Tunda la Neema
Wakati Yohana Mbatizaji na Bwana Yesu Kristo walipoonekana duniani, watu wa Mungu walikuwa chini ya sheria ya Musa kwa kipindi cha takribani miaka elfu moja na mia tano. Haishangazi kwamba Yohana na Bwana Yesu walitarajia kuona matunda kati yao.
Wakati viongozi wanafiki wa kidini walipokuja kuungana na wasikilizaji wa Yohana Mbatizaji waliokuwa wakiongezeka na kuomba kubatizwa, Yohana aliwaita “kizazi cha nyoka” na kuwaamuru “walete matunda yanayostahili toba” (Mathayo 3:7-8). Toba ya kweli, pamoja na matunda yenye kuthibitisha hilo, ilikuwa ni mahitaji ya kimsingi ya ufalme ambao Yohana alikuwa akiutangaza. Hili ni dhahiri kutokana na tangazo lake katika Mathayo 3:10:
” Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
Bwana wetu naye alitokea, akitangaza ujumbe ule ule kama Yohana, na pia akatafuta matunda kati ya watu wake (Mathayo 7:16-20; 21:33-43).
Tunajua, hata hivyo, kwamba Yohana Mbatizaji alikatwa kichwa na Bwana wetu Yesu Kristo akasulubiwa. Matunda yaliyotengenezwa chini ya Sheria yalikuwa madogo kweli kweli. Hata baada ya kufufuka kwa Yesu Kristo watu wake wengi walikataa kutubu na walishindwa kuzaa matunda yaliyohitajika.
Lakini kile Sheria inachokitaka, neema hukitoa! Ilikuwa ni wakati huu ambapo Mungu alimwinua Mtume Paulo, ambaye “mahubiri ya msalaba” yalionyesha kwamba Kristo hakuwa amekufa kifo cha mapema (kabla ya wakati), bali kwa upendo usio na kipimo alikuja ulimwenguni kuwafia wenye dhambi ili waokolewe kwa neema, kwa njia ya imani (Waefeso 2:8-9). Ujumbe wa Paulo uliitwa “injili [habari njema] ya neema ya Mungu” (Matendo 20:24), na pale ambapo Sheria ilishindwa kuleta matunda, neema ilizaa sana – ilileta matunda mengi zaidi.
Neema ya Mungu katika Kristo, inapopokelewa kwa imani ya kweli, huzaa matunda mema kila wakati. Kwa sababu hiyo Paulo aliwaandikia Wakolosai kwamba habari yake njema ilikuwa ikienea ulimwenguni kote, kwa kusema maneno haya:
“Kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli” (Wakolosai 1:5-6)
Kubali ujumbe wa neema ya Mungu, mtegemee Kristo kama Mwokozi wako na atakusaidia kuzaa matunda mema.
Kwa utukufu wa JINA, lipitalo majina yote!
Leave a Reply