma vitabu vya Zaburi mpaka Wimbo Ulio Bora uweze kupata mashairi ya Kiebrania yenye hekima na yanayogusa hisa. Vitabu vya unabii, Isaya hadi Malaki, vinaweza kuwa vigumu pia kuvielewa lakini, kumbuka jambo la muhimu katika kusoma na kuielewa Biblia ni kuomba hekima ya Mungu (Yakobo 1:5). Mungu ndiye mwandishi wa Biblia, na anataka wewe na mimi wote tulielewe vizuri neno lake. Ni muhimu pia kujua kwamba si kila mtu anaweza kuwa mwanafunzi bora wa Biblia. Ni wale tu wenye kujinyenyekeza kwa Roho Mtakatifu ndio wanao kuwa na sifa ya kulisoma neno la Mungu na kuweza kulielewa kwa neema za Mungu :
Je, umeokolewa kwa imani katika Yesu Kristo (1 Wakorintho 2:14-16)? Je, una njaa ya neno la Mungu (1 Petro 2:2)? Je, unayachunguza maandiko kila siku kwa bidii (Matendo 17:11)? Kama jibu lako ni ndiyo kwa maswali hayo yote matatu, unaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu atabariki jitihada zako za kutaka kumjua Yeye pamoja na Neno lake, haijalishi ni wapi utaanzia wala mtindo wako wa usomaji. Kama wewe huna uhakika kuwa ni Mkristo – YAANI umeokolewa kwa imani katika Kristo Yesu na Roho Mtakatifu yuko ndani yako – utaona ni vigumu sana kwako kuelewa maana halisi ya maandiko. Ukweli wa Biblia umefichwa kwa wale ambao hawajaujilia wokovu kwa imani katika Kristo, lakini ni uzima kwa waaminio (1 Wakorintho 2:13-14, Yohana 6:63).
Leave a Reply