Home 2024 September 07 DUMU KATIKA HAYO…!!!

DUMU KATIKA HAYO…!!!

DUMU KATIKA HAYO…!!!

“Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. BALI WEWE UKAE KATIKA MAMBO YALE ULIYOFUNDISHWA NA KUHAKIKISHWA, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao” (2 Timotheo 3:13-14).

Haya yalikuwa ni miongoni mwa maneno ya mwisho ya Mtume mkuu Paulo, yaliyoandikwa katika mtazamo wa kukaribia kwake kufa kishahidi, kwa Timotheo, mwanawe mpendwa katika imani.

Hali, kwa nje, haikuwa ya kutia moyo. Ilionekana kwamba siku za mwisho za kipindi cha neema kwa hakika zilikuwa karibu kutimia. Mtume mkuu Paulo, mpaka wakati huu, alikuwa amevumilia “mateso” na “adha” nyingi na sasa “alikuwa akipata taabu, kama mtenda mabaya, hata kufungwa”. Kulikuwa na wale ambao, kama Yane na Yambre, walikuwa “wanaipinga kweli” (Mstari wa 8). “Iskanda, mfua shaba, alionyesha “ubaya mwingi” na “alikuwa akiyapinga maneno yake” (2 Timotheo 4:14-15); Na “watu waovu na wadanganyifu” walikuwa wameinuka kila upande na “walizidi kuwa waovu zaidi, wakidanganya na kudanganyika” (2 Timotheo 3:13).

Kulikuwa na uasi hata miongoni mwa ndugu zake katika imani, kiasi kwamba sasa, kutoka katika gereza lake la Kirumi, ilimbidi kutoa taarifa kuwa: “Wote walio wa Asia waliniepuka…; Dema ameniacha…; Luka peke yake yupo pamoja nami” (2 Timotheo 1:15; 4:10-11).

Na sasa je, shauri lake la kuaga ni lipi kwa kijana wake Timotheo? Je, anasema: “Labda nimekuwa mkali sana; Au mbinu zangu za huduma zimetengeneza maadui wengi? Au pengine anamshauri Timotheo awe wa kidiplomasia zaidi na awe mvumilivu zaidi kuliko alivyo kuwa yeye?” Hata Kidogo! Kwa kuwa kumbukumbu za Kibiblia zinaonyesha kwamba Mtume Paulo alikuwa ni miongoni mwa watu mwenye busara na mwenye ujuvi mwingi. Mateso yake hayakuwa ni matokeo ya roho ya ugomvi, bali yalitokana na uaminifu wake katika kutangaza ujumbe ule ambao unamfedhehesha na kumkasirisha sana “adui yetu Ibilisi”, ujumbe ambao ni jibu la neema la Mungu kwa mahitaji ya mwanadamu na pia mi jibu la Mungu kwa uchongezi wa Shetani – “INJILI YA NEEMA YA MUNGU”.

Hivi ndivyo ni Mtume Paulo anavyomhimiza Timotheo, kwamba: “ENDELEA… USIONE HAYA… UWE HODARI”. Mtume Paulo alijua vyema kwamba, katika ulimwengu huu uliolaaniwa na dhambi, tumaini pekee la mtu binafsi ni ‘kupatikana’ katika toleo la Mungu la wokovu kupitia imani katika ukombozi uliofanywa na Kristo pale Kalvari.

Utukufu una Yeye KRISTO YESU Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *