Home 2020 February 03 Je, Ni njia gani nzuri ya kusoma Bibilia?

Je, Ni njia gani nzuri ya kusoma Bibilia?

Je, Ni njia gani nzuri ya kusoma Bibilia?

Kupata maana halisi ya maandiko ni mojawapo ya jambo muhimu sana kwa kila mwamini na mfuasi wa Bwana wetu Yesu Kristo katika safari yake ya wokovu. Mungu ametuagiza kwamba ni lazima tusome vyema Biblia na pia tuweze kulitumia kwa usahihi neon la kweli (2 Timotheo 2:15). Kuisoma Bibilia inavyotakikana si jambo jepesi na pia kuyapitia maandiko juu juu huweza kuwa ni sababu ya kutoa tafsiri isiyo sahihi. Kwa hivyo, ni muhimu kuelewa mambo muhimu kwa kupata maana kamili na iliyo sahihi ya maandiko.

Kwanza, mwanafunzi wa Bibilia lazima aombe na kumruhusu Roho Mtakatifu ampe uwezo wa kuelewa, kwa maana hiyo ndiyo kazi yake. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote akatakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.(Yohana 16:13). Kama vile Roho Mtakatifu alivyowaongoza wanafunzi wa Yesu kuandika Agano Jipya, vilevile atatuongoza kuyaelewa maandiko. Kumbuka, Bibilia ni kitabu cha Mungu, na inatupasa kumuuliza Yeye ni nini hasa kitabu hicho kinamaanisha. Kama wewe umeokoka na unamwamini  Yesu Kristo, mwandishi mkuu wa Bibilia, Roho Mtakatifu, anakaa ndani yako, na yeye anataka wewe uelewe, na yuko tayari kukuelekeza kile alichokiandika kwenye hiyo Biblia.

Pili, usichukue mstari mmoja wa Biblia na kuutafsri kipekee bila kupata hasa maana ya sura nzima inahusu nini (Context), Kila mara lazima usome sura nzima ili kuweza kujua maana halisi ya mstari husika. Pamoja na kwamba maandiko yote yanatoka kwa Mungu (2 Timotheo 3:16; 2 Petero 1:21), Mungu lakini aliwatumia watu kuandika. Hawa watu walikuwa na maudhui ya kuandika katika akili zao, lengo la kuandika, na walikuwa wakitatua hali fulani iliyowazunguka.

Pia ni muhimu tusome historia ya kitabu husika cha Bibilia, ili tupate kujua ni nani alikiandika kitabu hicho, kiliandikwa lini na katika mazingira gani, aliwaandikia akina nani, na ni kwa nini alikiandika au sababu za kuandikwa kitabu husika. Vile vile ni vyema sana tukiyaacha maandiko yajieze yenyewe kwani, mara nyingi sana, watu wanaweka maana zao au tafsiri zao katika maandiko ili watimize makusudi yao nje ya kusudi halisi lililolengwa na Roho wa Mungu katika uandishi wa msitari husika.

Tatu, tusipendi kujitenga au kujisomea peke yetu maandiko ya Mungu, ni vyema tukisoma katika vikundi au jumuiya. Ni kupungukiwa kufikiri kwamba hatuwezi kupata chochote kutoka kwa watu wengine wanaoisoma Bibilia kama sisi. Roho Mtakatifu amewapa watu karama mbalimbali katika mwili wa Kristo. Mojawapo ya karama hizo ni ile ya ualimu (Waefeso 4:11-12); 1 Wakorintho 12:28). Hawa walimu wamepewa na Mungu uwezo wa kuyaelewa maandiko na kuyafundisha kwa wengine. Kwa kujitenga peke yako, unaweza usiwe na karama hiyo na hivyo ukakosa msaada muhimu sana katika kuyapambanua maandiko. Kwahiyo, ni njia ipi bora ya kuisoma Bibilia? Kwanza, kupitia maombi na unyenyekevu, lazima tumtegemee Roho Mtaktifu atupe uwezo wa kuelewa. Pili, lazima tuisome katika mkutadha wa ujumbe, tukitambua kwamba Bibilia yajieleza. Tatu, lazima tuheshimu juhudi za Waamini wengine, waliopita na waliopo, ambao wamejaribu kuisoma Bibilia. Kumbuka, Mungu ndiye mwandishi wa Bibilia na anataka tuielewe vyema.

Author: magebo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *