Kwanini Paulo?
KWANINI MTUME PAULO?
Kuna mabishano mengi juu ya uwepo au umuhimu wa Mtume Paulo kwenye Biblia na hasa pale anapopewa umuhimu pengine kuliko Mtume Petro ambaye wengine wanadai au wanamwona kama ndio msingi wa Imani yetu kinyume na Mtume Paulo kwa maana Kanisa la Kristo limejengwa kwake!
Ni vyema kabla sijazungumza mengi yanayomhusu Mtume Paulo, ngoja nijaribu kwanza kuonyesha baadhi ya ‘ukweli’ unaomhusu (facts):
- Aliitwa kwa wito maalumu kwamba akawe mtume wa Yesu Kristo kwa Mataifa (Matendo 9:1-28; 22:1-21; 26:4-23)
- Alifunuliwa siri (mystery) kwamba Mataifa nao ni warithi (Efeso 3:1-9)
- Aliyatimiza kwenye mwili wake yale yaliyopungua kwenye mateso ya Kristo (Wakolosai 1:24 – 27)
- Ni Mtume wa kwanza kuandika Kitabu katika Agano Jipya (Wagalatia 47 AD, na sio vitabu vya Injili ya Mathayo, Marko, Luka na Yohana kama wengi wanavyodhani)
- Ni Mtume pekee aliyefanya safari za kimisionari kuyaendea mataifa mara tatu (Matendo 13 – 14; 15:36 – 18:22; 18:23 – 20:38)
- Ameandika 52% ya Agano Jipya, 21% ya Biblia yote (Vitabu 14 kati 66)
- Ameandikwa mara 186 (Sauli 23, Paulo 163) dhidi ya Petro 162. Kwenye Matendo ya Mitume, Paulo ameandikwa mara 153, Petro mara 57 tu!
- Mtume pekee aliyethibitishwa na Mtume mwezake ( 2 Petro 3:15 – 16)
- Ni mtume pekee aliyekataa kula sadaka (Matendo 20:35, 1 Wakorintho 9:12 – 15)
Angalizo: Ikumbukwe kwamba Nyaraka za Mtume Paul ni maandishi ya awali kabisa kwenye Agano Jipya, kinyume na wengi wanavyojua, na kwamba Nyaraka au Barua za Kichungaji za Mtume Paulo ambazo alizituma kwenye makanisa aliyoyafungua kuonya au kujibu hoja fulani zilizoibuka kwenye makanisa hayo, ziliandikwa mapema kabla ya Injili zile nne na Kitabu cha Matendo ya Mitume kuandikwa. Ukweli huu unapingana na mpangilio wa sasa ya Vitabu vya Agano Jipya ambapo watu wengi hudhani au huamini kwamba mpangilio wa sasa unaendana na tarehe za uandishi wa vitabu hivyo. Inaaminika kwamba hata waandika Injili, walifanya hivyo baada ya kusoma maandishi ya Mtume Paulo na hata neno ‘INJILI’ (Euangelion) lilitumika kwa mara ya kwanza katika maandiko na Mtume Paulo, yeye peke yake akilitumia mara 69 kati ya mara 104 neno lilipotumika katika Biblia.
Hakuna sehemu nzuri ya kuanza kuandika au kuilezea habari ya Mtume Paulo Zaidi ya historia yake na hasa kuanzia pale alipoonekana kwenye maandiko kwa mara ya kwanza. Lakini ikumbukwe historia ya Mtume Paulo imeandikwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume na Luka, ambaye pia ndiye aliyeandika kitabu cha Injili ya Luka. Mara ya kwanza, Paulo (Sauli) anaonekana kwenye Matendo ya Mitume 7:58-60 akiwa mmoja wa mashaidi wa kuuawa kwake Stefano. “wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.” Kuona vema kwa Sauli kwa tukio la kuuawa kwa Stefano maana yake ni kwamba yeye alilibariki tukio lile kwa maana alikuwa mstari wa mbele katika kulipinga Kanisa la Bwana.
Kuitwa kwake:
Luka ametoa ushuhuda wa kuitwa kwa Mtume Paulo na Bwana Yesu, kwa sababu maalumu, mara tatu kwenye kitabu chake cha Matendo ya Mitume:
“Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua apate kulichukua jina langu mbele ya Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya jina langu.” (Matendo 9:15-16)
“Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake. Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia. Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita jina lake.’ “Baada ya kurudi Yerusalemu, wakati nikiwa ninaomba hekaluni, nilipatwa na usingizi mzito nikamwona Yesu akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu mimi.’ “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyokwenda kwenye kila sinagogi ili kuwatia gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. Wakati damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomwua’. Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ” (Matendo 22:14-21)
“Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’ “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’ Naye Bwana akajibu, “ ‘Ni Mimi Yesu unayenitesa. Lakini sasa inuka usimame, kwa miguu yako, kwa sababu nimekutokea kwa kusudi hili ili kukuweka utumike na kushuhudia juu ya mambo ambayo umeyaona na yale nitakayokutokea kwayo. Nitakuokoa kutoka kwa watu wako, na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, uyafungue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni na kutoka kwenye nguvu za shetani, wamgeukie Mungu ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini Mimi.” (Matendo 26:14-18)
Ushuhuda wake wenyewe:
“Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo. Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa Kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilikuwa na bidii kubwa katika desturi za baba zangu. Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu ye yote, wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski. Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa na nilikaa naye siku kumi na tano. Lakini sikuwaona mitume wengine wowote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo. Baadaye nilikwenda sehemu za Syria na Kilikia. Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo. Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akitaka kuiangamiza.” Kwa hiyo wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu. (Wagalatia 1:11-24)
Katika maandiko yote haya, kuna jambo moja la msingi linalojirudia, ya kwamba wito wa kuitwa kwake ilikuwa ni kwa ajili ya watu wa mataifa, ambao kutokana na Waefeso 2:11-12, ni watu ambao walikuwa wamefarakanishwa na jamii ya Israeli, ni watu waliokuwa wamekosa tumaini, hawakuwa na Mungu duniani!
Leave a Reply